BIASHARA YA SODA, MAJI, JUISI, SABUNI NA SIGARA |
Nimekuwa nikifanya biashara ya kuuza bidhaa rejareja kwa
muda mrefu sasa na kuna vitu kadhaa nilivyogundua kutoka kwa wateja wa bidhaa
hizo ambavyo pengine hata wazalishaji wa bidhaa zenyewe au wenye viwanda na
makampuni ya uzalishaji bado hawajavifahamu. Na isitoshe hata wanapofanya
utafiti wa soko la bidhaa zao mitaani hawajisumbui kuwauliza vitu hivyo wauzaji
wa maduka ya rejareja au wamiliki wa biashara zinazouza bidhaa zao. Hawajui
kama wanafahamu siri nyingi sana za kufanikiwa au kuanguka kwa mauzo ya bidhaa
wanazozizalisha.
Muuzaji wa duka au yeyote yule anayefanya biashara ya
kuuza bidhaa rejareja, bidhaa kama vile, maji ya chupa, juisi za matunda na
zile za kawaida, sigara na hata sabuni, unapofahamu siri hizo na ukazitumia
kikamilifu utakuta ukizidisha mauzo yako mara dufu au hata zaidi ya ulivyokuwa
ukiuza hapo awali.
SOMA: Hakuna biuashara isiyokuwa na faida.
SOMA: Hakuna biuashara isiyokuwa na faida.
Sababu
ni kwanini wateja huamua kupenda bidhaa ya kampuni fulani dhidi ya kampuni
nyingine.
Utakuta bidhaa fulani kwa mfano maji ya kunywa,
yanazalishwa na makampuni tofauti A, B na C, lakini jambo la ajabu wateja
wanapofika dukani kununua maji hutaka wapewe maji aina A tu huku B na C yakitoka kwa uchache. Ukiangalia
aina zote za maji wala hazitofautiani kiubora na ujazo ni uleule, kama ni
chumvi, maji yote, A, B na C hayana nk.
Zipo sababu nyingi kwanini wateja huamua kuchagua kununua
bidhaa ama huduma za kampuni fulani dhidi ya nyingine lakini sababu ambayo mimi
nitajikita nayo zaidi hapa leo ni Mtazamo wa wateja(customer Perception). Mtazamo ni kitu kikubwa sana kwa mteja
kuchagua kununua bidhaa ya kiwanda fulani. Na mtazamo wa mteja juu ya
bidhaa unategemea vigezo vingi kama
vile, kifungashio, bei, matangazo nk.
Nitatoa mifano kadhaa, ambayo sitayataja moja wa moja
majina ya bidhaa husika au makampuni, bali nitatumia tu herufi A, B na C
1.
MAJI.
Wateja wanaweza wakawa wanayapenda maji ya kampuni fulani
kwa sababu tu ya mtazamo wao katika chupa yalimowekwa. Sababu inaweza ikawa ni
umbile la chupa, rangi ya chupa, au ukubwa/ujazo. Kwa mfano niliwahi kushuhudia
kampuni moja(tuiite A) wakati fulani maji yake wateja walikuwa wakiyapenda na yalikuwa yakiuzwa kwa wingi sana. Lakini
ilifika kipindi kampuni ikabadilisha rangi ya chupa zake. Kila mteja aliyefika
dukani kununua maji akawa anauliza, “Ni
rangi gani hii waliyotuwekea? Maji hayapaswi kuwa na rangi bwana”
SOMA: Hatua 10 za kuanzisha biashara ya rejareja.
SOMA: Hatua 10 za kuanzisha biashara ya rejareja.
Wateja zamani walizoea chupa nyeupe inayoonyesha maji
kama yalivyo(clear). Lakini sasa rangi ya chupa waliyoweka ilikuwa inayafanya
maji yaonekane kana kwamba yametiwa rangi au dawa fulani vile. Nilishangaa
kuona wateja karibu wote wa maji wakihamia kupenda maji ya kampuni nyingine B
ambayo chupa zake hazikuwa na rangi, zilikuwa ‘clear’. Sijui kwa maeneo mengine
lakini eneo lile zima nilipokuwa na biashara hata na maduka ya jirani
walisikika wakilalamika juu ya kampuni ile kubadilisha rangi ya chupa zake za
maji.
