Ajira siyo laana.
|
Kwa miongo mingi sasa Duniani, kumekuwepo na
mjadala mzito juu ya ajira na shughuli za kujiajiri binafsi au unaweza ukasema
kumiliki biashara mwenyewe. Njia zote hizi mbili, kufanya kazi ya ajira na kumiliki
mradi wa kiuchumi, ni njia za kumfanya binadamu aweze kupata kipato
kinachomuwezesha kuishi hapa duniani.
Katika mjadala huo, kila upande, iwe ni wale
waliokuwa upande wa ajira au wanaotetea suala la kujiajiri, kila upande
unavutia kamba kwake. Lakini mara nyingi upande ule wa ajira binafsi au
kumiliki biashara ndio upande unaoonekana kuwa na nguvu na hata kufika mahali
ambapo karibu kila mtu hushawishika na kuamini ya kwamba kuajiriwa ni kama vile
laana na kujiajiri au kumiliki mradi wa kiuchumi ndiyo “habari ya mjini.”
SOMA: Vijana wanaosubiri mifumo iliyowekwa iwasaidi kujikwamua kiuchumi wataendelea kuwa watumwa wa wengine-Reginald Mengi.
Kujiajiri binafsi ni kweli kwamba ndiyo njia
sahihi na ya uhakika zaidi inayoweza kumhakikishia mtu kipato kuliko ajira
lakini hakuna kitu chochote duniani kisichokuwa na faida na hasara zake.
Kwamfano wakati kujiajiri au kumiliki biashara kunatazamwa kama njia bora zaidi
ya kufikia uhuru kipesa, kuna changamoto nyingi zinazoambatan na kuendesha
biashara tofauti na upande wa ajira ambao mwajiriwa akishaingia mkataba na
mwajiri basi, kazi yake kubwa inabakia kutekeleza yale anayotakiwa kuyatekeleza
akisubiri mshahara wake, haumizi kichwa pesa zitatoka wapi wala ni vipi faida
itakavyopatikana.
Je, Inawezekana kila mtu duniani akajiajiri binafsi?
Dunia kwa jinsi ilivyoumbwa, karibu kila
kitu, viumbe hai na hata vile visivyokuwa na uhai hutegemeana. Ni lazima kitu
fulani kiwepo ndipo na kitu kingine nacho kiweze kuwepo. Hebu tutazame mifano
michache ifuatayo;
Uislamu
na Ukristo.(Religious diversity)
Natumia dhana hii nyeti sana ya dini
kuonyesha uzito wa vitu tofauti vinavyotegemeana hata ikiwa katika mazingira ya
kawaida inategemewa haviwezi kabisa kutegemeana.
Uislamu na Ukristo, kila kimoja kingelipenda
mwenzake atoweke duniani kusudi chenyewe kiweze kuenea maeneo yote duniani.
Lakini kwa bahati mbaya asili haiwezi ikaruhusu jambo la namna hiyo kutokea.
Dini zote hizi mbili zitaendelea kuwepo
duniani milele na milele na wala hamna moja itakayoweza kumtokomeza mwenzake
ili iendelee kuwepo. Hivi ndivyo Mungu alivyoumba Ulimwengu. Moja ikitoweka
basi na ujue nyingine haitakuwepo tena. Duniani kungelikuwa na dini moja tu,
basi hiyo wala isingelikuwa na jina, kwanza haingekuwepo kwa sababu hamna
nyingine ya kuitofautisha nayo.
Mimea
na Wanyama(Ecosystem)
Kila siku wanasayansi hupiga kelele; “Jamani
msikate tena miti ovyo, msiue tembo,…msifanye uvuvi haramu….!” Wanajua kitu
kimoja hutegemea kingine na kinapotoweka basi kile kinachotegemea nacho hakipo
tena. Unaweza ukauliza, “kwani Tembo wana kazi gani, kwanza ni waharibifu
wakitoweka sisi binadamu tuna hasara gani?” Akitoweka Tembo ujue kuna viumbe
wengine wengi na mimea ambavyo navyo vitatoweka. Kwa mantiki hiyo athari hizo
huenda mpaka kwenye kuathiri hali ya hewa, maziwa, mito na hata bahari na
matokeo yake ndiyo kama hayo tunayoyashuhudia sasa hivi, ukame, joto kuongezeka
sambamba na kina cha bahari.
Ajira
na biashara binafsi(kujiajiri) ni vitu viwili vinavyotegemeana sana.
