DR. SLAA, PROF. LIPUMBA UJASIRIAMALI WA KISIASA UKO WAPI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

DR. SLAA, PROF. LIPUMBA UJASIRIAMALI WA KISIASA UKO WAPI?








Kwa mujibu wa vitabu mbalimbali na kamusi, Mjasiriamali maana yake ni ni yule mtu mwenye uthubutu/ujasiri wa kuanzisha kitu kipya kwa lengo la kupata faida lakini wakati huo huo pia huwa yuko tayari kukabiliana na hasara yeyote ile inayoweza kujitokeza mbele ya safari.

Katika kitabu kilichoandikwa na mwandishi Peter Augustino Paul na kuchapishwa na kampuni ya Self Help Books Publishers kiitwacho “JIFUNZE MICHANGANUO YABIASHARA NA UJASIRIAMALI” katika sura ya kwanza kabisa, neno ujasiriamali limeelezewa hivi;  

Ujasiriamali  maana yake ni Uratibu na Uendeshaji wa shughuli za kibiashara  kwa Ubunifu kwa lengo la kupata Faida na utayari wa kukabilia na Hasara  yeyote itakayojitokeza.”

Kwa mantiki hiyo basi tunaweza tukasema kwamba, Ujasiriamali wa Kisiasa(Political entrepreneurship) ni mchakato wa kusaka faida ya kisiasa au kijamii kwa kuanzisha aidha chama cha kisiasa ama sera fulani katika jamii kwa ajili ya wanajamii husika na faida hiyo ya kisiasa inaweza ikawa uungwaji mkono kisiasa, kushika madaraka au hata kupata umaarufu kisiasa.

Tukilinganisha ujasiriamali wa kisiasa na ule wa kawaida wa kujichumia mali ni kwamba, chama cha kisiasa ni sawa na biashara, faida ya pesa tunaweza tukailinganisha na kushika madaraka au umaarufu kisiasa, faida wanayopata walaji/wateja tunaweza tukailinganisha na sera nzuri zilizopo kwenye ilani za vyama na wagombea.

Hasara inaweza ikatokea katika kila upande kwenye biashara na pia katika siasa. Katika biashara mtaji unaweza ukakatika kabisa biashara ikafa na kwenye siasa nako unaweza ukakosa kushinda uchaguzi au hata chama kukosa kabisa  mashabiki.

Tukirudi katika mada yetu ya leo, ambayo inawahusu viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, Dr. Wilbroad Slaa, na CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walioamua kukaa pembeni mwa “uwanja wa mapambano” na kuwaacha wafuasi wao njia panda, tunapaswa kujiuliza viongozi hawa kweli wanaelewa maana ya 'ujasiriamali wa kisiasa' ama walidhani siasa ni jambo rahisi rahisi tu?

Kwanza mimi binafsi naomba niweke wazi kwamba Blogu hii pamoja na mimi ninayeandika makala hii hatuna upande wowote katika suala hili. Siyo mashabiki wa chama chochote iwe ni upinzani ama chama tawala hata kama katika mioyo yetu ni wafuasi wa upande fulani lakini katika makala ama blogu hii hatupo upande wowote bali lengo ni kujadili hali iliyojitokeza na kujaribu kuonyesha kila upande ili wasomaji wenyewe wawe mahakimu.

Na zaidi ya yote tunataka watu waone umuhimu wa kuwa na uvumilivu katika kufikia malengo wanayojiwekea iwe katika taasisi au kibinafsi, kutokukata tamaa njiani haraka na kuacha “kuchimba hata ikiwa dhahabu ilikuwa bado futi chache tu ipatikane”.

Maelezo yatakayofuata katika makala hii, yatakuwa katika mtindo wa kulinganisha hali mbalimbali zilizowahi kujitokeza huko nyuma miaka iliyopita hasa katika medani za kisiasa na uongozi kwa ujumla, watu, wanasiasa, vyama, Wafalme, Dini na madhehebu na hata Mitume na Manabii.

