Ni
kisa nilichokishuhudia mwenyewe kwa macho yangu.
Joyce, siyo jina lake halisi, alikuwa ndiyo kwanza ana
wiki mbili tu tangu aanze kazi ya kuuza duka la tajiri yake jina pia siwezi
nikalitaja hapa kwani hajaniruhusu. Duka hilo la vinywaji baridi mchanganyiko na vileo kama bia
lilikuwa karibu kabisa na mahali nilipokuwa nikifanya shughuli zangu kwa wakati
huo.
Wateja wa aina mbalimbali walikuwa wakifika mara kwa mara
katika ‘pub’ hiyo hasa
nyakati za jioni kwa lengo la kupoza makoo yao.
Siku hiyo kuna kaka mmoja umri wake ni wa makamo hivi,
alifika hapo na baada ya kukaribishwa na yule mhudumu yaani Joyce aliketi na
kisha akaagiza kinywaji (Bia)na kuanza kunywa. Lakini kama
ilivyokuwa ada kwa wateja wengi hasa wa
jinsia ya kiume wanapokwenda katika maeneo vinapouzwa vileo, wengi wao huwa na
malengo zaidi ya kupoza koo. Yule kaka alianza kumtongoza yule mhudumu naye
baada ya kubaini nia yake hakufanya ajizi akaanza kupanga mikakati ya “kumchomoa
noti”.
Joyce kwa kweli katika wiki nzima ile alikuwa akisikika na
majirani wa pale nikiwamo na mimi mwenyewe akilalamika sana juu ya hali ngumu
ya maisha, alikuwa akihangaika sana juu ya namna atakavyoweza kupata pesa kwa
ajili ya kulipa pango la chumba cha kuishi alichopanga ambacho ilionekana muda
ulikuwa mbioni kumalizika. Kwa kweli hata kile kilichokuja kutokea pale
hakikunishangaza sana kwani Joyce alikuwa tayari kwa lolote ilimradi tu azipate
pesa kwa ajili ya kulipa pango hilo.
Basi kaka yule aliendelea kuburudika na kinywaji chake huku
maongezi ya hapa na pale na Joyce yakiendelea. Baada ya kitambo kidogo kupita
majirani tulishitushwa na kilio cha Joyce aliyekuwa akilalamika kwamba pesa
zake zote za mauzo ya tangu jana yake usiku, zaidi ya shilingi elfu sabini
zilikuwa zimetoweka kutoka katika droo ya pesa katika mazingira ya kutatanisha.
Huku mikono ikiwa kichwani na machozi kweli
yakimlengalenga, Joyce aliwafanya wengi wa watu waliokuja kushuhudia tukio lile
waamini kuwa ni kweli lilikuwa limetokea.
Mtuhumiwa wake mkuu aliyedai kuwa ndiye mhusika wa
kuzichukua pesa zie kimiujiza alikuwa ni yule mteja wake, kijana aliyekuja pale
kujiburudisha na bia. Huku akiwa ameketi palepale kwenye kiti kama alivyokuja,
kaka yule alipigwa na bumbuwazi asijue la kufanya, hata kujitetea ilikuwa ni
shida kwa jinsi Joyce alivyokuwa akipiga makelele.
Kwa amaelezo ya Joyce ni kwamba yule kaka mara tu baada
ya kufika na kukaa pale kwenye kiti, alitazama kwenye droo na aliziona pesa
zote zikiwa salama, lakini alidai kwamba baada ya kukaa muda fulani alitazama
tena katika droo na kukuta hamna kitu, pesa zote zimetoweka. Alipoulizwa ikiwa
kuna muda wowote alitoka pale kaunta akaenda nje na kumuacha yule kaka peke
yake pale alijibu kuwa wala hakutoka kabisa na yule kaka wala hakuinuka hata mara
moja pale alipokuwa ameketi.
Aliendelea kusisitiza kuwa kaka yule ni lazima atakuwa
mchawi na huo utakuwa ndio mchezo wake kwenda katika biashara za watu
akijifanya anakunywa kumbe lengo lake ni kuchukua mauzo kwa njia za
kimiujiza(chuma ulete)
Joyce alikataa kata kata kwamba labda fedha hizo zilikuwa
zimechukuliwa na mtu mwingine hapo kabla, labda na vibaka wanaopitapita wakati alipojisahau.
