Chupa za maji ya kunywa zilizokwishatumika, juisi na hata
makopo na mikebe mbalimbali ya bidhaa zilizokwishatumika mara nyingi hutupwa
katika majaa na kisha baadae huchukuliwa na mamlaka husika kwa ajili ya kwenda
kutupwa kwenye madampo makubwa ya takataka
katika miji na majiji mbalimbali.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni baada ya ongezeko kubwa
la viwanda vya kutengeneza maji ya kunywa na vinywaji baridi, kumekuwa na
uhitaji wa kuzirudisha tena viwandani chupa hizo(recycling) kusudi ziweze
kutumika tena na tena kama njia mojawapo ya kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Chupa hizi na mifuko ya nailoni baada ya kukusanywa na kurudishwa viwndani, huchambuliwa,
kuoshwa, kusagwa na hatimaye kuyeyushwa tena kwa ajili ya kuunda chupa au
vyombo vingine vya plastiki.
Mchakato huo wote huhitaji watu wa kukusanya chupa hizo
mitaani, kazi ambayo watu wengi wamekuwa wakiifanya kwa ujira kidogo, kwa
wastani chupa kiasi cha kilo moja huuzwa siyo zaidi ya shilingi 150 mpaka 200.
Unaweza kukuta mtu kafungasha furushi kubwa la chupa lakini akikuambia kiasi
cha fedha atakachokwenda kupata utashangaa.
Hata hivyo ukizingatia kwamba gharama
wanayotumia kuzipata ni kidogo na sana sana utakuta ni ule muda wao wanaoutumia
tu, basi kiasi hicho cha fedha wanachopewa ni haki wala hawadhulumiwi. Ujira
kidogo unaotokana na shughuli hii umesababisha ionekane na baadhi ya watu kuwa ni kazi “kichaa” isiyolipa na inayostahili
kufanywa na wale wenye ugonjwa wa akili tu. Hata wengine hudiriki kusema kwamba
kila anayeokota chupa(makopo) basi ni sharti avae ‘maguo’ machafumachafu.
Nilikuwa miongoni mwa watu wanaoamini kauli hizo hasi lakini
siku moja kwa mshangao mkubwa nilijikuta nabadilisha kabisa mtazamo wangu juu
ya kazi hii “kichaa” baada ya kukutana na mtu mmoja mwanaume aliyekuwa akiifanya kazi hii. Nilifanya naye
mahojiano yasiyokuwa rasmi kwa kujaribu kumdodosa ni vipi kazi ile iliweza
kumsaidia kimaisha baada ya kumuona alikuwa tofauti sana na waokota chupa
wengine. Kwanza alionekana nadhifu, nguo zake zilikuwa safi, mkononi alishika
fuko la kadiri, siyo kubwa sana na chupa alizookota alichagua zile zilizokuwa
katika hali nzuri peke yake. Zaidi ya hapo, tofauti na waokotaji wengine, yeye
hakuziponda chupa kabla ya kuzitia kapuni bali aliziweka kwa utaratibu zikiwa
nzima.
Katika mahojiano nilibaini kuwa muokota chupa yule ni
baba wa watoto watatu, anaishi na mkewe na wote anawatunza vyema kutokana na
kipato anachopata kwa kazi hii, “mimi kila siku ni lazima niwabebee mke wangu
na wanangu vipaja viwili vitatu vya kuku wakatafune, na mke wangu hubadilisha
khanga kila anapohitaji, nimejenga japo ni kigogo na nina kakiwanja eka mbili
Chanika” Aliniambia kwa kujidai.
Lakini bado nilikuwa na maswali kibao kichwani niliyohitaji kuyajua majibu
yake, kwanza ni vipi anaweza kutengeneza pesa kiasi hicho zinazomuwezesha
kufanya mambo ambayo hata mtu mwenye ajira ya wastani ama biashara ndogo ni
vigumu kuweza kumiliki vitu anavyomiliki huku familia ikimtegemea. Nilikuwa na
mashaka ikiwa ni hii kazi ya kuokota chupa za maji pekee iliyokuwa ikimuweka
mjini. Alinihakikishia pasi na shaka yeyote kuwa kazi yake ilikuwa ni ile ile
ya kuokota chupa za maji zilizokwisha tumika, bali yeye kinachomsaidia kuweza
kutengeneza pesa nyingi ni ubunifu wa kipekee aliouanzisha.
Wakati waokota chupa wengi soko lao hutegemea wanunuzi wa
jumla wanaonunua kwa ajili ya viwanda vinavyokwenda kuyeyusha kwa ajili ya
kutengeneza upya chupa za maji, yeye hufanya tofauti kabisa. Amechagua soko
lake tofauti. Katika maduka ya kawaida ya vyakula mara nyingi wale wenye maduka
huhitaji chupa tupu kwa ajiliya kuwekea vitu mbali mbali mfano, mafuta ya taa,
mafuta ya kula na hata wengine huhitaji kwa ajili ya kuhifadhia dawa za asili.
Ili mtu uweze kuzipata kutokana na siku hizi kuwa hazizagai ovyo, inakubidi
ufanye kazi ya ziada na hata kama utaokota basi ili upate nyingi ni lazima
ukubali kuzunguka kwa muda mrefu mitaani huku jua likikuwakia.
Baada ya baba huyu wa watoto watatu kubaini uhitaji
mkubwa wa chupa hizi katika maduka na kwa watu wanaofanya shughuli mbalimbali
zinazohitaji chupa tupu kwa bei rahisi, basi aliamua yeye kuziokota na
kuwapelekea, na badala ya kuziuza kwa bei rahisi kimafungu kama wafanyavyo wale
wanaokwenda kupima kwenye mzani, yeye huuza chupa moja ndogo ya robo lita kwa
shilingi kati ya 50 mpaka 100, ile ya nusu lita huiuza kati ya sh. 100 mpaka
150 na ya lita moja sh. 100 mpaka 200. Kwa mtindo huo huweza kujipatia kiasi
kikubwa cha fedha kwa siku tofauti na kama angeamua kuziuza kwa kilo.
Na ili kuziongezea dhamani zaidi wakati mwingine
huzisafisha kwa maji safi ya moto na sabuni ambapo ni zile wanazotoa oda wateja
malumu kama vile wanaozitumia kwa ajili ya kuwekea vinywaji mbali mbali kama juisi, togwa na mbege. Anasema kwa zile chupa
anazoosha bei yake huongezeka kidogo mfano badala yash. 50 huuza sh. 100 kila
chupa. “Huwa nakuwa sina haraka, nyumbani nimelundika kiasi kikubwa cha chupa
ambazo naziuza taratibu taratibu, sina ‘presha’ na biashara” alijigamba
mgeni wangu huyu.
Nilibaini kumbe kweli siyo kila unayemuona akiokota vitu
chakavu akili zake zimeruka, wengine wana mipango na mikakati mizuri kushinga
hata wenye biashara rasmi za mitaji mikubwa. Wanatunza familia zao kwa kazi
hizohizo na hata kujiwekea akiba kwa ajili ya kuja kufungua miradi mikubwa
zaidi hapo baadaye. Kwa hiyo chunga usije ukawacheka!
Chanzo cha picha iliyotumika ni: jumamtanda.blogspot.com
0 Response to "SI KILA MUOKOTA MAKOPO NI KICHAA,WAPO WANAOTENGENEZA NOTI KUSHINDA KARANI WA BENKI "
Post a Comment