MBOWE NI MJASIRIAMALI WA KWELI WA KISIASA.
Tusianzie mbali sana, tuanzie hapa hapa Ukawa. Labda aje kubadilika mbele ya safari manake ni nani alijua Slaa na Lipumba “wangekujakugeuka kuwa mawe ya chumvi?” Unaweza ukamjua kwa kauli zake mbalimbali alizotoa hasa wakati anatoa kauli kuhusu ukimya na kutoonekana katika shughuli za chama kwa Dr. Slaa, alijaribu sana kuelezea jinsi ambavyo walivyoanza mchakato wa kuhakikisha upinzani unachukua nchi, baada ya kushuhudia miongo karibu miwili wanagombea na kukosa wakaamua watumie kila mbinu kama ujasiriamali wenyewe unavyosema ikiwemo ya kumleta Edward Lowasa aliyetemwa na mahasimu wao CCM.

Anasema katika mchakato mzima walikuwa wote pamoja na wenyeviti wenza, Lipumba, Mbatia na Makaidi pamoja na Katibu Mkuu Dr. Slaa lakini cha ajabu karibu na mwishoni wa 'mchezo', kumbe wanakuja kurudi nyuma. Ujasiriamali wa Mbowe pia unadhihirishwa na namna ambavyo yeye binafsi hakuonyesha kutaka maslahi binafsi, kwani pia angeweza akadai apewe fursa ya kugombea Urais. Lakini kwa maslahi mapana ya chama na umoja wao Ukawa aliamua kwanza kuweka mbele dhamira yao kuu ya kukiondoa chama tawala CCM madarakani.

CHAMA TAWALA, CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
Kama wewe ni mdadisi wa kweli wa mambo yanavyokwenda ni lazima utakubaliana na mimi kuwa Chama cha Mapinduzi CCM kweli ni wajanja na pia ni wabunifu, mimi nilidhani labda kauli zao kama vile, “Tutashinda, hata kama ni kwa bao la mkono”, “CCM tuna mbinu nyingi za kushinda” nk. labda  wanamaanisha kuja kuiba kura wakati wa uchaguzi, lakini kwa jinsi zoezi la kuchuja wagombea lilivyoendeshwa kwa umakini wa hali ya juu, nilishawishika kabisa kwamba huenda kauli hizo hazikuwa na maana hiyo bali walikuwa na maana ya kwamba; “watatumia mbinu na mikakati ya ujasiriamali wa kisiasa katika kuhakikisha wanashinda uchaguzi mkuu”

Ujue kwamba hata katika mazingira ya biashara za kawaida, kijasiriamali mtu anapaswa mazingira yeyote yale ya hatari basi yeye  ayageuze kuwa FURSA na wala siyo kuona kwamba sasa anaanguka na hivyo kukata tamaa kabisa ya mafanikio na kukimbia au kujiengua katika biashara. Madhalani una banda lako la kuuzia vinywaji baridi wakati wa jua kali, halafu ghafla msimu wa mvua na baridi unaanza, badala ya kufunga banda na kukimbia kwenda kulala kwa kukosa wateja wa vinywaji baridi, geuza viti vile vile na meza kuuzia kahawa ya moto, chai na maziwa kwa wateja kwani sasa watahisi baridi na kuhitaji vitu hivyo. 

Ingawa wapo wanaosema Lowasa alikuwa mchafu sijui nini, lakini hiyo siyo sababu, hata kidogo, angalia Kenya hapo, kulikuwa na akina William Ruto walikuwa na Raila mpaka dakika za mwisho wakahamia kwa Uhuru Kenyatta. Uliona ni kitu gani kilichotokea?

Kwenye siasa hamna mchafu, angalia nchi za wenzetu mfano Israeli, Ujerumani hata na Pakistan, wanasiasa wanapounda “coalition” hawana muda wa kuanza kuulizana huyu msafi na yule mchafu. Ukawa njia waliyoanza nayo kwa kumkaribisha Lowasa ilikuwa sahihi kabisa kwani walikuwa wanaitumia FURSA vizuri lakini kwa ‘majemedari’ wake Slaa na Lipumba kukaa pembeni siyo ishara njema tena.

