Yanini kuanza kufikiria Mpango wa biashara
kwanza kabla ya kuanza kufanya biashara yenyewe?, kwanini mtu upoteze muda wakowa thamani kuanza kuchanganua na kufanya utafiti wa biashara ambayo ungeweza tu
kuanza na mambo mengine yakajipanga yenyewe mbele ya safari?.
Maswali haya na mengine mengi, yamekuwa
yakiulizwa na wajasiriamali popote pale duniani hasa wanapowaza juu ya
kutayarisha michanganuo ya biashara zao.Ijapokuwa wataalamu wa biashara
wamewahi kufanya utafiti na kubaini kuwa wafanyabiashara wengi na hata wale
wajasiriamali wana anza biashara zao pasipo kuhangaika kutengeneza mpango wa
biashara, lakini pia tafiti hizo zimegundua umuhimu na faida nyingi
zinazotokana na mtu kuandaa kwanza mpango wa biashara yake kabla haja anza na
hata ikiwa alikuwa amekwishaianzisha biashara yenyewe kitambo.
Kama mmiliki wa biashara, unaweza ukawa
unazifahamu baadhi ya faida za kuandika mpango wa biashara kama vile, kumsaidia
mjasiriamali kuongeza uwezekano wa mafanikio katika biashara anayoiandikia
mchanganuo, kumsaidia katika suala zima la kujipanga “organizing a business”,
kumsaidia katika mchakato wa kupata mtaji nk.
Kwa kifupi kabisa ni kwamba; ikiwa
una mpango wa kuanzisha biashara mpya, unapanga kuendeleza biashara
uliyokwishaanzisha zamani au unatafuta usaidizi kimtaji kutoka nje ya kampuni
yako; basi ujue kabisa yakwamba unahitaji Mpango/mchanganuo
wa biashara.
Lakini je, unazijua zile faida kuu tano (5)
muhimu kuliko nyingine zote?. Faida zipo nyingi tu, inategemea, umeamua
kuzitaja kwa kutumia vigezo gani, wengine hata wanaweza wakakutajia faida 20,
15 nk. Kulingana na wanavyozitazama.
Sasa
basi ikiwa faida za kuandika mchanganuo wa biashara ni nyingi kiasi hicho,
kwanini wafanyabiashara/wajasiriamali wengi hawapendi kuandika michanganuo
kabla au hata baada ya kuanzisha biashara zao?
Kimsingi hakuna hatari yeyote ile ya mtu
kuandika mchanganuo wa biashara, lakini wajasiriamali baadhi yao wamekuwa
wakitoa visingizio lukuki kwanini hawapendi kuandaa mipango ya biashara zao. Na
baadhi ya sababu na visingizio hivyo ni hivi hapa chini;
1. Kukosa
elimu sahihi ya Ujasiriamali na Biashara pamoja na kutokufahamu jinsi ya
kutayarisha mpango wa Biashara.
Ingawa wajasiriamali wengi wangependa kuandaa
michanganuo ya biashara zao lakini hukumbana na kikwazo cha kutokuwa na elimu
ya namna michanganuo yenyewe inavyoweza kuandaliwa, na hata wanapojaribu
kutafuta wataalamu wa kuwaandikia mpango wa biashara napo hufeli kutokana na ada au malipo kuwa
makubwa na hivyo kuishia kuanzisha biashara hivyo hivyo tu wakitegemea mpango
wa kichwani. Wengine mipango ya kichwani huwasaidia na wakafanikiwa lakini wengi
hushindwa.
2. Huwezi ukatabiri mambo yajayo, ni uchuro.
Wengine kutokana na imani potofu tu huona
kuanza kubashiri jinsi biashara itakavyoweza kuja kuwa miezi kadhaa ijayo au
miaka basi ni kama vile jambo la uchuro, ni sawa na mtu kujitabiria utakufa
lini nk. Imani kama hizi katika biashara hususani kwetu sisi waafrika ni jambo
la kawaida lakini nyingi zimekuwa zikiturudisha nyuma bila ya sisi kujua.
Wanadhani kutabiri kunaweza kukasababisha
wakose moyo wa kuendelea na biashara waliyoipenda endapo watatabiri biashara
kutokufanya vyema kama wanavyopenda iwe, mathalani mtu anatamani kupata faida
milioni moja, mpango ukitabiri atapata laki 5 basi hapendi. Wanakuwa kama
ngamia, kushindwa kukabiliana na ukweli wa mambo.
