Wazungu husema ni “Unconditional Love”, upendo
usiokuwa na masharti.Kuwa mzazi maana yake ni kwamba umpende mwanao kuliko hata
ulivyowahi kujipenda wewe mwenyewe maishani mwako.
Naandika makala hii kutokana na kisa kimoja kinachonihusu
binafsi, nami kutokana na kwamba kilinigusa mno basi nikaona ni vizuri
kukielezea hapa kama njia ya kupunguza mhemko niliokuwa nao juu ya tukio lenyewe
pia kumshirikisha yeyote yule hasa
ambaye ni mzazi.
Wiki jana wakati nikiwa katika mihangaiko yangu,
nilipigiwa simu na mke wangu akinijulisha juu ya matokeo ya kijana wangu Frank
anayesoma chekechea. Mama yake alikuwa amekwenda shuleni anakosoma kuchukua
matokeo ya mtihani wao wa mwisho wa mwaka. Nilishangaa!.
Mwanangu Frank ni mtundu, siyo ule utundu wa kawaida,
bali ni utundu ambao kila mtu anayemuona hushangaa. Siwezi nikaelezea kwa kina
sana namna alivyokuwa mtundu lakini inatosha tu kusema kuwa ni mtundu.
Kilichonishangaza mimi na hata mama yake ni matokeo yake ya mtihani wa kwanza
shuleni, katika watoto 60 aliweza kushika namba ambayo sikuweza kuamini kabisa
licha ya utundu aliokuwa nao. Aliweza kuwamo katika watoto 10 wa mwazo. Matokeo
yale yalinifanya nifikirie kwa kina sana juu ya namna ambavyo wazazi tunapaswa
kuwafunza maadili mema watoto wetu.
Frank kuna wakati
fulani alikuwa akifanya kosa huwa nilikuwa nikimtandika kwa lengo kwamba
hatarudia tena kosa lile, lakini kwa
mshangao hata siku haitapita utakuta kesharudia tena kosa lilelile. Kitendo cha
kuwa namchapa mara kwa mara niligundua kilikuwa kinamfanya mtoto awe anakuwa na
tabia ya ukatili zaidi badala ya kujirekebisha.
Kila nilipomchapa baadaye
nilikuwa nikiingiwa na huruma ninapomtazama, “kalivyokuwa kadogo!”,
kisha najisemea moyoni, “Mbona hata mimi
nilipokuwa mtoto nilikuwa nikifanya makosa kama yeye” Sikuwa napenda kabisa kumtandika bali nilidhani nisipofanya vile ndiyo
nilikuwa namharibu zaidi.
Baada ya kugundua kumuadhibu haimbadilishi, niliamua sasa
kutumia mbinu nyingine, kumchukulia kwa upendo kila anapofanya kosa, badala
sasa ya kuwa mkali nikawa kwanza naonyesha kuchukizwa na kile anachokifanya
kisha najaribu kumfanya ajue kwamba kile alichokifanya ni makosa, siyo sahihi.
Kidogo kidogo sasa naona mbinu hii inazaa matunda na mtoto ameanza kujiamini na kupunguza ule utundu aliokuwa nao. Hii haiondoi kabisa uwezekanao wa kumtandika, ila simtandiki kila mara tena hata kwa ‘vikosa’ ambavyo najua hata mimi nilikuwa navifanya nilipokuwa mtoto.
Kidogo kidogo sasa naona mbinu hii inazaa matunda na mtoto ameanza kujiamini na kupunguza ule utundu aliokuwa nao. Hii haiondoi kabisa uwezekanao wa kumtandika, ila simtandiki kila mara tena hata kwa ‘vikosa’ ambavyo najua hata mimi nilikuwa navifanya nilipokuwa mtoto.
Siku moja alifanya kosa kubwa shuleni kwake ambalo kwa
vyovyote vile alijua baba akija tu ni lazima atamchapa ikiwa ni pamoja na
kwenda mpaka shuleni pengine kumuadhibu mbele ya mwalimu na wanafunzi wenzake,
mama yake alimsikia akitamka, “leo
naomba baba asije tu nyumbani” kwa woga wa kuja kuchapwa.
Nilipofika nyumbani, alikaa mbali kabisa na mimi, baada ya
mama yake kunielezea sikuonyesha kabisa kukasirika, bali nilimuita kwa upole na
kuanza kumuuliza taratibu ni kwanini alikuwa amefanya vile (alikuwa na tabia ya
kuwapiga wenzake makonzi kichwani na siku hiyo mwalimu aliandika kikaratasi kwa
mzazi ili aende shuleni kuonana naye).
Ijapokuwa ni mtoto mdogo kabisa, kwa kweli alionyesha
kujutia kosa mno! Akaniambia “Baba sirudii
tena nisamehe”. Nusura machozi yanitoke, nikamkumbatia na kumuambia, “mwanangu nakupenda sana usiwe tena
unafanya makosa”
Baada ya kugundua hakukuwa na uharaka sana wa kufika pale
shuleni kwa ajili ya kosa lile, nilimwambia na mama yake wala asiongozane naye
moja kwa moja kwenda kwa mwalimu siku iliyofuata, bali atakwenda kuonana na
mwalimu wakati wake, mtoto mwenyewe hajui kama wameonana. Yote hiyo ilikuwa ni
kumfanya mtoto ajiamini na kutokuhisi kuwa anahukumiwa.
Upendo
wa bure pekee hapa duniani ni ule wa wazazi, wa wengine wote waliobakia ni
lazima uulipie gharama...
