Siku hizi sina kawaida ya kwenda kati kati ya jiji la Dar
es salaam kama zamani, na sababu kubwa ni kwamba huwa sina kinachonipeleka huko
mara kwa mara. Hutokea mara moja moja labda ninapokuwa na wateja wanaohitaji
niwapelekee vitabu kama siku ya jana nilipokwenda katika majengo pacha ya Benki
kuu ya Tanzania, ‘BOT’ kumpelekea mteja wangu kitabu cha “Michanganuo ya
Biashara na Ujasiriamali”.
Awali kwenye simu, mteja huyu aliniambia anaishi
Kigamboni hivyo nikifika Feri muda wa saa 10 jioni basi nimsubiri hapo feri
lakini nikiwa njiani akanipigia tena simu na kunijulisha kwamba muda huo
nimkute pale nje ya majengo ya Benki kuu. Nilipofika pale ilikuwa yapata kama
saa 11 jioni hivi, nikapiga namba yake na akanijibu tayari keshaniona nisogee
karibu na geti la benki. Kabla sijavuka barabara yeye alikuwa ndani ya geti mle
Benki, akatoka haraka akavuka barabara na kuja upande wa pili nilipokuwa
nimesimama mimi mkabala na lango la kuingia BOT.
Alikuwa ni kijana mchangamfu sana, baada ya kusalimiana
nikampa kitabu na kisha kumuonyesha vitabu vingine, viwili, kile cha “Mifereji
7 ya Pesa” na “Siri ya mafanikio ya biashara ya Rejareja”. Alivipenda na vyote
akavinunua kwa pamoja.Nilimuona ni kijana mwenye hamasa ya hali ya juu sana ya
mafanikio. Na japo sikuhangaika kumuuliza ikiwa pale Benki kuu anafanya kazi gani,
lakini nilifahamu fika kwamba, Benki Kuu hamna kazi ndogo hata kidogo.
Nilimsihi sana juu ya kuwekeza katika miradi mbalimbali bila kujali ukubwa wake
hasa kipindi hiki akiwa katika kazi ya ajira, “Hakuna tena wakati mzuri zaidi
wa kuweza kupata mtaji wa kuanzisha biashara kama huu, ambapo umeajiriwa
unapata mshahara kila mwezi” Nilimsihi, yeye akawa tu anacheka na
kufurahi. “Bwana Peter nimefurahi sana kufahamiana na wewe, nitakupa e-mail
yangu uwe unanitumia vitu unavyoandika mara kwa mara” kijana alimalizia,
tukaagana na yeye akavuka barabara akikimbia kuelekea kule liliko geti la BOT
ambako kuna mwenzake alikuwa akimuita.
Taratibu nilijiondoa hapo majengo pacha ya Benki kuu
nikielekea maeneo ya Kanisa la Azania Front ili nikapande usafiri
utakaonifikisha kwangu Mbezi. Tayari kigiza kama vile kilikuwa kinaanza kuingia
hivi lakini hata hivyo nadhani ilikuwa bado, ni kutokana tu na mawingu
yaliyokuwa yametanda angani, kwani hata saa 12 na nusu ilikuwa haijafika vizuri.
Nikiwa nashangaa shangaa hapo maeneo, nje kidogo ya
Hoteli ya New Africa (Casino), nikijiuliza, nikapande basi gani, daladala za
kawaida au Mwendokasi, ikanichukua takriban dakika 10 hivi bila uamuzi,
Mwishowe niliamua nisogee mpaka hapo Posta mpya nikaangalie daladala za kawaida
zinazokwenda mbezi. Kila daladala linalokuja ni Temeke, Mwenge na Mmbagala,
punde kidogo likaja la Kimara Suka, niaona ‘isiwe tabu, ngoja nijitose ndani
kitaenda kueleweka tu huko mbele ya safari’. Niliamua nipande la Kimara Suka
ili nikaunganishe jingine la mbezi. Kama kawaida tuliingia garini kwa msukumano
mkubwa mpaka shati nililokuwa nimevaa likachafuka, hata sijui ni kitu gani
nikajua pengine huenda mlangoni palikuwa na grisi au kuna mtu alishika chombo
kichafu kama ndoo ya samaki.
