Kuna wakati unaweza kukabiliwa na uchaguzi mgumu, uamue
kati ya mambo mawili ambayo yote yanakuogopesha na kuona kila moja baadaye
unaweza ukakabiliwa na matokeo mabaya katika maisha yako. Mara nyingi watu
huamua kubaki vilevile walivyo na maisha waliyoyazoea huku wakiahirisha uamuzi
muhimu juu ya mustakabali wa maisha yao.
Vipindi hasa vya mwaka mpya unapoanza kama sasa hivi
2017, mara nyingi ndiyo muda muafaka kwa mtu kujichunguza kama kuna jambo
lolote maishani mwako ambalo linahitaji kufanyiwa maamuzi muafaka lakini ukawa
unasitasita kwa muda mrefu ukihofia kufanya maamuzi(mabadiliko) kwa madai
kwamba pengine mabadiliko hayo yanaweza kukuletea balaa zaidi kuliko ambavyo
ulikuwa ukiishi zamani.
Kama binadamu tuna mambo mengi tunayoweza kuhitaji kuamua
au kufanyia mabadiliko, kwa mfano unaweza ukawa unaishi maisha magumu pengine
kwasababu tu kazi unayoifanya hailipi, mshahara ni kidogo nk. maisha na
mafanikio kwako unayaona yatabakia kwa muda mrefu kuwa ndoto kwa sababu tu ya
biashara uliyokuwa ukiifanya zamani na ambayo mpaka leo hii unaendelea nayo
haikupi faida ya kutosha, ni ngumu, haina wateja wa kutosha, ama ni biashara
isiyokua kimtaji.
Kimsingi, ugumu wa maisha hautokani tu na maisha tuliyokuwa
tukiishi na ambayo tunaendelea nayo mpaka sasa, bali hutokana hasa zaidi na
ugumu wa akili zetu kukubali kubadilika.
Sasa
Ikiwa Suluhisho Ni Kubadilika, Mbona Watu Huwa ni Wagumu Hivyo Kubadilika?
Sababu kubwa ni kwanini watu huhofia mabadiliko, wakati
kubadilika ndiyo suluhisho ni kwamba, watu wanaogopa mno matokeo mabaya yanayoweza
kutokea baada ya kubadilika. Kuna mifano mingi sana. Jamaa mmoja yeye anafanya
biashara ya kuuza samaki kwa miaka mingi sasa. Lakini kutokana na kuishi mbali
mno na Feri(anaishi Kibaha Kongowe) faida karibu yote ya biashara yake huishia
njiani kama nauli na ana familia kubwa inayomtegemea.
Watu walimshauri na hata yeye mwenyewe kufikiria kuachana
na biashara ya samaki na kuanzisha biashara ya kuuza mkaa ambao huupata karibu
na eneo analoishi. Bwana huyu mpaka dakika hii ninapoandika hapa hajaweza
kuamua kuachana na samaki japo kila siku husikika akilalamika haimlipi.
Anazeeka na biashara ile wakati fursa za biashara nyingine zipo nyingi na
zinaendelea kuzaliwa kila leo.
SOMA: Unaijua siri hii ya kufanikisha biashara yako?
SOMA: Unaijua siri hii ya kufanikisha biashara yako?
Wasiwasi wake mkubwa ni kwamba , Je, akiacha biashara ya
samaki aliyoizoea kwanza watu waliomzunguka watamfikiria vipi?, familia
itaishije siku atakazokuwa akiiboresha hiyo biashara mpya?, je, na kama hiyo
biashara mpya haitaleta faida atafanyaje?.
Kifupi ni kwamba jamaa huyu anajijengea mwenyewe
mazingira ya kwamba kuachana na biashara yake ya zamani isiyomlipa vizuri na
kuingia biashara mpya asiyokuwa na uhakika nayo kisha kwa bahati mbaya ikaja
kuyumba, itakuwa kwake kama ndiyo mwisho wa dunia vile. Anahisi kama hakuna tena
kitu kibaya kwake maishani kama hicho.
Uamuzi wake wa kuachana na biashara ya samaki na kuanza
biashara nyingine itakayompa uhuru kifedha na kimaisha ungeliweza kuwa rahisi
tu kama asingelifikiria zaidi mambo mabaya(hasi) yanayoweza kuja kutokea.