Kwanini nasema CCM ni wajanja? CCM walifahamu  mapema kabisa kwamba Lowasa alikuwa ni kama mtego uliokuwa ukisubiri kuteguka, na mtego huo hawakuutega wengine bali walikuwa ni viongozi hawa hawa wa Ukawa akiwemo Dr. Slaa na Profesa Lipumba ambao walishinikiza kujiuzuli kwa Lowasa baada ya kudai alihusika na kashfa ya Richmond. 

Ukawa walikuwa wakisubiri kwa hamu kubwa Lowasa apite CCM. Hizo kelele ambazo wangekuja kupiga wakati wa kampeni juu ya Lowasa na Richmond, sijui kama kuna mtu angekuwa na hamu ya kuipigia CCM kura. Na kwa kuona kuwa Wananchi ‘bidhaa’ wanayoihitaji zaidi sasa ni ‘vita dhidi ya ufisadi pamoja na uwajibikaji,’ CCM hawakuwa na sababu ya kumuweka Lowasa hata ikiwa kimsingi kashfa hiyo ilikuwa haina ushahidi wowote ule, bali Magufuli ambaye bado hajachafuliwa na kashfa yeyote.

Kimsingi CCM waliangalia katika soko kinahitajika kitu gani baada ya kufanya ‘research’ yao. Ni kweli Lowasa alikuwa anakubalika na watu wengi lakini ilikuwa ni lazima CCM waangalie na mazingira mengineyo kama vile wapinzani wao walikuwa na nguvu gani na watakuwa na nguvu gani baada ya uteuzi ule, kifupi walifanya kitu kinachoitwa “SWOT analysis”, au kupima Nguvu, Udhaifu, Fursa na Hatari waliokuwa nayo wao na washindani wao pia.

Walitulia hawakukurupuka. Kwa mfano mtu kama Abdurahaman Kinana, (Jembe)Katibu mkuu wa CCM, kutokana na haiba yake na uchapakazi wake uliotukuka, naye angeweza kuweka tamaa mbele ya kugombea urais lakini tumeona alikaa kimya akipambana kwa maslahi ya chama chake, haiwezekani kila nyuki akawa Malkia, ni lazima kuwe na askari, wanaokwenda kutafuta asali, nta na hata wengine kwa ajili ya kujenga mzinga.”.

NCHI YA MAREKANI (USA)
Kuna mifano mingi katika historia ya Taifa la Marekani ambayo kama wewe unapenda na kuamini kinachosemwa katika vitabu vya historia basi unaweza ukapata mafundisho makubwa sana hasa hasa katika suala zima la siasa na mapambano ya kujitoa katika ukandamizaji wa aina mbalimbali.

Utumwa na Ubaguzi wa Rangi.
Historia ya utumwa Duniani na ubaguzi wa rangi huwezi ukaielezea pasipo kuihusisha nchi ya Marekani na viongozi wake shupavu kama vile akina Abraham Lincoln, George Washington, Martin Luther King, John F Kennedy na hata Rais hata rais wa sasa Barack Obma.

Abraham Lincolin,Rais wa 16 wa Marekani.
Hawakukata tamaa ovyo, walikuwa wavumilivu, wabunifu na waliosimamia ukweli hata ikiwa maisha yao yalikuwa hatarini sembuse nafasi zao kisiasa. Huwezi kuamini Raisi wa 16 wa Marekani Abraham Lincoln licha ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na mgawanyiko mkubwa uliokuwepo wakati huo aliweza kuiunganisha Marekani kuwa Taifa moja na kukomesha kabisa biashara ya Utumwa.

