Kweli alikuwa ameingia katika Ulimwengu tofauti. Tulikuwa tumekataa kukubali kasoro za asili, na kwa shauku isiyokoma, tulikuwa tumeishawishi asili kurekebisha ile kasoro, kupitia njia pekee zinazowezekana zilizokuwepo.
Shauku
ilikuwa imeanza kutupa gawio lakini ushindi ulikuwa bado haujakamilika. Kijana
bado alitakiwa kutafuta njia muafaka na inayotekelezeka ya kubadilisha ulemavu
wake kuwa rasilimali inayolingana nao.
Akiwa bado hajatambua vizuri umuhimu wa kile ambacho kilikuwa
kimefanikishwa, lakini akiwa amechanganyikiwa kwa furaha ya ugunduzi wa Dunia
yake mpya ya sauti, aliandika barua kwa watengenezaji wa kile kifaa cha
kusaidia kusikia, akaelezea kwa shauku kubwa jinsi alivyojisikia. Kitu fulani
kwenye barua yake- kitu fulani, pengine, ambacho hakikuandikwa kwenye mistari
lakini kipo katikati yake- kiliifanya kampuni kumualika New York. Alipowasili,
alitembezwa kiwandani.
Alipokuwa akizungumza na Injinia mkuu, akimuelezea juu ya
dunia yake mpya, hisia, wazo, au mawazo ya kutia moyo- yaite vyovyote vile
utakavyo, yalimulika katika akili yake. Ulikuwa ni huu msukumo wa mawazo
uliobadilisha ulemavu wake kuwa rasilimali iliyokusudiwa kulipa gawio la pesa
na furaha katika mamilioni kwa wakati wote ujao.
Wazo kuu la huo msukumo wa mawazo lilikuwa hili;
lilimtokea ili kwamba aweze kuwa msaada kwa mamilioni ya watu wasiosikia ambao
wameishi pasipo kupata fursa ya kuwa na
vifaa vinavyowawezesha kusikia, kama angeliweza kupata njia ya kuwaeleza habari
za Ulimwengu wake mpya. Mara moja alifikia uamuzi wa kujitolea maisha yake
yaliyobakia kutoa huduma zenye manufaa kwa watu wenye matatizo ya kusikia.
Kwa mwezi mzima alifanya utafiti wa kina. Alichanganua
mfumo mzima wa soko la wazalishaji wa vifaa vya kusaidia kusikia, na kutengeneza
njia na namna ya kuwasiliana na wenye matatizo ya kusikia Duniani kote kwa
madhumuni ya kuwashirikisha Ulimwengu wake mpya aliougundua. Hili
lilipofanyika, aliandika mpango wa miaka miwili akitumia matokeo ya utafiti
alioufanya.
Katika kuwasilisha mpango kwenye kampuni, palepale
alipewa cheo kwa lengo la kutekeleza mpango wake. Alipokwenda kufanya kazi
hakuota kama alikuwa amekusudiwa kuleta matumaini na nafuu ya kweli kwa maelfu
ya watu wasiosikia ambao pasipo msaada wake wangeliweza kuangamia milele kwenye
uziwi-bubu.
Muda mfupi baada ya kuungana na watengenezaji wa kifaa
chake cha kusikia, alinialika kuhudhuria darasa lililoendeshwa na kampuni yake
kwa lengo la kuwafundisha wenye ulemavu wa kusikia na kusema ili waweze kusikia
na kusema. Sikuwa nimewahi kusikia aina hii ya elimu kwa hiyo nilihudhuria
darasa kwa tahadhari, lakini kwa matumaini kwamba muda wangu usingeweza kupotea
bure.
Hapa niliona ufafanuzi ulionipa maono makubwa ya kile
nilichokuwa nimekifanya kuamsha na kuweka hai katika akili ya kijana wangu shauku
ya kuwa na usikivu wa kawaida. Nilishuhudia wenye ulemavu wa kusikia na kusema
wakifunzwa kweli kusikia na kusema kupitia matumizi ya kanuni binafsi zilezile
nilizokuwa nimetumia zaidi ya miaka 20 nyuma katika kumuokoa mwanangu kutokana
na uziwi-bubu.
Hivyo kupitia mzunguko wa ajabu wa gurudumu la bahati,
kijana wangu Blair na mimi tulijaliwa uwezo wa kurekebisha uziwi hata kwa wale
ambao bado walikuwa hawajazaliwa. Hapana shaka akilini mwangu kuwa Blair
angeliweza kuwa kiziwi maisha yake yote, ikiwa mimi na mama yake
tusingelichukua hatua ya kutengeneza akili yake kama tulivyofanya.
