Mwafrika, mtu mweusi tajiri zaidi Duniani
Alhaji Aliko Dangote, biashara zake utazikuta katika nchi nyingi Barani Afrika ikiwemo
Tanzania. Utajiri wake mwaka jana ulikadiriwa kufikia Dola za Kimarekani, milioni
18 “US$18.9” na utajiri huo unatokana na biashara za cementi, sukari na nafaka.
Alianza rasmi biashara miongo mitatu
iliyopita baada ya kukopa fedha za mtaji kutoka kwa mjomba wake kiasi cha Naira
za Kinaijeria 500,000. Mjombake huyo ambaye pia hapo kabla alikuwa amemuajiri
Dangote alimpatia kiasi hicho cha fedha kwa makubaliano kuwa azirudishe baada
ya miezi mitatu. Dangote aliweza kuzirejesha chini ya miezi hiyo mitatu.
Alianza na biashara ya kuuza bidhaa
mbalimbali na kilichomsaidia sana ni kubuni mfumo wa usambazaji bidhaa uliokuwa
wa haraka kushinda washindani wake.
Sasa basi hebu tuanze kuona zile siri 10
zilizomsaidia Dangote mpaka kufikia pale alipo leo hii, ambazo pia Dangote
mwenyewe huwa hapendi kuzificha, huzisema waziwazi kila anapokuwa na fursa ya
kuzungumza na watu kuhusiana na mafanikio yake.
1.
Zalisha na siyo kubakia kuwa mchuuzi tu.
Aliko Dangote alianza biashara zake kama
mchuuzi wa bidhaa wa kawaida mithili ya
unavyoona hapa kwetu wafanyabiashara
wakinunua bidhaa kama nguo, mafuta,
viatu na kisha kwenda kuviuza kwa faida.
Kwa kadiri alivyokuwa akikua Dangote
alijipatia uzoefu mkubwa kibiashara na
hali ya kujiamini. Katika mahojiano yake na vyombo mbali mbali vya habari
aliyowahi kufanya, mara nyingi hupenda kuweka bayana kwamba, mafanikio yake
makubwa kibiashara yametokana na kuhama kutoka uchuuzi wa bidhaa kuwa
mzalishaji wa bidhaa.
Dangote mwenyewe anasema, “Zalisha
na siyo kufanya uchuuzi tu, kuna pesa kwenye uzalishaji , ingawa
unahitajika uwekezaji mkubwa. Ili nitoke, nililazimika kuanza kuzalisha bidhaa
kama zilezile nilizokuwa nikifanyia uchuuzi(nikiuza). Mimi natetea uzalishaji
kwa sababu siyo tu uzalishaji unazidisha hadhi yako katika biashara, bali pia
unakusaidia wewe kama mjasiriamali kurudisha kile ulichokipata kwa jamii yako
na nchi kwa ujumla kwa njia ya kuongeza nafasi za kazi pamoja na maendeleo ya
kiuchumi” Alimalizia Dangote.
2.
Jenga jina na kamwe usiliharibu.
Hii ni siri ya pili ya mafanikio ya Aliko
Dangote, Mfanyabiashara, Mnaijeria na mtu aliyekuwa tajiri zaidi kuliko
mwingine yeyote yule katika Bara la Afrika. Dangote ni muumini mzuri katika “nguvu ya jina” na kifuatacho ndicho
alichotamka juu yake;
“Ili ufanikiwe katika biashara, ni
lazima utengeneze jina na kamwe usiliharibu. Nguvu kubwa ya kiushindani
niliyokuwa nayo wakati nilipoingia ubia katika biashara ya uzalishaji bidhaa ilikuwa ni jina langu
“Dangote” ambalo nililijenga kwa juhudi kubwa katika kipindi changu chote
nilichokuwa nafanya biashara ya uchuuzi wa bidhaa.”-Aliko Dangote
Hebu tuchukulie mifano ya makampuni makubwa
kama vile Coca Cola na Pepsi, utakuta hata kuna wakati thamani ya majina hayo
“brand names” huwa kubwa kushinda thamani halisi ya rasilimali makampuni hayo
yanazomiliki. Hiyo ndiyo nguvu ya kujenga jina zuri la biashara. Sasa kwanini na wewe leo usianze kujijengea
la kwako?.
Jina lako la biashara laweza kuwa mwokozi
wako katika nyakati ngumu kibiashara, linaweza pia kugeuka nguvu kubwa ya
kiushindani katika biashara yako ndogo.