Martin Luther King Jr mwanaharakati na mpigania haki za watu weusi nchini humo aliuwawa angali akipigania haki hizo na hakukata tamaa wakati wa mapambano, ndiye aliyeota ndoto maarufu ambayo hatimaye ilikuja kuwa kweli takribani miaka karibu 40 baadaye, “I HAVE A DREAM” Alikuwa na ndoto kwamba kuna siku moja Marekani itakuja kutawaliwa na mtu mweusi licha ya ubaguzi mkubwa uliokuwepo wakati huo.

Martin Luther King Jr., mpigania haki za kiraia. 
John F. Kennedy hali kadhalika na yeye, alikumbwa na misukosuko sawa na wenzake lakini katu hakukata tamaa. Akiwa ni kutoka madhehebu ya Kikatoliki ambayo nchini Marekani ni wachache,ilikuwa ni vigumu sana kwake kuweza kupenya mpaka kupewa tiketi na chama chake cha Democrat kwani Waprotestant wengi walihofia kuwa endapo angepita basi maamuzi yake yangekuja kuathiriwa na msimamo wake wa dini.

John F. Kennedy Rais wa 35 wa Marekani.
Lakini akihutubia aliwaondoa hofu kwa kusema hivi; “Mimi siyo mgombea uraisi wa chama cha kikatoliki bali mgombea wa urais kwa chama cha Democrat ambaye pia nimetokea kuwa mkatoliki, sizungumzii umma maswala yahusuyo kanisa langu, na wala kanisa halinisemei mimi”. Mwisho wa vikwazo vyote Kennnedy alikuja kuwa Rais wa 35 wa Marekani.

Rais Barack Hussein Obama, naye ingelikuwa ni mtu wa kukata tamaa ovyo leo hii asingelikuwa rais wa Marekani. Historia yake wengi tunaifahamu na wala hatuna haja tena ya kuisimulia hapa. Amedhihirisha ujasiriamali wake hata wa kibiashara juzi alipotembelea Kenya na katika kuchaguliwa kwake kama wenzake niliotangulia kuwataja uliona jinsi alivyokumbwa na vikwazo vingi.

Kwanza kuna watu kwa makusudi tu walimzushia kuwa yeye hakuwa amezaliwa Marekani, na suala hili kweli lilimtoa jasho kwelikweli kwani ilimbidi authibitishie umma wa Wamarekani pasipo shaka kuwa kweli alizaliwa katika jimbo la Hawaii na mama Mmarekani na Baba Mkenya. 

Hiyo haikutosha wapinzani wakaja na swala la Rangi lakini hilo alilishinda kiurahisi kabisa kwa kutumia mbinu na mikakati ya kijasiriamali, hatimaye akawa Rais wa 44 wa Marekani na Rais wa kwanza mweusi.

Barack Obama, Rais wa 44 wa Marekani.
Obama amewahi kusema; “We are the changes we were waiting for” akimaanisha kwamba “Sisi ni mabadiliko tuliyokuwa tukiyasubiri”

TAIFA LA UINGEREZA (UK)
Likiwa limewahi kuwa Taifa kubwa(super power) karne zilizopita kama ilivyokuwa Marekani sasa, ukisoma historia ya Ufalme wa Uingereza utagundua kuliwahi kutokea misukosuko mingi kisiasa na hata katika ufalme wa nchi hiyo. Mfano mmoja wapo ni tukio la kujiuzulu cheo cha ufalme kwa aliyekuwa mfalme wa Uingereza miaka ya 1936, mfalme Edward viii.

Mfalme Edward wa viii 
Mfalme huyu katika historia nzima ya ufalme wa Uingereza alifanya kituko cha aina yake, baada ya kuweka pembeni taji la Ufalme, kisa eti ni kumpenda mwanamke (jimama) aliyemzidi umri tena aliyekuwa ameshaolewa na kuachika kwa wanaume wengine wawili, Wallis Simpson.