Blair alipokuwa mtu mzima, Daktari Irving Voorhees,
mtaalamu aliyebobea katika masuala hayo alimchunguza kwa makini.
Alistaajabishwa pale alipogundua ni kwa kiasi gani mwanangu alikuwa anasikia na
kusema vizuri, na alisema uchunguzi wake
ulionyesha kwamba “kinadharia, kijana asingeliweza kusikia kabisa”. Lakini kijana alikuwa anasikia,
licha ya ukweli kwamba picha za X-ray zilionyesha hakukuwa na uwazi katika fuvu
lake, eneo ambalo masikio yake yalipaswa kuwa kuelekea kwenye ubongo.
Wakati nilipopandikiza katika akili yake shauku
ya kusikia na kusema na kuishi kama mtu wa kawaida, msukumo huo uliambatana na
nguvu isiyokuwa ya kawaida iliyosababisha Asili kugeuka kuwa kiunganishi na
kuziba mwanya mkubwa wa ukimya kati ya ubongo wake na dunia ya nje kupitia njia
fulani ambazo wataalamu wa afya waliobobea bado hawajaweza kuzitafsiri.
Ingeliweza kuwa ni kufuru kwa mimi hata kubashiri ikiwa
ni jinsi gani Asili ilitenda huu muujiza. Ingelikuwa ni kitendo kisichosameheka
kama ningelipuuzia kuuambia Ulimwengu kwa kadiri ninavyofahamu kuhusu sehemu
japo ndogo ya huo uzoefu wa kushangaza. Ni wajibu wangu na fahari kusema
ninaamini, na siyo pasipo sababu, kwamba hakuna linaloshindikana kwa mtu ambaye
huipa nguvu Shauku kwa Imani stahamilifu.
Sina shaka kwamba shauku kuu ina njia zilizojificha za
kujigeuza yenyewe kuwa kitu kinachoshikika kilichokuwa na ukubwa sawa nayo.
Blair alitamani usikivu wa kawaida; sasa ameupata! Alizaliwa na
ulemavu ambao ungeliweza kirahisi kumtuma mtu mwenye shauku kidogo barabarani
akiwa na mzigo wa penseli na kikombe cha bati.
Ulemavu ule sasa unatarajia kuwa kiunganishi
kitakachomsaidia kutoa huduma stahiki kwa mamilioni ya watu wenye matatizo ya
kusikia, vilevile kumpatia ajira ya uhakika kwa ujira mzuri wa pesa katika
maisha yake yote yaliyobakia.
“Uwongo mweupe”
kidogo niliopandikiza ndani ya akili
yake wakati alipokuwa mtoto mdogo na kumfanya aamini ulemavu wake
ungeweza kugeuka na kuwa rasilimali kubwa ambayo angeweza kuitumia kama mtaji
ulikuwa umehalalishwa. Hakuna chochote, kizuri au kibaya ambacho
imani iliyochanganywa na Shauku kuu itashindwa kukigeuza kuwa
kweli. Sifa hizi ni bure kwa kila mtu.
Katika uzoefu wangu wote wa kushughulika na wanaume na
wanawake wenye matatizo binafsi, sikuwahi kushughulika na tatizo hata moja
ambalo linaelezea dhahiri kabisa uwezo wa Shauku. Waandishi wakati mwingine
hufanya makosa ya kuandika mada walizokuwa nazo lakini juujuu au kwa uelewa wa
chini sana. Imekuwa bahati kwangu kuwa na upendeleo wa kufanya jaribio la
utimilifu wa Uwezo wa Shauku kupitia ulemavu wa mtoto wangu mwenyewe.
Pengine ilikuwa ni bahati kwamba uzoefu ulikuja kama
ulivyofanya, kwa kweli hakuna mwenye kujiandaa vyema kuliko vile atahudumu kama
mfano wa kile kinachotokea wakati shauku inapofanyiwa majaribio. Ikiwa Mama
Asili huinama kwa mapenzi ya Shauku, kuna mantiki kweli mtu wa kawaida tu aweze
kuishinda Shauku kuu?
Uwezo wa akili ya binadamu ni wa ajabu na usiokadirika !