Kampuni hii A, hata kama ikiwa nia yake kubwa ilikuwa ni
kujihuisha upya “rebranding” basi pengine ingeliweza kusuluhisha sintofahamu
hii kwa wateja wake, kwa kuendelea kuzalisha maji ndani ya chupa zote mbili
yaani ile ya zamani isiyokuwa na rangi sambamba na hii mpya yenye rangi, na
kisha kutathmini taratibu jinsi mwenendo wa uitikiaji wa wateja wao
unavyotokea.
2.
SODA
Utawasikia wateja wengi wakikuambia, “Nataka chupa ya zamani” au wengine, “Nipe chupa mpya” na unapowauliza tofauti ya soda iliyokuwepo ndani
ya chupa ya zamani na chupa mpya ni ipi, wengine watakuambia, ya “zamani haina sukari sana” au wengine
pia hudai, “ina sukari zaidi” na
wengine, “ladha zake ni tofauti”.
Basi ilimradi hakuna atakayekupa jibu halisi la kitaalamu la ni kwa nini atake
‘soda ya zamani na siyo mpya’.
SOMA: Mbinu 7 za kutumia ikiwa unatembeza bidhaa za jumla maduka ya rejareja.
SOMA: Mbinu 7 za kutumia ikiwa unatembeza bidhaa za jumla maduka ya rejareja.
Kimsingi soda za kiwanda tuseme labda A, hutengenezwa
sehemu moja na wala hakuna ya zamani wala mpya isipokuwa tu ni yale matoleo ya
chupa ndipo watu huona kama kuna soda ya zamani na soda mpya. Na hii hutokana
na chupa hasa hasa zile za kioo kuwa zinarudishwa tena kiwandani, kuoshwa na
kujazwa soda upya tena na tena. Kwa hiyo hapa ni swala la mtazamo zaidi “perception”
, kuwa ile chupa ya zamani au mpya ndiyo bora zaidi. Pengine kampuni za soda
ingelifaa zijue ni kwanini wateja huchagua chupa za zamani kuliko mpya, au vinginevyo
basi wanapobadilisha waondoe kabisa zile za zamani au kutoa mpya lakini
zilizokuwa na sura ileile kama za zamani, na hilo litaondoa mkanganyiko
unaokuwepo.
3.
SIGARA
Kuna wakati kampuni A ya sigara iliweka mstari fulani
kwenye paketi zake wateja wakaja juu sana hata wengine wakadiriki kususa na
kuhamia sigara za kampuni B. Sababu kubwa waliyokuwa wakiitoa wateja ni kuwa,
sigara mpya za paketi iliyokuwa na mstari zilikuwa zimeongezewa ukali zaidi.
Nilipochunguza nikabaini wala hakukuwa na mabadiliko yeyote ya ladha bali tu
kampuni ilitaka kuzitofautisha paketi za sigara zinazouzwa nje ya nchi na zile
zinazouzwa hapa nchini.
Ilifikia hatua hata wateja wa sigara aina X wakahamia
sigara aina Y ambayo bado paketi zake zilikuwa hazijaanza kuwekewa mistari
ijapokuwa ni sigara za kampuni moja hiyohiyo A wakilalamika aina X ni kali
kupindukia. Kiuhalisia sigara haikuwa
imeongezewa ukali wala kubadilishwa ladha bali ni kutokana tu na mtazamo wa
akili za wateja bada ya kuona ule mstari wakajenga picha kuwa na ladha nayo
ilikuwa imebadilishwa.
4.
JUISI
Kampuni A inayotengeneza juisi za matunda, zamani chupa
zake za juisi zilikuwa na mdomo mwembamba. Wakati fulani walianza kutengeneza
chupa za juisi zilizokuwa na midomo mipana zaidi. Hata hivyo kampuni hii
iliendelea kuzalishaa juisi zenye chupa za aina zote mbili, midomo mikubwa na
midogo.
Nilichogundua ni kwamba, wateja walianza kupenda zaidi
zile juisi zilizokuwa na mifuniko mipana na ikawa sasa kila mteja aliyefika
dukani ukimpatia juisi ya mfuniko mwembamba, mteja huyo anakuwa radhi kukuambia
anakwenda duka jingine. Kumbuka ubora na ladha ya juisi vilikuwa ni vilevile
hakukuwa na kitu kilichobadilishwa isipokuwa upana wa mzunguko wa mdomo wa
chupa peke yake.
5.
