MACHINGA COMPLEX KUDORORA, SABABU ZATAJWA. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MACHINGA COMPLEX KUDORORA, SABABU ZATAJWA.

Jengo la Machinga complex
“………….Tunakuja kwenye maswala mengine tukiangalia biashara ndogondogo, wamachinga, wafanyabiashara ndogondogo, wanaohamahama, leo wapo hapa na kesho wamehamishiwa sehemu nyingine, lakini tazama, katika yale maeneo ambayo wamekuwa wakihamishiwa, utakuta kwamba wanahamishiwa kwenye maeneo ambayo ni vigumu kupanua soko, inamaana kwamba unaziweka bidhaa zao katika maeneo ambayo hazina uwezo wa kuwavutia wateja, hivyo hawawezi kupanua mgawo katika soko la bidhaa zao.

Mwishowe watu hurudi tena katika maeneo yaleyale waliyotakiwa kuondoka na mfano mzuri ni Machinga Complex, Jengo la Machinga complex ni jengo lililojengwa vizuri sana na unajua  kama watu wangeweza kwenda na kufanya biashara pale, pangeliweza kuwa ni mahali panapofaa sana lakini kinachoonekana sasa ni ukosefu wa wateja wa kutosha  na hii ndiyo sababu unaona watu wanazidi kungangania pale viwanja vya Karume, na hilo ni tatizo jingine, na serikali inaposema ni lazima wahame pale inakuwa ni tatizo pia……….”

Hiyo ilikuwa ni sehemu  ya mjadala uliofanyika wiki jana kati ya Mtaalamu wa biashara kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam, School of Business Administration Dr.Francis Michael na Radio ya taifa TBC International, juu ya Namna ya kuanzisha biashara.


Dr. Francis alifafanua maswala mengi na kuhusiana na hili la Machinga comlex alisema kwamba wote, serikali na wananchi kila mmoja anastahili kulaumiwa, wananchi ni kutokana na kutokuwa na utashi wa akili wa kuhamia katika jengo hili na serikali kwa upande wake kushindwa kujenga soko katika eneo ambalo kila upande wateja na wamachinga wataridhika. Akitolea mfano alisema kwamba kwa mfano jengo kama hilo lingejengwa sehemu kama Ilala unafikiri watu wasingelikwenda pale?, mbona ilala pana vibanda na watu wanakwenda?;

Alisema kuhamia Machinga complex ni mchakato unaohitaji muda mrefu na haiwezekani, wamachinga wengine wana mikopo taasisi za fedha, kwenda kujitoa muhanga pale huku taasisi hizo zikija kuchukua dhamana zao walizoziweka ndiyo maana wanaamua kurudi kariakoo na kwingineko kwenye soko la uhakika. “Siyo swala la kwenda kuwabwaga sehemu nyingine tu na kuwaacha ambapo hawawezi kufanya biashara”

Kuhusiana na Namna ya kuanzisha biashara, alisema, vitu muhimu mtu unavyotakiwa kuangalia ni hivi hapa.;
·        Wazo zuri la biashara,
·        Watu au timu utakayofanya nayo biashara.
·        Utafiti wa soko, hata mdogo tu wa biashara unayotaka kufanya.
·        Maswala ya uendeshaji na
·        Maswala ya fedha za kuanzia.

Aliulizwa pia tofauti iliyokuwepo kati ya Makampuni yenye dhima ya ukomo Limited Company na yale yasiyokuwa na dhima ya ukomo  na jinsi ya kusajili akasema kwamba tofauti kubwa ipo katika maswala ya kisheria zaidi na mtu unapoanzisha biashara siyo lazima usajili kampuni, Limited, itategemea na aina ya biashara, nyingine mtu hata unaweza kufanya hata pasipokusajili kampuni wala leseni.

Alipoulizwa ni vipi vijana wasiokuwa na ajira wala dhamana yeyote na wanahitaji kipato  watakavyoweza kukopa mikopo midogo midogo, alisema kwamba hilo nalo ni tatizo jingine na wengi wao hawana uelewa ni kitu gani wanachotaka kufanya katika biashara. Kabla hata ya mtu hujaja katika maswala haya ya kupata mtaji  unatakiwa ujiangalie mwenyewe ni kitu gani unachoweza kukifanya, una uzoefu na nini, pengine umewahi kufanya kazi fulani kwa ndugu na jamaa, tumia uzoefu ule ule kuanza biashara yako.

Kitu kingine alisema wanatakiwa wafanye utafiti kujua soko lao ni lipi, “Huwezi ukamuuzia kila mtu, ni lazima ulenge soko linaloendana na biashara yako ”. Alimalizia kwa kusema kuwa changamoto za kupata mikopo sasa zimeanza kupata dawa kwani serikali imeanzisha utaratibu wa kuzitambua dhamana mbalimbali zilizoko maeneo yasiyokuwa rasmi au kupimwa. Vile vile taasisi ndogondogo nyingi za fedha zimeibuka zinazotoa mikopo ya masharti nafuu kama kutumia vitu na samani za ndani kama dhamana, na mikopo ya vikundi.

Mfanyabiashara katika jengo la Machinga Complex akisubiri wateja huku akiwa  amesinzia.
Alisema pia kwamba, siyo sahihi mtu kulipa kodi ya mapato kabla hajaanza kufanya biashara. Maafisa wa TRA wanaofanya hivyo hufanya kinyume cha utaratibu kwani kodi hutokana na faida, “Hii husababisha watu wengi kukwepa kodi” alisema.

Vikwazo watu wanavyokutana navyo wanapoanzisha biashara alibainisha kwamba ni pamoja  na kushindwa kufahamu soko la biashara zao, “Kusema kila mtu ni mteja wako ni tatizo” Kingine ni matarajio yasiyokuwa sahihi, matarajio ya juu sana au ya chini mno hayafai; Kukopi biashara, kwa mfano unaona mwenzako kafungua saluni na wewe unafanya hivyo hivyo pasipo kufanya utafiti kujua soko, mikakati na mahitaji yakoje. Kikwazo kingine ni tabia ya kushindwa kujitofautisha na biashara, “una duka nyumbani, ukihitaji kiberiti, sijui mshumaa, unakwenda kujichukulia tu bila ya kulipa”  Alisema hivyo siyo sahihi.

Na mwisho alitaja, kushindwa kutumia mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa. “Kwa mfano mtu anachukua milioni tano benki kabla ya kwenda kuingiza kwenye biashara kwanza anachukua hapo milioni tatu anaenda kuanzia nyumba yake, milioni mbili zinazobakia haziwezi kutosha kuifanya biashara isimame na mwisho wake itakufa.”

VYANZO
HABARI  : TBC Iternational.
PICHA     : Kutoka kwenye blogu ya mambobado.blogspot.com na nifahamishe.com


0 Response to " MACHINGA COMPLEX KUDORORA, SABABU ZATAJWA."

Post a Comment