3. Uza bei nafuu, zingatia ubora lakini angalia
usiue ushindani.
Kujenga biashara yenye mafanikio, Dangote
anasisitiza umuhimu wa kuuza bidhaa bora katika bei nafuu. Kuuza bidhaa zilizokuwa bora katika
bei ambayo kila mteja ataimudu. Husaidia katika kuongeza utiifu wa wateja.
Kuhusiana na ushindani, Dangote alikuwa na haya ya kusema;
“ Usiue ushindani, ushindani ni afya kwa
biashara. Unakuweka wewe mjasiriamali katika hali ya kuendelea kufanya jitihada
zako zote ili kutimiza malengo.”
Mjasiriamali mwingine, na aliyekuwa mwanaviwanda, Henry Ford kwa upande wake aliwahi kusema hivi;
“Kuna
kanuni moja kwa mwanaviwanda nayo ni: Tengeneza bidhaa bora kabisa kwa kadiri
inavyowezekana, katika bei nafuu kabisa inayowezekana , huku ukilipa mshahara
mkubwa kwa kadiri inavyowezekana.”- Henry
Ford
4. Anza kidogo lakini ukiwa na maono makubwa.
“Niliunda makampuni na kuwa mtu mweusi
tajiri zaidi duniani hapo mwaka 2008, lakini hili halikuweza kutokea kwa siku
moja. Ilinichukua miaka ipatayo 30 kufikia pale nilipo leo. Vijana wa leo
wanatamani kuwa kama mimi lakini wanataka kufikia lengo hilo kwa usiku mmoja.
Hiyo haiwezi kufanya kazi. Kujenga biashara yenye mafanikio, ni lazima uanze
kidogo na kuota makubwa. Katika safari ya ujasiriamali, ung’ang’anifu katika
kuyafikia malengo ndiyo kila kitu.”- Aliko Dangote
5. Jenga ushirikiano na tafuta ‘mpenyo mkubwa’.
Siri nyingine ya mafanikio ya Dangote ni
ushirikiano kwenye biashara. Aliko Dangote anaheshika kwa mtandao wake imara wa
kibiashara pamoja na ushirikiano wa
kisiasa. Unaweza ukajenga mashirikiano
na kukuza mtandao wako wa kibiashara kwa
kuongeza uwajibikaji wa kijamii, kuingia mikataba ya ubia na ushirikiano,
kuunda ushirikiano/muungano wa kimkakati, kuhudhuria shughuli na mikutano ya
kibiashara, kuchangia shughuli za kisiasa pamoja na kufanya ziara za kihisani.
Kudumu katika biashara, ni lazima uimarishe
ushirikiano wako kibiashara pamoja na mtandao, na muhimu zaidi, ni lazima uwinde ‘mpenyo
mkubwa’(big break). Mpenyo mkubwa ni muhimu mno katika uhai wa kijasiriamali.
Kwa kweli ni vigumu mno kukuta mjasiriamali yeyote mwenye mafanikio ambaye
hakupigwa jeki, kupitia mpenyo mkubwa(Big
breakthrough).
*Mpenyo mkubwa kwa lugha nyingine ni tukio kubwa
maishani lililokuwa na uwezo wa kubadilisha kabisa maisha kutoka hali duni
kuelekea maisha yenye fursa nyingi zaidi
1. Kwa
mfano, Diamond Platnumz alipata
mpenyo wake mkubwa pale alipopata dili la kurekodi kibao cha Mbagala, kila kitu
kilibadilika kuanzia pale!
2. Aliko
Dangote alipata mpenyo wake mkubwa pale alipofanikiwa kupata leseni ya kuagiza
simenti kutoka nje ya Nigeria.
3. Halikadhalika
na Bil Gates mpenyo wake mkubwa ni
pale aliposaini mkataba na kampuni kubwa ya kompyuta ya IBM
4. Je
na wewe mpenyo wako mkubwa (big
breakthrough) ni upi?
6. Amini kuwa unaweza ukatajirika hata ukiwa katika nchi yako ulikozaliwa.
Dangote anaamini kabisa kuwa, ili mtu uweze
kujenga biashara imara na yenye mafanikio, ni lazima uwe na imani thabiti juu
ya nchi yako, uamini kwamba fursa zimejaa tele kila mahali, ila tu
kinachotakiwa ni mtu awe na jicho la kijasiriamali lililokuwa na uwezo wa
kuona fursa hizo pale ambapo mtu wa kawaida asingeliweza kuziona kirahisi.