SABUNI.
Kampuni A inayozalisha sabuni za miche ilikuwa
vifungashio vya sabuni zake ni maboksi tu peke yake na miche yenyewe ya sabuni
ilikuwa ikipangwa ndani ya boksi ikiwa ‘uchi’. Kampuni nyingine ya sabuni B,
yenyewe ilianza kuvalisha miche yake karatasi ya nailoni kwanza kabla ya
kuipanga ndani ya maboksi.
Nilichogundua ni kuwa wateja walianza kuonyesha mapenzi
zaidi kwa sabuni za miche zilizokuwa zikizalishwa na kampuni B ambazo zilikuwa
zikivalishwa karatasi nyembamba ya nailoni kuliko sabuni za kampuni A
zilizokuwa zikiwekwa ndani ya maboksi yake zikiwa uchi. Lakini hapo pamoja na
mtazamo pia kuna kuongeza dhamani kwa
sabuni za kwenye nailoni za kampuni B
kwani ile nailoni husaidia sabuni kutokupoteza unyevu na kubadilika kuwa ngumu.
HITIMISHO
Kwa wauzaji na wamiliki wa biashara za rejareja kama
vile, maduka ya vyakula/rejareja, vioski, ‘super markets’, magenge na hata
wauzaji bidhaa wanaopanga barabarani, kigezo hiki cha mtazamo wa mteja/wateja
juu ya bidhaa au huduma wanazonunua kutoka kwenu ni kitu cha kutilia maanani
sana.
Unapofahamu mitazamo ya wateja wako, ni fursa nzuri sana
kwako ya kuongeza mauzo zaidi ya bidhaa na huduma zako. Kwa mfano baada ya
kujua wateja wako wengi wanapendelea
maji ya kampuni A zaidi, kutokana na muonekano wa chupa, rangi au chochote kile,
basi huna budi kuhakikisha maji A hayakosekani dukani kwako au kwenye biashara
yako. Halikadhalika ni hivyo hivyo kwa bidhaa na huduma nyinginezo.
SOMA: Chuma ulete anavyowanyanyasa wenye maduka Dar.
SOMA: Chuma ulete anavyowanyanyasa wenye maduka Dar.
Kwa makampuni yanayotengeneza bidhaa za viwandani, kama
maji, sigara, juisi, sabuni, vyakula, pombe nk. Wanatakiwa kujua kwa uhakika ni
nini mitazamo ya wateja wa bidhaa zao hasa hasa wale wa mwisho(walaji).
Wataepuka kutengeneza bidhaa zisizotoka. Wafanye utafiti na kuheshimu matokeo
ya majibu ya utafiti wanaofanya.
…………………………………………………………………………
Ndugu msomaji, endelea kupata elimu ya Ujasiriamali hapa
katika Blogu hii bila kukosa kila siku na Utakapohitaji msaada zaidi ili uweze
kufahamu kwa kina zaidi maswala mbalimbali yahusuyo Ujasiriamali na biashara
katika hatua ya juu kabisa basi usisite kujipatia vitabu vyetu mbalimbali hapa SMARTBOOKSTZ.
Vitabu vya Self Help Books ni tofauti sana na vitabu
vingine vya kawaida kwani vinatoa mafunzo ya kina ya jinsi ya kuanzisha na
kuendeleza biashara kivitendo zaidi kuliko nadharia, unasoma kitu ambacho moja
kwa moja unakwenda kukitumia katika biashara yako, Kitabu kwa mfano cha “Michanganuo
ya Biashara na Ujasiriamali” chenye kurasa 410, kina kila kitu ambacho
mjasiriamali anahitaji kuweza kuanzisha na kufanikiwa katika biashara yeyote
ile.
Uzuri sasa vitabu vyote kutoka SELF HELP BOOKS unaweza
ukavinunua kupitia mtandaoni na malipo ukafanya kwa Mpesa, Tigopesa au mitandao
mingine. Tunakutumia kitabupepe(softcopy) kupitia E-MAIL au TELEGRAM
@petertarimo. Unatutumia e-mail yako au namba ya simu unayotumia kwa telegram
katika namba za simu, 0712 202244 au email: jifunzeujasiriamali@gmail.com
0 Response to "BIASHARA YA SODA MAJI JUISI NA SIGARA: TUMIA SIRI HII KUONGEZA MAUZO × 2"
Post a Comment