Wengine hudai eti, unavyopanga mara nyingi
huja kubadilika na kuwa tofauti, hivyo hamna umuhimu wa kupanga kitu ambacho
baada ya muda mfupi kitapitwa na wakati. Lakini ndiyo maana ya kutabiri, ni juu
yako sasa kufuatilia na kuangalia ni jinsi gani biashara halisi
inavyotofautiana na mpango wako na kisha unaendelea kurekebisha kulingana na
taarifa halisi unazokutana nazo kila siku wakati ukifanya biashara halisi. Na
wala hii haitakupunguzia kitu sanasana itakuongezea uthibiti na umakini zaidi
wa hali ya biashara inavyotakiwa iende.
Malengo ya biashara uliyoweka endapo katika
hali halisi yataonekana kuwa chini basi mpango wa biashara utakusaidia kwani
sasa itabidi uongeze jitihada zaidi au kubadilisha mikakati kusudi uweze
kuyafikia malengo ama hata kuyazidi. Ikiwa hukuwa umejiwekea malengo utajuaje
kama hujafikia malengo?
3. Mjasiriamali
ana muda mchache sana, hivyo kuandika mpango wa biashara ni kuzidi kuupoteza
muda huo kidogo aliokuwa nao.
Sababu hii siyo kweli hata kidogo kwani,
ikiwa ina ukweli basi kwanini hata hao ambao hawaandiki michanganuo ya biashara
zao wakihofia kupoteza muda bado idadi ya biashara zinazokufa kabla ya
kufikisha hata mwaka mmoja ni kubwa?. Ukweli ni kwamba mchakato wa kuandika
mchanganuo wa biashara ikiwa wewe mjasiriamali ndiye uliyehusika katika kufanyautafiti/upembuzi yakinifu basi uwezekano wa biashara yako kufanikiwa ni mkubwa
zaidi kushinda yule aliyeanza kwa mkato bila kuandaa mpango wowote akikwepa
kupoteza muda.
Hauhitaji kuandika mamia ya kurasa, hata
kurasa mbili tatu unaweza ukayaweka mawazo yako juu ya ni wapi biashara inakotoka,
ni wapi ilipo na ni wapi inakoelekea. Na basi ukiona huna muda kabisa
waweza kumlipa mtaalamu au mtu mwenye uwezo wa kuandika akafanya kazi hiyo
badala yako.
4.
Mpango wa biashara(Business Plan) hausaidii kwa lolote kupata mkopo kutoka
benki au taasisi nyinginezo za fedha.
Sababu hii itategemea ni katika mazingira yapi
unataka kuutumia mpango wa bishara yako kupata mtaji kwa ajili ya kuanzia ama
kuendeshea biashara yako. Mathalani, ni ukweli usiopingika mazingira kama ya
hapa kwetu Tanzania, kwa kweli useme eti unakwenda benki na makabrasha yako ya
mpango wa biashara na benki wakakuamini kukupa mkopo kwa kigezo hicho pekee, ni
uwongo, hawawezi wakakupa kamwe.
Siyo mabenki tu bali hali ni hiyo hiyo hata
na kwa wadau wengine, wanaoweza wakawa chanzo cha kukupa mtaji kama vile wabia
na hata wawekezaji. Mwekezaji yeyote yule na popote pale, hupendelea kuwekeza
katika biashara iliyokwishaanzishwa ikasimama na inayoendelea, na zaidi ya hapo
wanapendelea kuona kitu zaidi ya makaratasi, (DHAMANA).
Lakini hiyo haiondoi umuhimu wa kuwa na
mpango wa biashara kwani, kama tutakavyoona hivi punde zile sababu kuu 5 za
kuwa na mpango wa biashara yako kabla hujaanza biashara yenyewe. Kwanza
kiumuhimu sababu hii ya kusaidia katika kupata mitaji, haipo kabisa katika
listi hiyo na hata kama ipo basi ni moja ya vipengele vya sababu nyingine kubwa
zaidi.
