Mpango mzuri wa biashara ni ule unaouandika mwenyewe na
wala siyo wa kuandikiwa na mtaalamu au mtu mwingine yeyote yule. Hata ikiwa
utaandikiwa na mtaalamu lakini unashauriwa kuhakikisha kwamba angalao vitu
vyote vya msingi unaviandaa mwenyewe, siyo lazima katika mpangilio maalumu,
lakini uwe na picha ya kile unachotaka kiandikwe kwa mfano mauzo yako unakadiria
yatakuwa kiasi gani, mtaji, nk.
Mpango wa biashara ni kama jino au kiungo fulani cha
mwili wako, ikiwa linauma huwezi ukamwambia mwenzako akangoe la kwake na kisha
ndipo la kwako lipone, hapana, jino ni la kwako kwa hiyo anayeyajua maumivu
yake ni wewe, na ni lazima wewe mwenyewe ndiye utakayehusika katika kulipatia
matibabu.
Anayeijua biashara yako zaidi ni wewe mwenyewe na wala
siyo mtaalamu au mshauri wa biashara, malengo, mikakati, mauzo, soko, na hata
kiasi cha mauzo unachokisia ni wewe mwenye biashara unayevijua vizuri zaidi kushinda mtu mwingine yeyote. Si hivyo
tu bali pia Mpango wa biashara ni kitu kitakachodumu kwa muda mrefu huku
kikibadilika kulingana na biashara nayo itakavyokuwa ikibadilika.
Hivyo ikiwa umeuziwa au kuandikiwa mpango wa biashara ambao huelewi ulivyo,
labda kwa lengo la kuombea fedha benki au kushawishi wabia nk., baada tu ya
muda mfupi mpango ule hautakuwa na manufaa yeyote tena kwako kwani utakuwa
huwezi kuubadilisha chochote kile biashara nayo itakavyokuwa ikibadilika. Utakuwa
tayari umeshapitwa na wakati.
Kwa hiyo mjasiriamali hata ikiwa hupendi kujisumbua
kujifunza kuandika mpango wa biashara lakini ni vizuri zaidi ukafahamu angalao
masuala yale ya msingi ili utakapokuwa ukiandikiwa mpango wa biashara yako na
mtu mwingine basi uwe unatoa mapendekezo ni vipi ungependa uwe kulingana na
mazingira ya biashara husika na utafiti ulioufanya, kwani ni wewe
utakayeendesha biashara.
Usije ukawa ni mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu hata
ikiwa anayekuandikia mambo mengine amefanya ilimradi mpango ukamilike.
Kama utakodi mtu akuandikie, basi tafuta mtu atakayekuwa
kama mshauri, atakayetoa mapendekezo, mtakayeshauriana na siyo atakayebeba jukumu zima la kuandika
kama lilivyo mithili ya mjenzi wa nyumba. Hivyo umuhimu wa kufahamu jinsi
mpango wa biashara unavyotakiwa kuwa ni mkubwa kwa kila mjasiriamali.
------------------------------------------------------------------------------------------
*Mpenzi
msomaji, unakaribishwa kuja kujipatia vitabu vyako, vya ujasiriamali kikiwamo
pia na kitabu Maarufu chenye kila kozi za ujasiriamali pamoja na jinsi
unavyoweza kuandika MPANGO au MCHANGANUO
wa biashara yako mwenyewe cha “Jifunzemichanganuo
ya biashara na Ujasiriamali” Tupigie simu zifuatazo; “0712
202244 / 0765 553030” au fika duka lililopo Buguruni sokoni stendi ukivuka barabara mbele kidogo
ya Akiba Commercial Bank utaona bango juu ya duka lililoandikwa wakala wa
vitabu vya Self Help Books.
0 Response to "KWANINI MPANGO WA BIASHARA WA KUANDIKIWA SIYO MZURI KWAKO?"
Post a Comment