Muda mwingi nimekuwa nifuatilia maisha ya
watu wengi maarufu na waliofanikiwa duniani wakiwemo wafanyabiashara matajiri
zaidi wa hapa kwetu Tanzania kama vile Mohamed Dewji, Rostam Aziz, Said Salim
Bakhresa na Reginald Mengi. Nilikuja kubaini kwamba hakuna kitu cha ajabu au
cha kipekee sana mtu kuweza kufanikiwa kiuchumi au kuwa bilionea, siyo elimu
kubwa sana wala akili nyingi sana wala kuzaliwa katika ukoo tajiri sana kunakoweza
kukakufanya wewe uwe tajiri au milionea.
Kikubwa unachokihitaji zaidi ili utajirike au
ufanikiwe kama nilivyokwisha andika miaka kadhaa iliyopita wakati naanza shughuli
hii ya kublogu ni, “Roho ya ujasiriamali”,
unahitaji pia uwe na ndoto(maono), nia thabiti na mpango unaotekelezeka. Vitu hivi
ni vwa kawaida sana na wala hauhitaji kuwa na fedha yeyote ili kuwa navyo.
Lakini bado nafahamu utaendelea tu kuniuliza, kuwa na vitu hivyo peke yake
kunatosha mtu kuwa tajiri?, mbona watu kibao wanavyo na huishia kufa wangali
masikini?.
Jibu langu kwako ni kuwa, hata mimi mwenyewe
sijui, hakuna njia moja rasmi mtu anayoweza akaitumia kutajirika, hata hao kina
Mengi, Dewji, Rostam na Bakhresa unaowaona leo, hawakufuata njia moja
inayofanana, kila mmoja alitajirika kivyake. Katika kitabu cha “Robert Kiyosaki”
‘Rich Dad’s Guide to Investing’, anasisitiza kwamba zipo njia nyingi za watu
kutajirika, alifafanua kwamba, mtu unaweza ukawa tajiri kupitia kurithi mali,
kupitia njia haramu za wizi au ufisadi, na hata kuna wanaotajirika kwa kuoa mwenza
ambaye kwao 'mambo ni safi'. Lakini vyovyote vile mtu anavyoweza kuwa tajiri ukiondoa
njia hizo haramu, haijalishi mtu kapitia biashara gani; ni lazima kuna kitu
kimoja ambacho mabilionea wote duniani huwa nacho kwa pamoja, nacho siyo
kingine bali ni roho ya ujasiriamali(spirit of entrepreneurship).
SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?
SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?
Kwa hiyo ikiwa utapenda na wewe kufanikiwa
kama wao hakuna budi kuwauliza kwa kuwa wameshapita njia hiyo na wanaelewa
kuliko mtu mwingine yeyote namna ya kutajirika. Na si rahisi kila mtu kuwafuata
uso kwa uso na kwenda kuwauliza, ni kwa njia kama hizi, baadhi ya watu kutafuta
historia zao na yale waliyoyafanya na kisha kuwagawia na wengine ambao hawana
muda wa kuyafuatilia.
Sasa tutakwenda kuzitazama njia 10 au hatua
ambazo watu wengi wanaofanikiwa
huzipitia iwe ni kwa kujua ama hawajui lakini ni lazima kwa namna moja
ama nyingine hujikuta wamezipitia katika safari yao ya kutajirika.
1. Huanza na Ndoto au Maono.
Kutajirika huanza na maono. Moja ya kitu cha
bure kabisa Mungu alichotujalia sisi wanadamu ni zawadi ya akili(uwezo wa
kufikiri) Haimgharimu mtu kitu chochote kuota(kuwa na maono) lakini watu wengi
huwa hawajisumbui kufanya hivyo na hata wale wanao kuwa nayo basi huwa na maono
mafupi au kwa maana nyingine huota mambo madogomadogo yasiyoweza kuwatajirisha.
Na mara zote watu wanaoota mambo madogo huendelea maisha yao yote kuwa
masikini.
2.
Hujijengea akilini mtazamo wa watu waliofanikiwa.
Ili kutajirika ni lazima akili yako ifikirie
kama wale watu waliotajirika. Hata kama bado haujaanza kutajirika lakini
inabidi ujijengee uwezo katika akili yako wa kutenda mambo kama wanavyotenda
watu waliofanikiwa. Vitendo hivyo ni kama vile, kuchukua hatari inayotokana na
pesa zako mwenyewe au hata za kukopa, kuwa tayari kupata faida lakini wakati
huo huo kutokuogopa kupata hasara kama ikitokea, kujitoa kikamilifu katika
kukamilisha majukumu ya biashara pamoja na kuwa na uwezo wa kuziona fursa
zilizojificha katikati ya matatizo ambazo watu wengine wa kawaida inawawia
vigumu kuziona.