Yapo mazingira ambayo mpango wa biashara ni
muhimu ili uweze kupata mtaji kutoka kwa wawekezaji au taasisi za fedha, kwa
mfano, miradi mikubwa mikubwa wakati mtu utataka kupata ufadhili, mkopo au hata
kutaka kujiunga na soko la hisa la Dar es salaam, basi mpango wa biashara
hauepukiki hata kidogo.
Kwa nchi zilizoendelea kama Marekani, Canada,
Uingereza na nyinginezo, biashara hata ikiwa ndogo unapoandaa mpango wako mzuri
wa biashara basi unaweza ukapata ruzuku au mkopo mdogo kutoka serikalini
kupitia taasisi mbalimbali zilizoanzishwa rasmi kwa ajili ya kuzisaidia
biashara ndogondogo, mfano wake hapa kwetu ni kama zile pesa za “Mabilioni ya
Kikwete” kipindi kile anaingia madarakani.
Na siyo kweli asilimia mia moja kwamba katika
taasisi ndogondogo za fedha na mabenki ya hapa kwetu Tanzania hayazingatii
kabisa suala la mpango wa biashara la hasha, kuna baadhi ya vipengele muhimu
katika mpango wa biashara ambavyo huviweka hata katika fomu zao za kuombea
mikopo ikiwa ni pamoja na wakati wanapokuhoji basi hujaribu kukuuliza uwajibu
maswali yaleyale ambayo kama ungeliandika mchanganuo wa biashara yako, basi
ungelikuwa umewajibu.
Maswali kama vile; “Biashara yako mauzo ni shilingi
ngapi kwa siku/kwa mwezi”, ‘Biashara yako ina thamani gani’, ‘Biashara yako
inadai/inadaiwa shilingi ngapi?’ ‘Matumizi
yako kwa siku/kwa mwezi ni kiasi gani?’ ‘Taja mali isiyohamishika uliyokuwa
nayo’, ‘Unawalipa wafanyakazi/vibarua wangapi na ni sh. ngapi?’ utautumiaje
mkopo utakaopewa nk. Tathmini ya maswali hayo yanawakilisha mpango wako
mzima wa biashara na siyo lazima mpango wa biashara uwe ni mamia ya kurasa.
Wajasiriamali wana sababu nyingi kwanini
hawapendi kuandika mpango wa biashara, ndugu msomaji kama na wewe ni mmoja kati
ya wamiliki wa biashara ndogo ndogo au hata zile za kati, basi unakaribishwa na
wewe uchangie, tuambie ni sababu zipi zinazokufanya usite kuandika mchanganuo
wa biashara yako. Toa maoni yako pale chini.
Kabla sijaenda kukutajia zile sababu kuu
zaidi 5 (tano) kwanini uandike mpango wa biashara, ningependa kwanza
nikusimulie ‘story’ ifuatayo na iliyotendeka kweli(siyo hadithi ya kutunga)
Miaka mitano iliyopita kuna rafiki yangu
mmoja kwa jina anaitwa J.Kileo, alianzisha kampuni yake ndogo ya kuuza nguo za
kike na vitu mbalimbali vya ‘luxury’
kama mabegi ya akina dada, saa za mkononi, viatu na urembo, vitu hivyo alikuwa
akienda kuvichukua China na wakati mwingine Hong kong na kisha kuja kuviuza
hapa Tanzania, Zambia na Malawi.
Biashara iliendelea vizuri tu mwaka wa
kwanza, wa pili na hata mwanzoni mwa mwaka wa tatu, lakini ghafla mambo
yakaanza kwenda ndivyo sivyo mwezi wa tano. Kengele ya hatari ilianza kulia
kichwani mwake pale ushindani wa hatari ulipoanza, wakazuka wafanyabiashara
wengine kibao walioiga biashara ileile ya kuagiza na kuuza nguo, viatu na vitu
vya akina dada kutoka china, tena kwa bei ya kutupa!
Biashara ilianza kupungua taratibu na
kufuatiwa na faida nayo kuanza kupungua kidogokidogo. Kileo hakuwa na jinsi,
akaamua kubadilisha biashara. Alianza biashara nyingine ya kuuza nguo za ndani
za kike kama vile, chupi, sidiria na andasketi za mitumba kwa wanawake,
biashara ambayo alipata faida kubwa sana karibu asilimia hamsini, yaani nusu
kwa nusu, akinunua chupi au sidiria moja shilingi mia tano(500) basi huenda
kupata faida shilingi mia tano.