Ilibidi waziri mkuu wa Uingereza wakati huo Stanley Baldwin aingilie kati kwa kuchukua maamuzi magumu ya kumtaka mfalme achague ama, kuendelea na mipango ya kumuoa mama yule Wallis Simpson na kuvua taji la ufalme, au kulinda heshima ya nchi na ufalme kwa kuachana kabisa na mipango hiyo.

Mfalme Edward wa 8 akiwa na Wallis Simpson. 
Mfalme alichagua kumuoa Wallis Simpson mwanamke wa Kimarekani aliyekuwa mwanamitindo maarufu na kuachia taji la Ufalme kwa hiyari yake. Ufalme ikabidi apewe mdogo wake George(hakuwa katika ratiba ya kuwa mfalme) ambaye alikuja kutambulika kama Mfalme George wa 6. Mfalme George vi baada ya kufa, ufalme ulirithishwa kwa mwanaye Malkia Elizabeth ambaye ndiye Malkia wa Uingereza mpaka sasa hivi.

Tunajifunza kwamab siyo kila kiongozi anaweza kuvumilia au kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya watu wake, Mfalme Edward viii alichagua kuusaliti ufalme alioachiwa na baba yake na Umma wote wa Uingereza kwa kitu kidogo tu, Mwanamke”, tena aliyekuwa ameshaachika na wanaume wawili!.

JAMHURI YA KISOVIET YA URUSI (USSR)
Nayo kama ilivyokuwa Uingereza na Marekani, liliwahi pia kuwa Taifa kubwa, ‘Super Power’ kwa miongo kadhaa, mpaka pale lilipokuja kuparaganyika miaka ya 90 baada ya aliyekuwa Rais wake Mikhail Gorbachev kushindwa kulinda maslahi mapana ya Muungano wa Kisovieti ambao wakati huo ulikuwa na nguvu sawa na Marekani kijeshi na hata kiuchumi ijapokuwa ilikuwa inachechemea lakini hilo lingeweza kurekebishwa na wala siyo kuisambaratisha kama ilivyotokea.

Mikhail Gorbachev, Rais wa mwisho wa iliyokuwa Soviet Union
Ndiyo maana hadi leo hii Rais wa sasa wa Urusi Vladmir Putin anamlaumu sana Gorbachev, angelikuwa ndio Rais wakati huo sidhani kama Urusi ingelisambaratika. Kusambaratika kwake kumeinufaisha Marekani na Ushirika wa NATO, ndiyo maana unaona matukio kama migogoro ya Ukraine na Georgia. Moscow usione ikitaifisha vinchi kama Kremia, zile ni sehemu za iliyokuwa nchi yake wala hawajakosea sana. 

Vladmir Putin, Rais wa sasa wa Urusi.
Mbona Marekani hawaruhusu kabisa moja kati ya majimbo yake kudai uhuru, au kujitenga?

HITIMISHO.
Kwa hiyo mifano michache ya viongozi mbalimbali Duniani katika nyakati tofautitofauti, utagundua yakwamba, mabadiliko yeyote yale ya kweli yawe ni ya kijamii, kisiasa, kiuchumi au hata kiteknolojia ni lazima yalipiwe gharama. Yanahitaji watu kujitoa mhanga, kupoteza baadhi ya vitu walivyokuwa navyo hapo awali, na hata ikiwezekana kupoteza uhai kwa maslahi mapana ya jamii itakayobakia. 

Na viongozi ndio hasa wanaopaswa kuonyesha mifano na kuwa mstari wa mbele kuyasimamia mabadiliko hayo na siyo kukimbia ama kukaa pembeni na kuwaacha wale wanaowaongoza wakiwa hawajui wafanyeje, wanakuwa ni kama vile vifaranga wa kuku waliokuwa na mama na baba yao ghafla alipotokea mwewe, mama na baba wote wakakimbia na kuwaacha vifaranga wakitweta kwa hofu ya kunyakuliwa na mwewe. 

0 Response to "DR. SLAA, PROF. LIPUMBA UJASIRIAMALI WA KISIASA UKO WAPI?"

Post a Comment