Lakini ukweli ni kwamba suala la matokeo wala haliwezi likawa na uzito kiasi
hicho, hebu fikiria ni mara ngapi katika maisha yako uliwahi kuona kabisa sasa
huna tena pa kutokea lakini muda ulipofika ukashangaa mambo yamepita salama?
Hata ulipokuwa shule ya msingi au sekondari, hebu kumbuka
ulipofanya kosa kubwa, wakati unasubiri siku ya jumatatu paredi(mstarini) uitwe
mbele na mwalimu mkuu na kupewa adhabu kali ya viboko, unashangaa siku hiyo
wala mwalimu mkuu mwenyewe hatokei shuleni, unasikia eti mara amesafiri kikazi
na wala hupewi tena adhabu yeyote, mambo yanayeyuka kimyakimya. Maisha ndivyo
yalivyo. Sasa hebu niambie, ingelikuwaje kama ungeliamua kujinyonga kwa hofu?
Watu wengi huamua kwa woga kuendelea kuvumilia, huku
wakifanya vitu/shughuli zisizowaridhisha hata kama zitagharimu muda wote wa maisha yao badala ya kuamua kubadilika na
kufanya vile vitu wanavyovipenda maishani na vilivyo na uwezo wa kuwapa faida
zaidi.
Unapoamua na kujitoa kiukwelikweli, ukajiambia “sasa basi
inatosha, mimi ninao uwezo wa kukabiliana na chochote kile kitakachojitokeza
mbele ya safari yangu hii ya mabadiliko kutoka hali duni niliyokuwa nayo
zamani(kazi au biashara)”. Hakika kweli utakuwa umefanya uamuzi wa busara na
hakuna lolote lile baya litakalokupata, na hata kama ikiwa hautafanikiwa kwenye
hiyo biashara au kazi yako mpya, MAISHA YATAENDELEA TU WALA HAUTAKUWA NDIYO
MWISHO WA DUNIA.
Mabadiliko
ni kama vile unavyofungua plasta kutoka katika kidonda ambacho bado ni kibichi
hakijapona sawasawa, panauma ghafla kwa nguvu lakini plasta ikishabanduka tu,
unapata ahueni na mambo yanakwenda kama kawaida
Maisha mtu unaishi mara moja tu, na sidhani kama
ungependa miezi 12 ijayo uje useme tena, “laiti ningelijua, ningelifanya hivi
au vile. Fanya leo, fanya sasa hivi, wakati ndiyo huu.
Hebu nikupe zoezi kidogo ambalo hata na mimi nalifanya
sasa hivi na nitakupa mrejesho wangu baadae hapo chini kwenye sehemu ya maoni.
1. Chagua
jambo moja ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikuumiza kichwa chako kufanyia
maamuzi, jambo lolote lile, laweza hata kuwa ni kazi, biashara, eneo unaloishi,
matumizi ya kileo, kufanya ibada, kuachana na nyumba ndogo/mchepuko nk. Amua
kufanya mabadiliko/maamuzi sasa hivi kabla hata haujamalizia kuisoma makala
hii.
2. Ukiweza,
weka maoni yako hapo chini kwenye kisanduku cha maoni, ukitueleza kuwa
unakwenda kubadilika sasa hivi. Siyo lazima uweke jina lako hapo au utambulisho
wako wowote ule, unaweza kutumia ‘Anonymous’
3. Kitu
kingine muhimu ni kwamba, kama makala hii ina kitu chochote kile chenye manufaa
kwako, tafadhali, ingekuwa jambo jema sana kama ukimshirikisha/ukiwashirikisha
na wale wote unaowajali kupitia mtandao wa kijamii wowote ule iwe ni facebook,
twitter, google nk. Usisahau pia kuwajuza kuhusiana na kampeni yetu
inayoendelea ya,
#JIRUDISHIEUKUUWAKOTENA au #MAKEYOURSELFGREATAGAIN
Ukihitaji
vitabu vyako vya biashara na Ujasiriamali kwa lugha ya Kiswahili, usisite
kutembelea ukurasa ufuatao, >>SMARTBOOKSTZ
Mhamasishaji na mwandishi wako,
Peter A. Tarimo
0712 202244
0765 553030
0 Response to "USIOGOPE, MABADILIKO YA MAISHA NI KAMA PLASTA IKISHABANDUKA KIDONDA HUPOA CHENYEWE"
Post a Comment