Anamtia moyo kila mtu kuzitafuta fursa ndani ya nchi zao na siyo kwenda
kuhangaika katika nchi za watu.
7. Fanya kazi kwa bidii.
Bidii!, bidii!, bidii, hivi ndivyo Dangote anavyosisitiza
mara zote anapopata nafasi ya kuwaelezea watu siri zake za mafanikio.Hebu soma
maneno yake mwenyewe hapa chini alivyosema;
“Mwenyewe huwa nafurahia sana maisha lakini
huwa napatwa na furaha zaidi ninapokuwa nafanya kazi. Ninaamini katika kufanya
kazi kwa bidii na moja ya siri zangu za mafanikio kufanya kazi kwa bidii”-
Aliko Dangote.
Ingawa Dangote hufanya kazi kwa bidii sana
lakini hafanyi kazi tu ilimradi amefanya, la hasha, hutumia akili na zaidi ya
yote HUPANGA kabla hajafanya kazi
zenyewe. Mfano mmoja wapo ni mradi wa kiwanda cha cementi cha Dangote Mtwara,
baada ya kufanya utafiti wa kutosha mwishowe aliamua kukiweka kiwanda hicho
Mtwara.
Ni kwa nini asingeamua kukiweka Dar es
salaam, Pwani au hata Mwanza kwenye mawe mengi ambayo yangetumika kama
malighafi rahisi?. Bila shaka kutokana na mipango na upembuzi yakinifu Mtwara ndiyo mahali panapofaa ili mradi/kiwanda
chake kiweze kurudisha gharama zilizotumika.
8. Rudisha
kile ulichokipata kwa wale waliokupatia.
Hata ungelikuwa na juhudi ya kazi vipi lakini
kamwe hauwezi ukasimama na kudai eti mafanikio yako hakukuchangia mtu, wateja
wenyewe wa biashara yako ni moja ya watu wanaochangia ufanikiwe. Huwezi
kutajirika kwa mikono yako mwenyewe. Kuna wafanyakazi, wadau mbalimbali, wabia,
taasisi, makampuni na jamii kwa ujumla wote wana mchango kwako ili ufanikiwe.
Kwa namna moja au nyingine kuna wakati
ulihitaji msaada fulani na ukasaidiwa na watu/mtu fulani ndipo ukaweza kufanikiwa.
Kwa hiyo basi ili waendelee kukupa ‘sapoti’ ama kukuunga mkono, huna budi
kuwakumbuka kwa kuwarudishia sehemu ya kile walichokupa. Kuna njia nyingi za
kuwarudishia ikiwemo, misaada ya kijamii, kufadhili shughuli mbalimbali nk. Dangote
hili ameweza kulitimiza kwa asilimia kubwa sana.
9. Heshimu na kutii sheria za nchi.
Katika hili, masuala kama ya kukwepa kodi
hakuna, inatakiwa kuhakikisha sheria zote na taratibu zilizowekwa na mamlaka
halali zifuatwe. Dangote hushauri wajasiriamali kuwa watu wenye kufuata sheria
za nchi pasipo kupindishapindisha ikiwa nipamoja na kulipa kodi halali.
10.
Ni lazima “ujasiriamali uwe ndani ya damu yako.”
Tabia za kijasiriamali ni lazima uwe nazo, na
hauwezi ukafanikiwa ikiwa hautazitilia maanani na kuziishi. Haitoshi tu kuzijua
kinadharia, kila kitu utakachofanya, ukifikiri, ukiota, ukifanya jambo lolote
lile basi liwe ni biashara na siyo kitu kingine. Roho ya ujasiriamali
utakayokuwa umeipanda kwa jinsi hiyo haitakufa kamwe hata ikiwa wewe kimwili
utakuwa umekufa, yenyewe itaendelea kuishi miaka mingi baadaye.
Ni kama unavyoona wajasiriamali mfano wa kina
Thomas Edison, hata baada ya kufa siku nyingi kampuni lake la General Electrics
badi lipo. Andrew Carnegie kitabu chake Think & Grow Rich ni miaka zaidi ya
70 sasa na bado kinawavutia watu wengi Duniani. Hata Mzee Warren Buffet
aliyewahi kuwa mtu tajiri zaidi Duniani, ingawa ameshazeeka sasa lakini bado
ndani ya damu yake ujasiriamali unaendelea kuchemka.
0 Response to "SIRI 10 ALIZOTUMIA ALIKO DANGOTE TAJIRI NAMBA1 AFRIKA KUTAJIRIKA"
Post a Comment