Watu tulishindwa kusuluhisha kwani Joyce
alikuwa akidai arudishiwe fedha za bosi
wake kwani asingekuja kumuelewa pindi ambapo angerudi.
Watu tuliokuwa pale tulishindwa kusuluhisha, ikabidi sakata lihamie kwa
mjumbe, mjumbe naye hakuliweza ikabidi yafike polisi. Kule polisi, sijui tuseme
ndiyo ujanja au ni kitu gani, walimfundisha abadilishe maelezo aliyokuwa
akiyatoa kutokana na sababu kwamba eti serikali haijihusishi na masuala ya
kishirikina.
Walimwambia ikiwa alitaka ile kesi iweze kufika mahakamani basi alikuwa hana budi kuyaondoa kabisa maneno yaliyohusiana na ushirikina au chuma ulete na badala yake aeleze kwamba, pesa zilipotea baada ya mtuhumiwa kufika pale na kuanza kumtomasa tomasa akiwa ndani ya kaunta ya vivywaji.
Walimwambia ikiwa alitaka ile kesi iweze kufika mahakamani basi alikuwa hana budi kuyaondoa kabisa maneno yaliyohusiana na ushirikina au chuma ulete na badala yake aeleze kwamba, pesa zilipotea baada ya mtuhumiwa kufika pale na kuanza kumtomasa tomasa akiwa ndani ya kaunta ya vivywaji.
Kusema ule ukweli, mimi mwenyewe binafsi mazingira ya
tukio nilivyoyaona, kulikuwa hakuna kabisa uwezekano wa mtu kuweza kuiba pesa
ilihali mhudumu akiwa palepale hata ikiwa alimsogelea kiasi gani kwani kulikuwa
hakuna uwezekano wowote wa kuweza kuifikia droo ya pesa. Hata hivyo akiwa
palepale alipokuwa ameketi alisachiwa na hakukutwa na hata senti tano zaidi ya
fedha zake mwenyewe alizokuwa nazo mfukoni.
Huku akiwa haamini macho yake yule kaka alijikuta
akitinga mahakamani, na kesi ikaanza kusikilizwa, wiki zilipita na hata miezi,
kesi si mchezo, iliwagharimu wote wawili si mtuhumiwa tu na hata yule mlalamikaji,
Joyce naye hata ikawa siku zingine hafiki mahakamani. Lakini mwenye haki ni
mwenye haki tu yule kaka wa watu hakukosa mahakamani hata siku moja, hata hakimu baada ya kuona mlalamikaji
haonekani ikabidi atumiwe ujumbe wa
kuitwa mahakamani.
Mwishoni ilionekana dhahiri kabisa kwamba mlalamikaji
hakuwa na ushahidi wowote ule wa maana bali alikuwa tu akilazimika kuhudhuria
mahakama kusudi tajiri yake aamini kweli kama pesa aliibiwa, mwisho kabisa na
kibarua chenyewe kiliota nyasi sambamba na kukatwa mshahara wake pesa
alizodanganya kaibiwa kichumaulete. Huku mahakamani nako yule kijana aliachiwa
huru. Watu walimshauri akamfungulie kesi ya udhalilishaji lakini akasema yote
anamwachia Mungu.
Biashara nyingi hususani zile za rejareja mtindo huu wa wasaidizi
kusingizia Chuma ulete, au masuala ya kishirikina kuwa ndiyo chanzo cha
biashara kuzorota au pesa kupotea umeota
mizizi sana. Bosi usipokuwa mwerevu na wewe ukawa ni mtu rahisirahisi tu wa kuamini
upumbavu huo basi unaweza ukajikuta ukiingia mkenge. Hawakukosea waliosema “Wajinga ndio waliwao” Usikubali kuwa
mjinga wa kuamini vitu vya karne zilizopita, tena visivyokuwa na ushahidi
wowote wa kisayansi.
Kuwa makini na wasaidizi/wafanyakazi wako, tengeneza
mfumo thabiti wa mahesabu ya biashara yako, tenganisha fedha za biashara na
matumizi yako binafsi pamoja na kupata maarifa na mbinu sahihi juu ya biashara
unayoifanya, ndiyo muarobaini wa ko wa kupambana na “Mdudu Chuma ulete”
hatimaye ukaweza kumshinda.
0 Response to "CHUMA ULETE ANAVYOWATESA WENYE MADUKA NA WAFANYAKAZI WAO DAR"
Post a Comment