Ni hivi karibuni nilikuwa nikipita katika mtaa mmoja
maeneo ya Manzese Tip Top ndani ndani, nikahitaji vocha kwa ajili ya simu yangu
ya mkononi, niliuliza vioski na
maduka si chini ya matano lakini cha ajabu kila mmoja
alinijibu hauzi vocha. Nikaenda duka moja kubwa ambalo nilidhani isingekuwa rahisi kukuta
hawauzi vocha za simu. Baada tu ya
kumtaka muuzaji anipe vocha ya sh. 1,000 nilishangazwa na majibu aliyonipa.
“Hatuuzi vocha
mjomba” muuzaduka alinijibu, na mimi ikabidi nimuulize ikiwa mtaa ule watu
hawatumii simu za mkononi, nilikuwa
nimechoka baada ya kupita maduka yote matano bila mafanikio. “Vocha labda uende kule Tip Top stendi, hazina faida kabisa mjomba,
tena hasa hasa hizi za shilingi mia tano sitaki hata kuziona, shilingi 20 faida! biashara kichaa hiyo hailipi”
alimaliza yule muuzaduka.
Siyo vocha za simu tu peke yake, ni biashara za aina nyingi zinazolalamikiwa na watu kuwa
hazina faida kutokana na faida yake kuwa kidogo, biashara hizo utakuta mara
nyingi ni zile ambazo asilimia ya faida ghafi
katika mauzo(gross profit margin) ni kidogo, chini ya asilimia 10%.
Watu wengi hupendelea wanaponunua kitu na kukiuza hasa
hasa wale wanaofanya biashara za
rejareja basi angalao pawe na asilimia
10% mpaka 25%. Hii inamaanisha kuwa, ikiwa bidhaa ameinunua kwa shilingi 2000,
basi akiiuza apate faida angalao shilingi 200 – 400. Lakini bidhaa mfano wa vocha zenye faida ghafi asilimia 5%, atapata
faida ghafi shilingi 100 pekee kwa vocha ya shilingi 2000.
Kitu watu wengi wasichofahamu ni kuwa, katika biashara nyingi ambazo mahitaji yake
kwa wateja ni makubwa, huwezi kukuta zina
faida kubwa sana, lakini kwa kuwa mzunguko wake nao ni mkubwa basi faida
ile ndogo ndogo huwa kubwa katika kipindi cha muda mfupi na ni ya uhakika kwani
wateja ni lazima waje wanunue. Nasema ni ya uhakika kwani, hebu fikiria kitu kama vocha ni sawa na chakula, mtu
anapokula leo, kesho ni lazima njaa itamshika na atahitaji kula tena.
Hivyo ninachotaka kusisitiza hapa tu ni kwamba, ikiwa
biashara ni endelevu, unaimudu kimtaji na soko lipo kwa maana ya wateja,
usiangalie sana ukubwa wa faida bali zingatia zaidi mahitaji ya wateja wako
huku ukitengeneza mkakati wa kupata wateja wengi zaidi, na kuhakikisha wale
uliokuwa nao hawakukimbii, faida kidogokidogo hatimaye itakuwa kubwa na
utashangaa ikiwa ni biashara ileile
uliyokuwa ukiidharau kuwa “hailipi, ni biashara kichaa”
Picha na Africa Business blog.
0 Response to "HAKUNA BIASHARA ISIYOKUWA NA FAIDA"
Post a Comment