Watu wanaweza wakawa na majibu tofauti mengi kuhusiana na swali hili kwamba, ni kitu gani ambacho wanadamu hupenda kuwa
nacho kuliko kitu kingine chochote kile hapa chini ya jua.
Simaanishi ile kanuni maarufu ya “Maslow’s hierarchy of needs” ya
hatua za mahitaji ya binadamu, kwani ingelikuwa ni hiyo basi tungelisema
binadamu anahitaji zaidi chakula na malazi ili aweze kuishi.
Kwa mtazamo wa wengi jibu linaweza likawa ni moja kati ya
vitu hivi vifuatayo(vimetajwa baadhi tu)
kabla hatujaangalia jibu sahihi ni lipi la ni kitu gani binadamu anachopenda
zaidi kuliko vitu vingine vyote hapa Duniani.
PESA.
Bila shaka yeyote, idadi kubwa ya watu ni
lazima watajibu kwamba, kile wanachopenda zaidi maishani mwao wawe nacho ni
PESA, au kwa maneno mengine wanapenda kuwa na utajiri utakaowawezesha kununua
kila kitu wakipendacho. Binafsi siwezi nikabisha hilo ingawa sina hakika ikiwa
pesa ina uwezo wa kununua kila kitu hapa duniani.
KAZI
NZURI.
Wengine watataja, wangependa kuwa na ajira
nzuri waipendayo yenye kulipa ujira
mnono, tena ikiwezekana serikalini kabisa, kusudi waweze kuwa na ulinzi wa
kutosha wa ajira zao na siyo tena mara leo kazi ipo keshokutwa unaambiwa imeota
majani. Pamoja na marupurupu ya uzeeni baada ya kustaafu kazi.
BIASHARA
NZURI.
Wapo watakao kuambia, wao kitu wanachotamani
sana kuwa nacho maishani mwao kuliko kitu kingine chochote kile, siyo kingine
bali ni kumiliki biashara ya ndoto zao, wawe mabosi wao wenyewe na mwishowe
kuwa na uhuru kifedha utakaowawezesha kufanya jambo lolote maishani pasipo
kumtegemea mtu mwingine yeyote yule wala kuhofia kesho watakula nini ikiwa leo
watatumia kiasi kikubwa cha fedha. Ina maana kuwekeza katika vitegauchumi vya
uhakika vitakavyowatiririshia pesa hata ikiwa wamelala usiku au hata baada ya
kufa.
MUNGU.
“Kuna
faida gani, ikiwa mtu atapata kila kitu hata kama ni Dunia yote, na
kisha akaipoteza Roho yake? “ Hiyo ni moja ya kauli utakazojibiwa na wale ambao
wao kwao kila kitu ni Ufalme wa Mbingu tu, hawataki kitu kingine chochote kile.
Hawataki pesa, magari, mali, wala chochote zaidi ya kupalilia maisha yao baada
ya kifo kwa kumtumikia Mungu wakiwa hapa Duniani.
KUFANYA
JAMBO LA KUKUMBUKWA MAISHANI.
Mwingine yeye shauku yake kuu maishani ni
kufanya jambo fulani liwe ni la kijamii,
kisiasa, kisayansi, kisanaa ama katika nyanja nyingine yeyote ile, ambalo
ni “tofauti” linalowagusa
watu na litakalobadilisha maisha ya wengi. Mwishowe jambo hilo liweze
kukumbukwa vizazi na vizazi hata baada ya mtu huyo kuwa amekwishaondoka duniani.
Iwapo akifa ameshatimiza jambo hilo basi ataridhika mchango wake ameshautoa.
CHOCHOTE
WASICHOKUWA NACHO
Kuna watakaojibu kiujumla kwa kusema kwamba wanachokipenda zaidi ni kile wasichokuwa
nacho, mathalani, ikiwa mtu hana pesa
atakuambia anataka pesa kushinda kila kitu kingine, ikiwa mtu ni mgonjwa
atakuambia anahitaji afya kushinda kila kitu kingine. Kikongwe atakwambia
anataka ujana na Mtoto atakuambia anataka kuwa mtu mzima. Hali kadhalika na kwa
mtu mpweke atakuambia anahitaji mpenzi au rafiki zaidi ya chochote kile.
Orodha ni ndefu ya vitu ambavyo watu wanaweza
kukuambia kuwa ndivyo wanavyotamani zaidi kuwa navyo maishani na hivyo kazi ya
kujua kwamba ni kitu gani hasa kimoja ambacho hupendwa zaidi na watu wengi kuwa
ngumu. Kwa bahati mbaya katika vitu vyote vilivyotajwa hapo juu hamna hata
kimoja ambacho unaweza ukasema ndicho kinachopendwa zaidi na watu.
Kwa mfano ikiwa utasema ni pesa elimu kubwa,
kazi nzuri, biashara nzuri au umaarufu, mbona basi tunashuhudia kila siku watu wenye vitu hivyo
wakijiua na hata wengine kuishi maisha ya kuhuzunisha? Hilo linazidi kunitia
shaka kwamba katika vitu vyote hapo juu hakuna jibu sahihi hata moja.
JIBU
SAHIHI NI LIPI BASI?
Ikiwa wewe ni mdadisi vya kutosha utagundua
yakwamba katika vitu vyoote vilivyotajwa na watu hapo juu, kwamba ndivyo
ambavyo wangetamani kuwa navyo maishani mwao kushinda kitu kingine chochote
kile, vina uhusiano moja kwa moja na kitu kimoja tu kinachoitwa FURAHA.
Halafu kwa makusudi kabisa kuna kitu kingine
kimoja ambacho sikupenda kukitaja ijapokuwa kimlolongo kilipaswa hata kiwe ni
cha kwanza; ‘KUPENDWA’.
Binadamu kwa asili tunapenda sana KUPENDWA na kuthaminiwa,upendo
namaanisha wa aina zote mbili, ule wa kawaida
kama wa mzazi na mtoto na ule wa mtu na mpenzi wake mfano wanandoa. Hali hii ya
kupendwa ndiyo humfanya mtu kuhisi FURAHA.
Hivyo basi unaweza ukasema kwamba katika kila kitu, wanadamu tunapenda zaidi
FURAHA kuliko kitu kingine chochote kile,
ndiyo maana kila mtu ana kitu chake maishani atakachokutajia anakipenda lakini
nyuma ya kitu hicho ndipo FURAHA yake ilipojificha.
Inasemekana kwamba mtu anapokuwa amekamilisha
kila kitu alichokuwa akikitaka maishani mwake, haoni tena sababu ya kuishi na
yupo tayari kufa muda wowote. Maisha huwa na maana tu pale mtu anapokuwa namalengo ya kukamilisha. Hii ndiyo kusema kwamba, mtu mwenye furaha ya kweli
moyoni mwake haogopi kifo kwani tayari anakuwa ameshakamilisha kilichomleta
Duniani.
Mpendwa msomaji, wewe kuna kitu gani unachopenda kushinda vyote katika maisha yako hapa Duniani?.
Mpendwa msomaji, wewe kuna kitu gani unachopenda kushinda vyote katika maisha yako hapa Duniani?.
Me ni pesaa tuu helaa tu hamna kinginee
ReplyDelete