Hakuna kitu kinachomkwamisha mjasiriamali mdogo kama
mtaji, jijini Dar es salaam kuna watu wengi wanaoishi kwa kufanya biashara
ndogondogo ambazo kwa haraka haraka mtu unaweza ukajiuliza watu hao ni kwa
namna gani huweza kupata faida wakaendesha maisha yao na hata wengine kuishia
kukuza mitaji yao na kufikia hatua ya kuanzisha biashara kubwa kubwa au za
kati. Kitu kingine cha kushangaza zaidi ni kuwa nyingi ya biashara hizo wala
hazihitaji gharama kubwa kama za kulipia pango la fremu ya biashara au kukata
leseni na kulipia kodi ya mapato.
Biashara ya nguo za mitumba na kutembeza vitu huhitaji mtaji kidogo kuanzisha. |
Biashara za namna hii wengi huziita sekta isiyokuwa rasmi,
umachinga au biashara ambazo bado hazijarasimishwa. Kuna faida na hasara za
kufanya biashara za namna hii lakini kwa mfanyabiashara mwenye mtaji kidogo yeye
hawezi kuangalia hasara zake, huangalia faida zake tu kutokana na sababu kwamba
hata ikiwa angetaka kufanya biashara iliyokuwa rasmi kikwazo cha mtaji wa
kutosha kuanzisha ni lazima kingemzuia.
Mtaji kwa ajili ya kuanzisha biashara nyingi ndogo siyo
mkubwa sana, zipo zinazoweza kuanza mpaka na shilingi elfu tatu, elfu 5 na
kuendelea, itategemea ni biashara ya aina gani mtu anataka kuanzisha. Moja ya
faida kubwa ya biashara za mtaji kidogo ni huo urahisi wa kupata mtaji.
Mjasiriamali hana kazi kubwa ya kuanza kuzunguka mabenki au kwa wakopeshaji
wengine wakiwemo vyama vya kuweka na kukopa, saccos au ndugu jamaa na marafiki
ili kujipatia mtaji wa kuanzisha biashara.
Biashara nzuri yenye mtaji mdogo siyo lazima mtu kuwa na
eneo kubwa wala eneo lenye watu wengi sana ndipo aanzishe, mjasiriamali anaweza
kuwapelekea bidhaa/huduma popote kule wateja walipo, wapo wengine kama mama
huyu hapa, mama mwakipesile niliyemkuta kwenye gari akiuza viungo mbalimbali
vya chain a masala kama mdalasini, tangawizi, mchaichai, asali mbichi, mlonge
nk.
Kama unapita maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam
muda wa jioni utakutana na wafanyabiashara wengi wanaofanya biashara hizi
zisizokuwa rasmi kandokando ya barabara, stendi za mabasi, na barazani mwaa
nyumba wanamoishi watu. Kimsingi haya ni maeneo ambayo mara nyingi huwa
hawayalipii chochote na hata kama hulazimika kulipia basi ni ushuru kidogo sana
ambao hauwezi ukaathiri kwa kiasi kikubwa faida wanayoipata.
Ubaya au hasara ya miradi ya aina hii ni kutokuwa na
uhakika, kwani maeneo yanayotumiwa mara nyingi kama ni biashara inayotakiwa
kupangwa mahali kama barabarani na stendi za mabasi, maeneo hayo utakuta
serikali haitaki watu kuyatumia kwa biashara. Serikali hudai wanaharibu
mpangilio wa mji na kweli ikiwa ingeruhusu kiholela watu kutumia eneo lolote hata
pale nje ya ikulu ungekuta watu wanapanga biashara.
Wafanyabiashara ndogondogo jijini wakiuza bidhaa zao mitaani. |
Ili mjasiriamali kukwepa kikwazo hiki cha marufuku ya
serikali anapaswa kuwa mbunifu zaidi kwa mfano, kupanga biashara yake muda
ambao serikali haihangaiki na mtu kama masaa ya jioni, kubuni biashara
isiyochukua eneo kubwa kwa mfano biashara ya kuuza kadi/vocha za mitandao ya
simu za mkononi pamoja na kuuza biashara zile mtu unazoweza kuzunguka nazo
kwenye begi au mfuko wako kama viungo, nguo, viatu na bidhaa ndogondogo.
