Tukio hilo lilitokea juzi saa
nne asubuhi baada ya majirani zake kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Kiwanja cha Ndege, Dia Zongo kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya
boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.
Zongo alisema majirani hao
walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa
nje.
Baada ya kupata taarifa hizo,
Zongo alimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu Mgagala na kuongozana naye hadi
kwenye nyumba hiyo na kumhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa akijibu kwa
kubabaika.
Moja ya maswali aliyoulizwa ni
idadi ya watoto wake na akajibu kuwa ana wawili lakini wakati akiendelea kujibu
maswali, ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa
wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na kumkuta
mtoto Nasra akiwa ndani ya boksi.
Ofisa mtendaji huyo alisema
wakati wakimtoa mtoto huyo ndani ya nyumba, kundi kubwa la watu waliokuwa na
fimbo na mawe walianza kumshambulia mwanamke huyo na kumlazimu mtendaji kutoa
taarifa polisi.
Alisema muda mfupi baadaye,
polisi waliwasili na kumkamata Mariam na kumpeleka katika ofisi ya kata ambako
aliwekwa chini ya ulinzi.
Baadaye aliwekwa rumande
katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa
Jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Leonard Paulo alisema wanaendelea kukusanya taarifa za tukio hilo
ikiwamo matokeo ya vipimo vya madaktari kuhusu afya ya mtoto huyo kabla ya
kuchukua hatua zaidi.
Kamanda Paulo alisema
watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa kosa la kumfanyiwa mtoto vitendo vya kikatili.
Hata hivyo, kamanda huyo
alisema polisi wanakadiria kwamba mtoto huyo alianza kufichwa kwenye boksi hilo
akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu.
Utetezi wa Mariam
Akijibu maswali ya polisi,
mwanamke huyo alikiri kuanza kumlea mtoto huyo tangu akiwa na umri wa miezi
tisa baada ya mama wa mtoto huyo kufariki dunia mwaka 2010.
Pia mtuhumiwa alikiri kwamba
mtoto huyo hajawahi kupewa chanjo yoyote wala kupelekwa kliniki.
Alikuwa akitoa maelezo hayo
huku akiwa amemshikilia mtoto huyo aliyetapakaa uchafu ikiwamo haja kubwa na
ndogo alizokuwa akitoa ndani ya boksi na kusema kwamba mara ya mwisho
alimwogesha Julai mwaka jana.
Pia alisema alikuwa akimwekea
chakula na maji ndani ya boksi lililokuwa nyuma ya mlango wa chumba.
Mume wa mwanamke huyo, Mtonga
Ramadhani anayefanya biashara katika Soko la Mawenzi, Morogoro ambaye pia
anashikiliwa na polisi, alidai kuwa hakuona sababu ya kutoa taarifa za kufichwa
kwa mtoto huyo kwa sababu hamhusu na wajibu wake ni kutafuta chakula.
Alivyonaswa
Baadhi ya majirani wa mwanamke
huyo ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema Mariam alihamia katika nyumba
hiyo mwaka 2010 na hawajawahi kumwona mtoto huyo akitolewa nje wala kufanyiwa
usafi.
Walisema mtoto huyo alibainika
baada ya kusikika akikohoa na kulia nyakati za usiku, jambo lililozua wasiwasi
kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa mshirikina anayefuga misukule.
Baba wa mtoto
Baba mzazi wa mtoto huyo,
Rashid Mvungi alisema hakujua kama mwanaye alikuwa analelewa katika mazingira
hatarishi.
Akihojiwa na Ofisa Ustawi wa
Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu, Mvungi alisema alimzaa mtoto huyo
nje ya ndoa na amekuwa akituma fedha za matumizi kwa mama yake mkubwa.
Mvungi ambaye ni mtumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, alisema baada ya mzazi mwenzake kufariki
dunia alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke.
Alisema hata hivyo,
alikubaliana na upande wa familia ya marehemu kuwa mtoto huyo alelewe na mama
yake mkubwa.
Mtoto azungumza
Wakati Mvungi akihojiwa,
baadhi ya watu waliofurika katika Ofisi za Ustawi wa Jamii walianza kuangua
kilio baada ya mtoto huyo anayeonekana mlemavu kuanza kujibu maswali aliyokuwa
akiulizwa na maofisa wa Ustawi wa Jamii.
Swali: Unaitwa nani:
Jibu: Naitwa Nasra
Swali: Ulikuwa unapewa chakula
gani?
Jibu: Ubwabwa na maharage
Swali: Una umri wa miaka
mingapi?
Jibu: Miaka minne
Swali: Baba yako yuko wapi?
Jibu: (anamwonyesha kwa
kidole)
Ngungamtitu alisema huenda
ulemavu wa mtoto huyo umetokana na kuishi kwenye boksi au kukosa lishe yakiwamo
maziwa ya mama, hewa safi na upendo.
Alisema si ajabu mtoto huyo
kushambuliwa na magonjwa mbalimbali kama minyoo, pneumonia, utapiamlo na
malaria, ndio maana aliagiza apelekwe katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi,
chanjo na tiba.
Ofisa huyo alisema matibabu
mengine atakayopatiwa ni pamoja na kunyooshwa viungo, mikono na miguu
iliyolemaa.
Ngungamtitu aliwaomba
wasamaria wema, mashirika ya dini na wadau mbalimbali kutoa misaada ya nguo,
lishe, matibabu na mahitaji mengine kwa mtoto huyo.
HABARI HII IMETOKA GAZETI LA MWANANCHI.
0 Response to "BINADAMU TUNATISHA HERI HATA WANYAMA, MTOTO HUYU KOSA LAKE NI NINI?"
Post a Comment