Hatufahamu njia ambayo hutumia kila hali, kila mtu, kila kitu kinachoweza
kushikika kilichokuwa ndani ya uwezo wake kama njia za kugeuza shauku kuwa kitu
halisi chenye ukubwa unaolingana nayo. Labda sayansi itagundua siri hii.
Nilipandikiza akilini mwa kijana wangu shauku ya kusikia na kusema kama mtu
yeyote yule wa kawaida anavyosikia na kusema.
Shauku ile sasa imegeuka kuwa kweli. Nilipandikiza
akilini mwake shauku ya kubadilisha ulemavu wake mkubwa kabisa kuwa rasilimali
yake kubwa kabisa. Shauku hiyo imeshuhudiwa. Mbinu zilizotumika kuleta matokeo
haya ya kushangaza siyo vigumu kuzielezea. Zina vitu vitatu vyenye ukweli
kamilifu. Cha kwanza, NILICHANGANYA IMANI na SHAUKU kwa ajili ya usikivu wa
kawaida, ambavyo nilivihamishia kwa mwanangu.
Pili, niliwasilisha shauku yangu kwake katika kila njia
inayowezekana iliyokuwepo kupitia uvumilu, juhudi endelevu, kwa kipindi cha
miaka mingi. Tatu, ALINIAMINI MIMI.
Miaka kadhaa nyuma, mmoja kati ya washirika wangu
kibiashara alikuwa mgonjwa, hali yake iliendelea kuwa mbaya kadiri muda
ulivyokuwa ukipita, na mwishowe alipelekwa hospitalini kwa ajili ya upasuaji.
Punde tu kabla hajapakizwa kwenye baiskeli ya magurudunu matatu kuelekea chumba
cha upasuaji nilimuangalia na kushangaa ni kwa jinsi gani mtu mwembamba na
aliyedhoofu kiasi kile angeliweza
kufanyiwa upasuaji mkubwa na akatoka salama.
Daktari alinionya kwamba, kulikuwa na uwezekano mdogo
sana, kama upo wa mimi kuja kumuona tena akiwa hai. Lakini hayo yalikuwa ni maoni
ya Daktari. Hayakuwa maoni ya
mgonjwa mwenyewe. Punde kabla hajapelekwa, alininongoneza kwa unyonge; “Usiwe na wasiwasi bosi wangu, nitatoka hapa
siku siyo nyingi”.
Muuguzi aliyekuwa akimwangalia alinitazama kwa huzuni.
Lakini mgonjwa alikuja kutoka salama !
Baada ya kila kitu kwisha, daktari wake alisema; “Hakuna kitu kingine
zaidi ya shauku yake ya kuishi kilichoyaokoa maisha yake. Kamwe asingeweza kutoka,
ikiwa asingekataa kukubali uwezekano wa kifo”.
Ninaamini katika nguvu ya Shauku ikisaidiwa na Imani kwa sababu
nimeona hii nguvu ikiwainua watu kutoka mwanzo duni mpaka ngazi ya madaraka na
utajiri; nimeiona ikipora makaburi ya
wahanga wake; nimeiona ikihudumu kama jukwaa ambalo watu hulitumia kurudi
baada ya kuwa wamefeli mara tofauti 100. Nimeiona ikimpatia kijana wangu
mwenyewe furaha ya kawaida, maisha yenye mafanikio, licha ya Asili kumtuma
Duniani bila ya kuwa na masikio.
Ni kwa jinsi gani mtu anaweza akaitumia nguvu ya Shauku?.
Hili limekuwa likijibiwa kupitia sura hii, na sura zinazofuata za
kitabu hiki.
Natamani kufikisha wazo kwamba mafanikio yote, bila
kujali asili yake ikoje wala lengo lake, ni lazima yaanze na Shauku
kubwa ya kukipata kitu halisi. Kwa kupitia kanuni fulani za ajabu na
zilizokuwa na nguvu ndani ya “kemia ya akili”, asili huficha ndani ya msukumo
wa shauku
kuu ‘kitu hicho fulani’ ambacho hakitambui kamwe neno, ‘haiwezekani’
wala kukubali ukweli kama kufeli.
........................................................................................................
........................................................................................................
*Ndugu msomaji wetu na hii ndiyo sehemu ya mwisho (ya7 ) ya Sura hii ya pili, karibu uendelee kusoma sura ya Tatu........
0 Response to "UWEZO WA AKILI YA BINADAMU NI WA AJABU NA USIOKADIRIKA!"
Post a Comment