Katika mchakato unaoendelea wa kampeni za
Uchaguzi Mkuu wa kuwapata Rais, Wabunge, na Madiwani, kumekuwa na ushabiki
mwingi hasa katika pande mbili kuu, nikiwa na maana ya Chama Tawala CCM na vile
vya Upinzani vinavyowakilishwa na Umoja wa Katiba au UKAWA ingawa pia kuna
vyama vingine kadhaa ambavyo havijajiunga na Umoja huo kama vile TLP na ACT.
Huko mitaani nako Wananchi nao utakuta
wamegawanyika, wengine wakishabikia CCM, wengine UKAWA, na wengine katika vyama
vilivyosalia. Jana mchana nikiwa nimekaa mahali fulani niliona gari moja la
kampeni likiwa limesimama kando kando ya maduka huku wahusika wakiwa wanaingia,
mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba, duka kwa duka, wakiwa wameshikilia
mabango(posters) waliyokuwa wakiyabandika katika kuta, milango, katika nguzo za
umeme na simu na mahali pengine popote pale walipoona panafaa kubandika.
Si hivyo tu walikuwa pia wakigawa vipeperushi
na beji kwa watu mbalimbali. Uzuri ni kuwa hawakuwa wakibandika tu hovyo hovyo
pasipo ridhaa ya wahusika, walikuwa wakiwaomba wenyeji waliowakuta pale
wakikubali basi ndipo na wao hubandika.
Kuna baadhi ya sehemu, nyumbani na hata
baadhi ya maduka na biashara ambapo walikataliwa, nadhani wengine ni kutokana na
misimamo yao kuwa tofauti na ya kile chama wale wahusika walichokuwa
wakikipigia debe. Lakini inawezekana pia wengine walikataa tu hata ikiwa
mirengo yao wanayosimamia ilikuwa sawa na hayo matangazo na hapa hasa ndipo
mimi ninapotaka kupazungumzia zaidi.
Kwa maoni yangu binafsi nadhani hata
kitaalamu inaweza ikawa ni sahihi, sidhani kama ni jambo zuri kuhusisha moja
kwa moja ushabiki wa kisiasa au hata jambo lolote lile lenye kuleta mihemko
kama vile dini katika biashara unayoifanya.
Suala hili limeelezewa kwa undani zaidi
katika kitabu cha “SIRI YA MAFANIKIO YA BIASHARA YA REJAREJA”, kilichoandikwa na Peter Augustino na kuchapishwa
na Self Help Books Publishers ltd. Ni katika ukurasa wa 36-38, kwenye somo
linaloosema; “MAKOSA YATAKAYOKIMBIZA WATEJA DUKANI KWAKO NA KUDHANI UMELOGWA”
chini ya kipengele kilichoandikwa; ‘Kubandika Matangazo ya Ajabuajabu’
Hii
ni sehemu(kipande) tu ya kitabu hicho inayozungumzia makosa yanayoweza yakakimbiza
wateja katika biashara yako na wewe ukadhani
labda umelogwa.
|
Kumbuka katika biashara yako ndogo wewe
unahitaji wateja kutoka kila upade ili uweze kukua pasipokujali huyu ni CCM,
huyu ni UKAWA, huyu ni TLP, ACT au huyu ni Muislamu, huyu ni Mkristo, huyu ni
Mhaya, yule ni Mngoni, Mzaramo nk. au tabaka jingine lolote lile. Kuna watu
huwa wanakwazika kwa jambo dogo sana, madhalani yeye anashabikia CCM,
atakapofika kwenye biashara yako kwa lengo la kununua kitu kisha akakutana na bango
linaloshabikia UKAWA, basi mteja huyu kuna mawili, umkose kabisa au hata
akinunua basi siku nyingine itakuwa vigumu kurudi tena katika biashara yako
kwani yeye moja kwa moja anajenga chuki na ile biashara yako.
Hawezi kuitofautisha na wewe. Kwa kuwa
anachukia ule upande wa pili ambao wewe ndiyo unaoshabikia, ndivyo hivyo hivyo
atakavyoichukia na biashara yako. Kwa hiyo kwa mtindo huo hebu fikiria ni
wateja wangapi utakuwa umewakwaza kuja kukuungisha?
Si jambo baya kuonesha upo upande gani,
lakini wewe pima kwanza, ukiona madhara yanayoweza kutokana na wewe kuonesha
ushabiki katika biashara yako kupindukia ni makubwa na yatakayoweza kukuletea
athari mbaya basi huna sababu ya kufanya hivyo.
Kuna watu wamewahi kupata hasara kubwa
kutokana tu na ushabiki, zinapotokea vurumai, mahasimu huzilenga zaidi biashara
na mali za wale mahasimu wao waliokuwa
mstari wa mbele zaidi wakishabikia. Kama upo tayari kukabiliana na yote hayo
endapo yatatokea basi siyo vibaya
kuonesha ukereketwa wako hata ikiwa ni kwa kuzungushia bendera za chama chako
nyumba nzima.
0 Response to "MJASIRIAMALI UNAWAHITAJI WATEJA WOTE, CCM NA UKAWA"
Post a Comment