Biashara hii ya nguo za ndani za mitumba,
alidumu nayo kwa muda wa miezi sita tu (6) kabla balaa jingine halijazuka tena,
Serikali ilikuja na sera mpya iliyopiga marufuku kabisa biashara ya nguo za
ndani za mitumba kwa wanawake na wanaume, zikiwemo chupi, sidiria underskirt,
na hata bukta. Ndani ya miaka 4(mine) mtaji wote wa Bwana Kileo ulikatika
kabisa kutokana na sababu mbalimbali kama zilivyoelezwa hapo juu.
Kosa moja kubwa alilolifanya Bwana Kileo, ni
kuanzisha biashara yake ya kwanza kabisa pasipo kufanya utafiti wa biashara, na
hatimaye kuwa na mpango wa biashara ambapo angeliweza kubaini mapema hatari
mbalimbali au hasara ambazo zingeliweza kuja kujitokeza hapo baadaye kama
tulivyoona na hivyo angeliweza kujipanga kuzipunguza au kutafuta njia mbadala
ya kuzikwepa kabisa.
Sasa bada ya kukushirikisha mkasa huo
uliomkuta rafiki yangu wa karibu bwana Kileo, moja kwa moja hebu tuone zile
Sababu tano(5) kwanini Mpango wa biashara una faida kuuandika, iwe ni kabla ya
kuanza biashara mpya au hata wakati biashara imekwisha anza siku nyingi unataka
kuiboresha.
Sababu
kuu 5(tano) ni kwanini kuandika mpango wa biashara yako kwanza kabla huja anza
biashara yenyewe.
1. Kuweka malengo mahsusi ya biashara yako;
· Ni
dira itakayokuongoza katika kufanikisha malengo uliyojiwekea. Hukulazimisha
ufikirie kwa kina kuhusiana na biashara unayotaka kufanya.
· Biashara
ili iweze kwenda vizuri inahitaji uweke malengo mahsusi halafu uyatekeleze
pamoja na kufanya tathmini mara kwa mara kadiri makisio “assumptions” nayo yatakavyokuwa yakibadilika
kusudi uweze kufahamu biashara halisi na mpango wako vinatofautiana kwa kiasi
gani. Na ni lazima vitofautiane, hiyo ndiyo maana ya makisio popote pale hata
ingelikuwa unatabiri hali ya hewa.
· Utatekelezaje
majukumu ya biashara pasipo kupanga? Hebu jaribu kufikiri ikiwa wewe ni mwanamke au hata mwanaume unapotaka kwenda sokoni kununua vitu vya nyumbani au shopping yeyote ile, kiukweli niambie, hukai chini na kupanga utaenda kununua kitu gani,wakati mwingine bila shaka unachukua kalamu na kuandika katika karatasi.
· Utajuaje
ni kitu gani kinachotakiwa kifanyike labda tuseme kesho, keshokutwa au
mtondogoo kama haujakaa chini ukafikiri na kupanga?
· Wanaojidai
hawana haja na mipango wala biashara zao hawakutumia mipango kuzianzisha ni
waongo! Hata kupanga kichwani mwako pasipo kuandika mahali nao ni mpango wa
biashara. Kama unao uwezo wa kupanga kwa kichwa pekee bila kusahau, basi
vizuri, una bahati, ila ukitaka upange kwa weledi na kwa uhakika zaidi, basi
huna budi kuandika kwenye karatasi.
· Ili
biashara ifanikiwe, UTEKELEZAJI ni
kila kitu, hiyo inamaanisha kwamba, unatakiwa uweke vipaumbele, ubainishe
malengo na upime matokeo baada ya utekelezaji.
2. Kutambua mahitaji ya kifedha na rasilimali
nyinginezo mbalimbali zinazohitajika zikiwemo rasilimali watu.
· Je,
biashara yako itahitaji fedha kutoka mahali pengine? Kama ndiyo, ni kiasi gani?,
utazipata kutoka wapi na utazitumiaje?, watendaji/wafanyakazi ni kina nani,
gharama mbalimbali, makisio ya mapato nk. Vyoote hivyo mchanganuo wa biashara
utakusaidia kujibu.