Unapokuwa na uwezo wa kukabiliana na matatizo
mbalimbali basi ujue wewe unao pia uwezo wa kuzitambua fursa mbalimbali.
Mjasiriamali mzuri ni yule mwenye tabia kama za mwandishi wa habari, mwandishi
wa habari anao uwezo wa kunusa habari popote pale ilipo, na mjasiriamali
anapokuwa ameifundisha akili yake mbinu stahiki huwa na uwezo wa kunusa fursa popote
pale wengine wanapoona mikasa na majanga. Wakati Mzee Mengi anaanzisha kiwanda
cha maji ya Kilimanjaro watu wengi waliamini hawezi kufanikiwa kwa sababu
kwanza waliamini maji ya kunywa huwa hayauzwi bali hupewa tu bure. Sasa hivi
hebu tazama, maji yanauzwa kila kona.
3. Huongeza
ufahamu wao juu ya biashara wanazozifanya.
“Kitakachokufanya
utajirike siyo pesa bali ni maarifa sahihi juu ya pesa” - Kitabu chaSiri za mafanikio: Biashara ya Rejareja.
Kujiongezea maarifa ya biashara kwa
mjasiriamali yeyote yule ni jambo muhimu sana. Matajiri siyo tu hutegemea elimu
walizopata vyuoni ama shuleni bali pia hujifunza kupitia uzoefu wa kila siku
wanaokutana nao katika shughuli zao.Kiyosaki
anakuambia; “Uwezo wa kuuza ni
ujuzi namba moja katika biashara, ikiwa huwezi kuuza, usijisumbue kufikiria
kuwa mmiliki wa biashara”.-Robert Kiyosaki
4.
Hutafuta wazo la biashara lenye uwezo wa kulipa haraka.
Kama uonavyo siku hizi magari ya mwendo kasi na
yale yanayokwenda taratibu, mawazo ya biashara pia kuna ambayo yana uwezo wa
kukutajirisha haraka na yale yatakayo kwenda taratibu kama mwendo wa kinyonga.
Hapa sasa ndipo kazi ya ujasiriamali huanza. Kutimiza ndoto zako ulizojiwekea
utahitaji wazo la biashara unayojua kabisa litakuvusha haraka likifuatiwa pia na
mpango wa haraka unaotekelezeka.
Ninamaanisha kitu gani ninaposema “wazo la
biashara lililokuwa na uwezo wa kulipa haraka?. Ndiyo maana pale mwanzoni
nikatangulia kusema kwamba mjasiriamali anayetaka kutajirika ni lazima
ahakikishe anaongeza maarifa na ufahamu wake juu ya biashara. Hii ina maana
kwamba, dunia imejaa mawazo tele ya biashara, na kwa kweli karibu kila wazo
linao uwezo wa kumletea mtu utajiri lakini kila wazo kuwa na uwezo wa
kumtajirisha mtu hiyo tu haitoshi. Unahitaji wazo lenye uwezo wa kukutajirisha
harakaaa. Wazo la namna hiyo ni lile ambalo kwa wakati huo linashika chati ya
juu zaidi, ikiwa ni bidhaa au huduma basi zina uhitaji mkubwa sana na wateja.
Lina uwezo wa kutatua tatizo kubwa kwa watu na wakati mwingine wazo la namna
hiyo, linakuwa ni tegemeo la kwanza la watu katika mahitaji yao.
SOMA: Siri matajiri wasiyopenda kuitoa.
SOMA: Siri matajiri wasiyopenda kuitoa.
5.
Huwa na watu wao wa mfano(Mentors)
Mtu yeyote anayefanikiwa ni lazima utakuta,
alivutiwa na mtu mwingine ambaye alishawahi kufanikiwa. Kwa hiyo unapotafuta
mtu wa kukupa hamasa au kuwa kama mtu wako wa mfano, angalia yule aliyefanikiwa
tayari katika tasnia uliyokuwepo. Kama wewe unafanya biashara ya usafirishaji,
mwangalie mtu aliyefanikiwa katika sekta ya usafirishaji, mambo yake anafanya
fanyaje na hata kama itawezekana jenga naye ukaribu muwe hata marafiki
atakufunulia siri nyingi za wewe kuweza kutajirika haraka kama yeye. Lakini
angalia sana usije ukaanza kumuomba akupe fedha utaharibu kila kitu. Je, wewe mtu wako wa mfano ni nani?