Ukimkuta mtu anakuhubiria kuwa ajira ni
mbaya, ajira ni utumwa, ajira haifai kabisa, hebu mchunguze vizuri, je,
nyumbani kwake hana hata housegirl? Kama ni mwanamume, labda amemfungulia mkewe
mradi mfano wa saluni, je, hiyo saluni mkewe huwa anashinda hapo mwenyewe na
kufanya kila kitu peke yake wateja wanachohitaji?
Nijuavyo mimi asilimia kubwa ya watu
matajiri, huufikia utajiri baada ya kufungua miradi ya biashara zaidi ya mmoja.
Katika kitabu nilichoandika kiitwacho, “MIFEREJI7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA” jambo hili nililielezea kwa
kina sana. Na huwezi ukahudumia mradi zaidi ya mmoja pasipokuwa na wasaidizi
ambao ni lazima tu uajiri watu, penda usipende, vinginevyo basi utajiri uusikie
tu kwa wenzako. Au pengine iwe utajiri huo unaupata kama urithi au umeshinda
bahati na sibu, mambo ambayo ni adimu mno kutokea, katika watu tuseme labda
1000 hutokea watu wa namna hiyo 2 au 3, sasa hebu fikiria ni wangapi
watabahatika?
Kwa upande mwingine napo, kwa kuwa siyo
rahisi kila mtu akawa na rasilimali za kufungua biashara au mradi binafsi wa
kiuchumi, utakuta wale wasiokuwa na biashara hutafuta kazi za kuajiriwa kutoka
kwa wale wenye miradi/biashara au katika taasisi za uma. Hilo hutokea moja kwa
moja ‘automatiki’ kabisa na wala siyo kwa mtu kulazimishwa. Unahitaji pesa kwa
ajili ya kuendeshea maisha, huna mtaji wala mradi wowote, utaishije kama siyo
kuomba kazi ya ajira mahali?
Suluhisho.
Kuajiriwa na kuajiri kulikuwepo tokea enzi za
dahari, na vitu hivi viwili vitaendelea kuwepo huku vikitegemeana mpaka pale
Ulimengu utakapofikia tamati. Cha kuzingatia hapa ni kwamba, binadamu
unapozaliwa mpaka siku ya kufa kwako, hapo katikati hutokea mabadiliko mengi.
Kuna kipindi utaajiriwa na kuna kipindi utaajiri watu. Nyakati hazilingani na
wala siku kamwe hazigandi. Aliyeajiriwa leo siye atakayeajiriwa kesho.
Kuna nyakati fulani watu kama kina Steve
Jobs, Reginald Mengi, Aliko Dangote na wengine wengi waliwahi kufanya kazi za
ajira katika maisha yao iwe ni serikalini au makampuni binafsi, lakini
walichotilia maanani ni kuwa, ajira ilikuwa ni kazi ya mpito kwao na chanzo
kikuu cha mtaji wa kuanzishia miradi yao ya kibiashara. Mwenyezi Mungu hawezi
tu kukuumba tangu unatoka tumboni mwa mama yako wewe uwe ni mtu wa kuajiri watu
tu hapana, ni lazima kuna wakati fulani utawatumikia watu wengine hata ikiwa ni
kwa kazi ya kujitolea. Hata mwanamfalme wa Uingereza kabla hajatawazwa rasmi
kuwa mfalme au malkia, hupangwa kwanza kazi za kuwatumikia watu kama raia
wengine wa kawaida.
Na hii ndiyo maana nasema; “Ajira siyo laana,
bali ichukuliwe kama chanzo kizuri kuliko vingine vyote vya mitaji ya kuanzisha
miradi na biashara binafsi.
……………………………………………………………………….
Mpenzi msomaji, sasa hivi vitabu vyetu vyote
unaweza ukavipata moja kwa moja mtandaoni kwenye simu yako ya
mkononi(smartphone), tablet au kompyuta ya mezani kupitia;
· E-mail
yako au
· Telegram
Wasiliana
na sisi kupitia;
Simu: 0712 202244
/ 0765 553030 / 0689 303098
E-mail: jiunzeujasiriamali@gmail.com
Kucheki vitabu vya biashara na ujasiriamali vya kiswahili
tembelea SMARTBOOKSTZ
Kudownload/kupakua kitabu cha bure cha kiswahili pamoja
na vitabu vingine vizuri 25 katika lugha ya kiingereza bonyeza hapa kujiunga na blogu hii.
0 Response to "AJIRA SIYO LAANA, NI MTAJI WA UHAKIKA KULIKO AINA NYINGINE ZOTE ZA MITAJI"
Post a Comment