· Unaweza
ukajiepusha na kosa la kupoteza muda bure wa kufanya biashara hata mwaka mzima
na baada ya hapo unakuja kubaini kumbe mtaji ulikuwa hautoshi au biashara
haizalishi faida, kama mtaji ni kidogo ni dhahiri uwezekano wa biashara hiyo
kufanikiwa ni finyu sana, kumbuka “kufanyabiashara na mtaji finyu nisawa na mtu anayelima kwa jembe lisilokuwa na mpini”. Kuandika mpango
wa biashara kutakuepusha kufanya maamuzi ambayo baadaye utakuja kugundua
hukupaswa kuyafanya lakini, “too late”.
3. Kutathmini uwezekano wa kufanikiwa kwa wazo
la biashara/mradi.
· Je,
wazo lako hilo ni zuri kiasi gani?, litalipa?. Mchakato mzima wa kuandaa mpango
wa biashara unakulazimisha ufanye utafiti wa soko lengwa la bidhaa/huduma zako
pamoja na washindani wako na hivyo kubaini nguvu uliyokuwa nayo kuwapita
washindani hao.
· Utakapobaini
kwamba wazo linalipa basi hatua inayofuata unaendelea na mchakato wa kufanya biashara
lakini ikiwa itaonyesha hailipi unaweza ukafikiria mara mbili uachane nayo au
uendelee.
4. Kuthibitisha
umakini wako na kujitoa katika biashara unayotarajia au ambayo tayari
unaifanya.
· Mpango
kamili wa biashara ni muhimu ukaonyesha
kwa wadau wote(pande mbalimbali) kwamba
ni kweli umejipanga vilivyo na umejitoa kiukwelikweli kufanikisha
biashara yako.
· Wadau
hao wanaweza wakawa; wafanyakazi, mke, mume, wateja wanaokusambazia bidhaa,
wateja wanaonunua, wawekezaji, wabia,
taasisi za fedha kama benki nk., bila ya kusahau na wewe wenyewe binafsi. Hebu
fikiria, wadau wako wasingependa kufahamu ni kitu gani kinachotakiwa kufanywa
ndani ya biashara yako?
· Halikadhalika
wadau wako unaotegemea watakupa mtaji mfano, benki, taasisi za fedha, wabia au
wawekezaji, hii ndiyo njia muafaka ya kuwashirikisha mikakati na maono yako, na
ndiyo maana watu wengi tumekuwa tukiuchukulia mpango wa biashara kama ni chombo
cha kuombea fedha(mikopo) tu bila ya kujua kwamba mpango wa biashara ni zaidi
ya hapo, na una kazi nyingine nyingi zilizokuwa muhimu hata kushinda kuombea
mkopo benki.
5. Kusaidia ugunduzi wa fursa mpya za masoko.
· Kupitia
mchakato mzima wa maandalizi ya mpango mzima wa biashara, unahusisha kufikiria
kwa kina, kuhoji watu, kutafiti machapisho mbalimbali yahusuyo biashara husika
pamoja na kuitazama biashara yako katika mtizamo tofautitofauti. Matokeo yake,
utaibuka na mawazo mapya kuhusiana na namna ya kutafuta soko la biashara yako,
jinsi ya kuiendesha na kuikuza zaidi.
……………………………………………………………….………
Mpenzi msomaji na huo ndio mwisho
wa makala yetu hii, tunakuomba uendelee kuwa na sisi kila mara, pia usisahau
tuna vitabu vizuri zaidi vya
ujasiriamali
katika lugha ya Kiswahili, tunakuahidi pia kuendelea
kukuletea makala nzuri za kuelimisha kila siku na mwisho usisahau ule usemi
usemao;
“kushindwa kupanga, ni kupanga
kushindwa”
Aisee mpo vizuri, mtawasaidia watanzania wengi. Lakin pia mngefikiria kuandaa semina katika maeneo mbalimbali km makanisan, vyuon na nk kwasababu watanzania wengi siwasomaji wataarifa hizi nzuri. Watawasikia na itakuwa vzur pia mkiwashauri umuhimu wa kusoma makala haya, pamoja na vtabu. Na mm nahitaji sana hvyo vtabu
ReplyDeleteAsante sana Shadrack, ushauri wako tumeupokea kwa mikono 2 na tutaufanyia kazi. Unakaribishwa, vitabu vinapatikana tuwasiliane tu kwa namba 0712202244
Delete