6. Huanza
biashara.
Dunia ya leo hakuna njia nyingine rahisi ya
kutajirika zaidi ya kumiliki na kuendesha biashara yako mwenyewe. Waangalie
Mabilionea wote duniani, kina Larry Ellison, Bill Gates, Warren Buffet, Aliko
Dangote, Jerry Yang wa Yahoo, Mark Zuckerberg wa Facebook na wengineo kibao,
walianza biashara zao chini kabisa, sijawahi kusikia yupo mmoja wao aliyeanza
na mamilioni ya dola, lakini matokeo yake ni makampuni makubwa kabisa
tunayoyaona leo na ambayo yamewafanya kuwa watu matajiri wakubwa Duniani. Utajiri
uwe tu ni matokeo ya biashara utakayoanzisha na wala isije kuwa eti utajiri
ndiyo lengo lako kuu, utafeli.
SOMA: Siori 10 alizotuymia Aliko Dangote kutajirika.
SOMA: Siori 10 alizotuymia Aliko Dangote kutajirika.
Kwahiyo ikiwa watu waliofanikiwa zaidi
duniani walifika pale walipo kupitia kumiliki biashara tu, basi ni ushahidi
tosha kabisa kwamba ni kweli mtu yeyote anaweza akatajirika kupitia
ujasiriamali. Ikiwa tayari unayo biashara, tengeneza mpango utakaokuvusha
haraka, weka malengo katika kuikuza biashara yako na usichoke kujifunza vitu
vipya. Mwishowe utatajirika hata kama itachukua muda mwingi kidogo zaidi ya
vile ulivyokuwa umepanga.
7. Huunda
timu imara ya biashara zao.
Kujenga biashara nzuri ambayo hatima yake
itakutajirisha unahitaji kujenga timu nzuri ya watu ambao watakusaidia katika
kutimiaza ndoto zako hizo. Watu hawa siyo lazima wawe ni wale wafanyakazi tu
hapana, kuna watu wengine kama vile, washauri, makundi ya kubadilishana mawazo “mastermind
groups”, wadau mbalimbali kama, wateja,
wanaokusambazia bidhaa nk.
Kwa mfano unapokuwa na timu nzuri ya
wafanyakazi, unavutia hata wawekezaji au wabia na hata unaaminika zaidi na wale wanaokukopesha.
Mtu kama Mzee Bakhresa utakuta katika timu yake ya usimamizi ameweka watu makini
sana, na hata wakati mwingine hulazimika kuajiri watu kutoka nje ya nchi ikiwa
utaalamu unaohitajika hawezi kupata watu kutoka hapa. Hakuna mtu yeyote duniani
aliyewahi kutajirika mwenyewe. Wote utakuta walikuwa na timu za washaurin na
wafanyakazi ambao wakati mwingine wana ujuzi hata kuwashinda wao wenyewe.
8. Hutafuta
mtaji wa kuendeshea biashara zao.
Hapo juu tulishaona anayefanikiwa kuwa tajiri baada ya kupata wazo la biashara yenye uwezo wa kulipa haraka, na
hatimaye kuanzisha biashara yenyewe kwa mtaji kidogo aliokuwa nao sasa tutaona
hatua nyingine wanayopitia ambayo ni hatua ya kupata mtaji wa kulitekeleza lile
wazo kikamilifu. Unaweza ukapata mtaji kutoka kwa wabia, au wawekezaji binafsi
wanaoweza wakawekeza pesa zao katika wazo lako hilo kwa makubaliano ya kuja
kugawana faida itakayopatikana. Njia nyingine pia ni mikopo ya benki au taasisi
za fedha.
SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara uipendayo.
SOMA: Njia 7 za kupata mtaji wa biashara uipendayo.
Lakini njia zote hizi zina hasara zake ambazo wakati mwingine
watu huzikwepa mpaka pale wanapokuja kufikia hatua wameshatengemaa kabisa ndipo
huzitumia kama kichocheo. Kwa mfano makampuni makubwa karibu yote ya mitandaoni
kama facebook, yahoo, google, Apple na hata Amazon, wote hawakukurupuka kwenda
kukopa pesa za watu, walikomaa kwanza na mitaji yao mpaka pale kilipoanza
kueleweka. Na unapofikia hatua kama hiyo, utachagua mwenyewe ukakope wapi kwani
wakopeshaji hukufuata wenyewe wakikuomba wakukopeshe. Ushauri wangu kwako: na
wewe jaribu kwanza njia hii kabla hujakwenda kukopa au kutafuta mbia ndipo baadae ukatafute mtaji kutoka mahali pengine.