Biashara
ndogo ndogo unazoweza kufanya Dar kwa mtaji mdogo sana pasipo hata kulipa pango
la fremu ya biashara.
Orodha ya baadhi tu ya biashara hizo ni hii ifuatayo, ila
na wewe ndugu msomaji unaweza ukaongeza na za kwako kwani zipo nyingi;
- Biashara ya kuuza vyakula, baba na mama lishe.
- Biashara ya kuuza mahindi ya kuchoma au ya kuchemsha
- Biashara ya kuuza mihogo ya kukaanga au ya kuchoma
- Biashara ya kuuza mishikaki
- Biashara ya kuuza vitu vya kutafuna kama karanga, ubuyu, kashata, miwa nk
- Biashara ya kuuza mihogo mibichi na nazi za kutafuna kwa njia ya kutembeza mitaani.
- Biashara ya kuuza matunda kama maembe, machungwa, matango, mananasi na mafenesi.
- Biashara ya kuuza vocha na line za mitandao ya simu mbalimbal.
- Biashara ya kuuza vyombo na vitu vya majumbani.
- Biashara ya kuuza viatu na nguo za mitumba
- Biashara ya kuuza maji baridi, soda na juisi.
- Biashara ya kuuza samaki
- Biashara ya kuuza uji
- Biashara ya kuuza mandazi, chapatti, kalimati, ufuta, vitumbua, mikate, skonzi, sambusa na visheti
- Biashara ya kuuza vifaa vya umeme
- Biashara ta kuuza nyama za kuku za kukaanga
- Biashara ya kuuza urembo
- Biashara ya kutembeza rangi za kupaka kucha na kusafisha
- Biashara ya kusuka rasta za kimasai chini ya mti
- Biashara ya kuuza juisi ya miwa kwa mashine ya kuzungusha kwa mkono
- Biashara ya kuuza maji ya kufunga(Kandoro)
- Biashara ya kuuza sigara za rejareja
- Biashara ya kuuza karanga nk.
Biashara hizo nyingi kama nilivyotangulia kusema,
hazijapewa ruhusa rasmi na serikali
hasahasa maeneo zinakofanyikia. Lakini kwa mjasiriamali anayetafuta kujikwamua
kwa lengo la kupata mtaji wa kuanzia hana budi wakati mwingine kujikuta
anakiuka sheria, hata hivyo serikali sasa inaonyesha ina nia ya thati
kuhakikisha maeneo mengi yakutosha yanaandaliwa kwa ajili ya wajasiriamali
wadogo wasiokuwa na mitaji ya kutosha au hata wenye mitaji midogo sana kama ya
kuanzia shilingi elfu 10 nao kupata mahali pazuri pakufanyia biashara zao.
...................................................................................................
Ndugu
msomaji, napenda kuchukua nafasi hii kukujulisha juu ya kuanzishwa Darasa la
Michanganuo ya biashara ambalo linaendeshwa mtandaoni katika blogu ya MICHANGANUO YA BIASHARA. Unapojiunga na
darasa hili unajifunza kila kitu kuhusiana na mipango ya biashara kuanzia namna
ya kuandaa mpaka michanganuo yenyewe halisi.
Kiingilio
mtu anapaswa kununua kitabu cha MICHANGANUO NA UJASIRIAMALI ambacho ni shilingi
10,000/= Unatuma fedha na Email yako ya GMAIL kisha tunakutumia kitabu pamoja
na kukuunganisha na blogu hiyo utakayoweza kuingia na kujifunza kozi hiyo.
Kwa
maelezo zaidi kuhusu darasa hilo fungua hapa(Tanzania Online School Of Business Planning)
Vilevile
vitabu vyetu vingine, kama MIFEREJI YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA
na SIRI YA MAFANIKIO YA BIAHSRA YA REJAREJA, vipo na ukihitaji tunakutumia pia kwa email.
SIMU:
0712 202244 AU 0765 553030 Peter Augustino Tarimo
Kaka nimependa kweli umelenga watu wenye kipato kidogo sana na hata umeonyesha njia kabisa za kufanya.
ReplyDeleteila website bado haina muonekano wa kuvutia ukipata msaada wa template nzuri utafanya watu wengi zaida wavutiwe
elisante Shibanda.
Tech blogger ecltech.blogspot.com
Asante sana Elisante kwa ushauri na pongezi,kuhusu template nitawatafuteni.
Delete