Daladala imekwisha ondoka sasa tukawa tupo mtaani
kuelekea maeneo ya Mnazi mmoja, hapa katikati karibu na jengo la TTCL, vijana wanne
niliokuwa nimeketi nao siti ya nyuma wakawa wanazungumza kilugha cha kwao
mchanganyiko na kiswahili, Kwa haraka haraka mtu ungegundua vijana wale ni wa kutoka
kanda ya ziwa na baadhi yao walikuwa wageni hapa jijini, kutokana na mmoja kati
yao kuwa alikuwa akiongea kwa simu akimjulisha aliyekuwa wakiongea kuwa yeye
kaja Dar kumuuguza ndugu yao hospitali ya Muhimbili.
Mmoja wa vijana hao aliwauliza wenzake, “Mbona
huku Dar es salaam kila baada ya nyumba chache utakuta jengo la benki?”
Mwingine alijibu, “Siku hizi biashara ya mabenki mijini imekuwa dili sana, siyo
kama zamani” Mwingine akadakia; “Inatokana na watu kuendelea, hakuna tena mtu
anayeweka pesa kwenye vibuyu kama ilivyokuwa zamani”. Japo sikuchangia chochote
lakini nilipenda mjadala ule uendelee lakini mara walibadilisha mada ile
wakaendelea ‘kuchapa kilugha cha kwao’. Sikuelewa wanazungumza nini japo
nilisikia wakitajatajaneno ‘milioni’ mara kadhaa.
Gari ilikuwa inafika Magomeni Mapipa sasa, wale vijana
wakashuka, mle kwenye basi likabakia zogo kubwa, kina dada fulani waliokuwa wameketi
mbele yetu wakawa wanawasema wale vijana kwa kutaja kabila lao kuwa ni watu
wanaopenda sana kuzungumza lugha ya kwao na popote pale wanapokuwa huwa hawapendi
tabu ndiyo maana kwenye siti waliyokuwa wameketi walikuwa wakijiachia kiasi
hata abiria wengine waliokuwa wamekaa nao kama mimi kupata kero.
Siti inakaa watu wanne lakini wao walilazimisha tukakaa
watano na bado ukaaji wao wanataka wao wote waegemee kitini huku wewe
ukijitahidi kujiinamisha mbele, na ni watu walioshiba kwelikweli. “Ukimuona kavaa
jaketi, buti na soksi ndefi basi ujue ana pesa, katoka kuuza mifugo au madini,
wanapenda kuficha pesa ndani ya majaketi au kwenye viatu ndani ya soksi”
alielezea mmoja wa wale kinadada.
Ule mjadala mimi haukunipendeza hata kidogo, nikahisi ule
ni kama ubaguzi wa kikabila vile, kitu kisichopendeza hata kidogo na tena
isitoshe kama kulikuwa na mtu wa kabila lile mle kwenye gari asingelijisikia
vizuri, nikamwambia yule dada, “basi jamani makabila kila moja lina kasoro zake,
waacheni vijana wa watu”.
Nilifika zangu Kimara Suka nikashuka na kwenda kupanda
daladala lingine lililonifikisha Mbezi kwa Msuguri.
.................................................................................................
Mpenzi Msomaji wa Blogu hii ya jifunzeujasiriamali, Ikiwa utahitaji vitabu vyetu au huduma nyingine yeyote ile kama vile ya Ushauri basi usisite kuwasiliana na sisi kwa namba za simu ya mkononi; 0712 202244, au 0765 553030 au 0689 303098 au unaweza kutumia emai, jifunzeujasiriamali@gmail.co na pia Telegram ni @petertarimo.
Vitabu vyetu vyote sasa unaweza ukavipata popote pale tanzania na nje ya Tanzania kupitia mtandao wa kisasa wa internet, email, Telegram na Watsaap.
0 Response to "BENKI KARIBU KILA KONA YA JIJI LA DAR ES SALAAM, SIRI YAKE UNAIFAHAMU?"
Post a Comment