9. Hufanya
biashara zao katika mfumo wa makampuni.
Mabilionea karibu wote duniani, sidhani kama
yupo anayeendesha biashara ya mtu mmoja, “sole proprietorship”, huunda
makampuni ambayo hata yakifilisika mali zao zingine haziwezi kisheria kukamatwa
ili kufidia madeni yao. Vile vile kupitia mfumo huo wanakuwa na wigo mpana
zaidi wa uendeshaji biashara zao kwani huajiri wasaidizi mbalimbali wa
kuendesha biashara. Hata mtaji inakuwa rahisi kupata hasa inapofikia hatua
kampuni ikawa na uwezo w kuingia katika soko la hisa.
10.
Huwekeza katika biashara zingine.
Hii sasa ndiyo ile hatua rahisi kabisa ya
mchakato wa mtu yeyote yule anayetaka mafanikio ya utajiri. Uwe tayari umesha
kuwa bilionea au bado upo katika ngazi ya umilionea, kuendelea kubakia kileleni
au kupiga hatua zaidi ni lazima ukubali kutumia mkakati na mbinu ya kuwekeza
kwenye vitegauchumi vingine vingi zaidi ya kile unachomiliki. Na hapa sasa
ndipo utakapoona umuhimu wa kufanya kazi na timu ya watu kama tulivyozungumza
hivi punde.
Mwisho, kupata mafanikio kipesa au kuwa
tajiri ni kitu ambacho kila mtu anao uwezo wa kukifikia, lakini watu wengi tunashindwa
kufanya hivyo kwa sababu moja tu, “Tunaogopa mno kulipa gharama ya kufikia
hatua hiyo na kuamua tu kubakia kuwa katika maisha ya kawaida tuliyoyazowea”.
Ikiwa unayo ndoto ya siku moja kuja kuwa bilionea tajiri kama walivyo kina
Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa, Mohamed Dewji, Rostam Aziz na wengineo,
basi huna budi kufuata hatua zilizotajwa hapo juu. Na zaidi ya yote unatakiwa
kuwa mvumilivu. Hakuna kinachoshinda
uvumilivu.
....................................................................................................
Ndugu msomaji wa blogu hii, kama ulikuwa hujasoma kitabu cha "Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio", tunachokitoa bure baada ya mtu kujiunga na blogu hii, tafadhali KIDOWNLOAD HAPA mapema ili uweze kukisoma au kukihifadhi kwa ajili ya kuja kukisoma hapo baadae. Mwisho wa ofa hii ni hivi karibuni, kitabu hiki kitaanza kuuzwa kama vitabu vingine na bei yake itakuwa ni Tsh. 5,000/= Asante.
Vitabu vyetu vingine vinapatikana kwa njia za E-mail au Telegram mtandaoni na pia ukihitaji vitabu vya karatasi navyo vipo, ila bei hutofautiana. Mtandaoni bei ni nusu ya vitabu vya karatasi. Kwa maelezo zaidi Fungua ukurasa huu wa SMARTBOOSTZ.
Kwa mawasiliano ni;
0712 202244, 0765 553030 na 0689 303098
Telegram: @petertarimo
e-mail: jifunzeujasiriamali@gmail.com
....................................................................................................
Ndugu msomaji wa blogu hii, kama ulikuwa hujasoma kitabu cha "Kanuni ya kujifunza elimu ya pesa na mafanikio", tunachokitoa bure baada ya mtu kujiunga na blogu hii, tafadhali KIDOWNLOAD HAPA mapema ili uweze kukisoma au kukihifadhi kwa ajili ya kuja kukisoma hapo baadae. Mwisho wa ofa hii ni hivi karibuni, kitabu hiki kitaanza kuuzwa kama vitabu vingine na bei yake itakuwa ni Tsh. 5,000/= Asante.
Vitabu vyetu vingine vinapatikana kwa njia za E-mail au Telegram mtandaoni na pia ukihitaji vitabu vya karatasi navyo vipo, ila bei hutofautiana. Mtandaoni bei ni nusu ya vitabu vya karatasi. Kwa maelezo zaidi Fungua ukurasa huu wa SMARTBOOSTZ.
Kwa mawasiliano ni;
0712 202244, 0765 553030 na 0689 303098
Telegram: @petertarimo
e-mail: jifunzeujasiriamali@gmail.com
Nimefurahia sana masomo ya ujasiliamali, naomba kufahamu kama mna tawi la ofisi Arusha au Kilimanjaro?
ReplyDelete