Kwa kweli nimegundua kwamba hata wazazi wengi
wanaowafanyia watoto wao ukatili wa kutisha baada ya kufanya makosa, wengine si
kama wanapenda bali ni mihemko inayotokana na hasira huku wakidhani kwa kuwapa
adhabu kali basi watajirekebisha kumbe ni kinyume chake. Si kama hawawapendi
bali wanakosa tu subira na kutokutambua kwamba mtoto popote pale na katika
vizazi vyote hufanya makosa na wanachohitaji zaidi ni kuelekezwa kwa upendo
zaidi kuliko hasira.
Frank nimeona hamna namna nyingine ya kumfanya apunguze utundu zaidi ya kumuonyesha upendo
wa hali ya juu pamoja na kumuombea Mungu. Na kwa kweli ameonyesha mabadiliko
makubwa sasa na anapenda kujisomea awapo nyumbani. Kila mzazi angependa mtoto wake
awe na tabia njema, lakini changamoto hujitokeza, ni kwa namna gani utamfanya
afuate yale yaliyokuwa mazuri tu na kuacha mabaya.
Mawasiliano mazuri na mtoto huku ukimtia moyo kuzungumza
yale anayofikiri yeye kuwa ni sahihi itakusaidia kutambua kwanini mtoto
anafanya makosa na itakuwa rahisi kumrekebisha kwa njia ya kumuelimisha
taratibu. Imani pia inasaidia, unapokwenda na mtoto katika nyumba ya ibada, iwe
ni Kanisani au Msikitini huku ukianza kumfundisha taratibu kuwa, kuna Mungu na huwa hapendi watoto wawe
wakorofi nayo inasaidia sana.
Huruma na Upendo vilivyopitiliza kwa watoto kila kiumbe
hasa sisi binadamu tunavyo, lakini usipokuwa makini unaweza ukamharibu mtoto
aidha kwa kuchelea kumfundisha tabia njema au kwa kutumia njia zisizokuwa
sahihi za kikatili mno ukijaribu kumrekebisha.
Nimegundua ukiwasiliana naye vizuri kwa upendo unamjengea
uwezo wa kujiamini na pia uwezo mkubwa zaidi wa kufikiri na kujifunza masomo ya
shuleni na pia yale yaliyomo kwenye jamii inayomzunguka.
Kuna nukuu hii maarufu kutoka kwa mtu mmoja aitwaye ‘Kevin
whately’ isemayo;
“From the time you are a tiny
baby, a parent's love is usually unconditional. Whatever you do, your parents
think you are the tops, but when their memory goes, you stop recouping the love
you've put in” Kevin Whately
Anamaanisha kwamba;
“Tangu ukiwa mtoto mchanga, Upendo wa mzazi hauna masharti, chochote
kile ulichokifanya, wazazi wako walikichukulia kwa umakini mkubwa, lakini
kadiri kumbukumbu zao zinavyopotea ndivyo na wewe unavyoacha kukumbuka upendo
uliojengewa”
Nyingine ni kutoka kwa Bill
Ayers nayo inasema hivi;
“Your kids require you most of all to love them for
who they are, not to spend your whole time trying to correct them.”- Bill Ayers
Akimaanisha kwamba;
“Watoto wako wanachohitaji zaidi kutoka kwako, ni
wewe kuwapenda kama walivyo, na siyo kupoteza muda wako wote ukijaribu
kuwarekebisha”.
Wimbo huu hapa chini
uliimbwa na mwanamuziki Jim Reeves, “But
You Love Me Daddy”(Lakini unanipenda baba) akijibizana na mwanawe wa miaka
mitano 5. Jim alikuwa akimweleza mwanawe kwa lugha ya upendo kabisa jinsi
anavyomsababishia maudhi mengi huku mwanawe huyo akimjibu, “Lakini baba si unanipenda?”
Video ya wimbo "Lakini unanipenda baba";
Audio ya wimbo, lakini unanipenda baba;
Mashairi
ya wimbo “Lakini unanipenda baba” katika kiswahili.
Uso wako wa miaka mitano
Unatia aibu kwa uchafu
Lakini unanipenda baba
Unatupa tupa ovyo midoli yako
Na unapiga sana kelele
Lakini unanipenda baba.
Unajua mwanangu
Unaweza
ukawa mbaya sana
Lakini unanipenda baba
Unaniamsha alfajiri
Wakati ninapotaka kuendelea kulala
Lakini unanipenda baba
Sasa unakula biskuti
Wakati nakukataza
Lakini unanipenda baba
“Ndiyo sababu unaniambia hivyo”
Na umekuwa mgumu sana kukanya
“Kwakuwa
wewe ni wangu wa miaka mitano
Kwasababu unanipenda baba
Nikuvishapo nguo
Unakwenda kucheza na mtoto wa mbwa
Lakini unanipenda baba
Ninapokuwa napiga simu
Huniachi peke yangu
Lakini unanipenda baba
Unamhuzunisha dada yako
Kwa kumvuta nywele zake
Lakini unanipenda baba
Unakwaruza sakafu
Na kuandika katika mlango
Lakini unanipenda baba
Unauliza maswali ya kijinga
Sasa unajua kwamba ni kweli
Lakini unanipenda baba
Sasa unajua kwamba unanipenda
Unakuwa mgumu sana kukanya
Kwasababu wewe ni wangu wa miaka mitano
Kwasababu unanipenda baba.
........................................................................................................
Ungependa pia kusoma makala hizi juu ya watoto?
0 Response to "KWANINI HURUMA NA UPENDO WA WAZAZI WENGI KWA MTOTO HUPITA KIASI?"
Post a Comment