BIASHARA YA MITINDO YA NGUO ZA KIUME NA VIATU INAVYOWEZA KUKUTAJIRISHA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA MITINDO YA NGUO ZA KIUME NA VIATU INAVYOWEZA KUKUTAJIRISHA

Inawezekana ulikuwa na wazo la kuanzisha biashara ya kuuza nguo za kiume au kwa maneno mengine mitindo ya nguo za kiume ukijumuisha kushughulika na vitu kama, nguo za kiume, majeans, suruali za kitambaa, mashati, viatu vya kiume, mikanda, saa, kofia, suti za harusi na hata suti za kuvalia katika hafla na sherehe mbalimbali, au tayari unayo biashara ya namna hiyo na ungependa kuzijua siri za kufanikiwa katika biashara hii.
Hapa chini nitaorodhesha vitu(dondoo) muhimu sana ambazo wanaume karibu wote duniani hupendelea wanapokwenda kufanya shopping ya nguo zao au ukipenda ‘viwalo’ vya aina mbalimbali. Kwa kuzifahamu dondoo hizi muhimu, muuzaji wa fasheni za wanaume utakuwa katika wakati mzuri zaidi wa kulihudumia kikamilifu sokolako au wateja wakawa wanarudi tena na tena kila nguo, kiatu au chochote kile walichonunua kwako kinapokwisha.

§  Wanaume wengi wana tabia ya ajabu sana, kwani huwa hawapendi kabisa kwenda dukani kununua nguo ovyo ovyo hasa wanapokuwa peke yao, na hata wanapokuwa na wenzi wao yaani wake, kwa wale waliooa, basi huwa ni kwa mbinde kwelikweli! Ni lazima “wakokotwe” mithili ya mbuzi anayevushwa mto. Na hata wanapokubali basi ujue nguo wanazopendelea mara nyingi huwa ni zile za kawaida kama vile jeans au nguo nyinginezo zilizo katika fasheni.

§  Wanaume wengi utakaokuta wakinunua nguo mara kwa mara ni wa umri kati ya miaka 18 mpaka 36 au 40.

SOMA: Ni kwanini ukibuni kitu kizuri ni hatari?

§  Kitu cha kwanza mwanaume atakachotaka kufahamu kutoka dukani kwako au sehemu yeyote anayokwenda kununua nguo ni, saizi ya nguo ama kiatu anachohitaji. Akigundua unababaika kutafuta saizi anayoitaka basi ujue yupo radhi hata kuondoka. Ukiwa mfanyabiashara mjanja wa fasheni za kiume, jitahidi kupanga kila saizi mahali pake na ujue kabisa wateja wako wengi huwa wananunua zaidi nguo ama viatu vya saizi ipi, kusudi uweke stoku ya kutosha ya saizi hizo wanapofika kununua usiwavunje moyo kwa kuwaambia “hakuna saizi yako”.

§  Siku hizi kuna teknolojia za kisasa kama vile ‘apps’ za smartphones zenye uwezo wa kuonyesha kila kitu kilipo dukani na wateja kwa kutumia teknolojia ya ‘wifi’ wanaweza wakajiunga na app hiyo.

§  Wanaume hupendelea kuona vitu ‘live’ au kuelekezwa kwa kutumia mfumo uliotengenezwa maalumu na wala siyo kuulizauliza maswali. Unawez pia kuweka mpangilio wa nguo zako kwa namna ambayo mtu anapofika basi huweza mara moja kufahamu kila kitu kilichopo pale ni kitu gani, saizi yake ni ipi na bei ya kuuzia.

§  Tofauti na mwanamke, mwanaume hujali sana kuhusiana na ni lini, wapi na katika mazingira gani anatakiwa kuvaa nguo fulani na kuna maeneo manne muhimu wanayozingatia pindi waendapo kununua nguo nayo ni;

                 i.    Kazini; Huchagua mavazi yanayoendana na kazi wanazozifanya, kwa mfano kama ni mwalimu zipo nguo zinazoendana na waalimu, kama ni fundi makenika pia atanunua maovaroli nk.

               ii.    Nyumbani na mitaani: Huva nguo za kawaida na mfano wake ni jeans na tshirt ambazo hupenda sana kuvaa siku za weekend wakiwa na ndugu jamaa na marafiki. Kwa kawaida wanaume hawana mitindo ya nguo mingi kama walivyo wenzao wanawake. Ukiacha suruali za vitambaa, majeans, mashati na kanzu.

             iii.    Sehemu rasmi: Ni uvaaji wa wanaume wakati wanapohudhuria hafla na sherehe mbalimbali au kwenye shughuli za kiofisi zinazohusisha ugeni mkubwa. Mara nyingi nguo hizi huwa ni suti, tai na kiatu kizuri cha ngozi au wakati mwingine utamkuta mwanamme kavalia mavazi ya vitenge.

             iv.    Nusu rasmi nusu kawaida: Uvaaji huu ni maalumu hasa mwanamme “anapotoka out” au kuwa na miadi na mwanamke. Anaweza akachanganya suruali ya jinsi(jeans) na shati la kawaida, au Tsheti(tshirt) na suruali ya kitambaa au jeans, vyovyote vile atakavyoona yeye inafaa.

§  Kwahiyo mfanyabiashara wa mitindo ya nguo za kiume unapaswa ujue kabisa mwanaume anaposema labda anataka mavazi kwa ajili ya kuendea kazini basi umpe mavazi yapi. Hata ikiwezekana wewe ndiye umpe ushauri ni mavazi ya aina gani au ni mtindo wa mavazi upi anaopaswa kuvaa utakaoendana na kile anachotaka kwenda kukifanya. Kwa mfano kuna mishono ya nguo za harusi kwa wanaume ambapo mara nyingi huwa ni suti lakini kuna staili na madoido ambayo kama mtu wa mitindo na mavazi ya wanaume unapaswa kuyajua.

§  Wanaume mara nyingi hupendelea mitindo na staili za nguo zinazoendana na wakati hasahasa vijana, utakuta wakitaka kuvaa kama mastaa mbalimbali wa muziki na filamu. Utawasikia wakisema, “nataka nionekane kama Ommy Dimpoz, au nataka nitokelezee kama Diamond Platnumz, Ali Kiba, Mr. Blue, AY” nk. Mitindo yao ya mavazi na hata namna wanavyoziweka nywele zao huathiri kwa kiasi kikubwa namna wanaume na hasa vijana wanavyonunua mavazi yao.

    SOMA: Hatua 10 za kufuata unapotaka kuanzisha duka lako

§  Kama wewe siyo mjuzi wa mambo ya mitindo ya mavazi ya wanaume na una biashara ya kuuza fasheni za wanaume basi ni bora hata ukamuajiri mtu maalumu mwenye taaluma hiyo akakuvutia wateja wa kutosha ukamlipa kwa mwezi. Jijini Dar es salaam kuna wafanyabiashara wa mitindo ya nguo za wanaume wengi walioamua hata kuajiri wanamitindi kutoka nchi jirani kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa ajili ya kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na wateja wanajaa madukani mwao.

Kwa mahitaji ya vitabu vyako vya biashara na ujasiriamali katika lugha ya kiswahili usikose kutembelea ukurasa huu wa SMART BOOKS TANZANIA. Na kama pia ulikuwa hujapata kile kitabu chenye Kanuni ya kujifunza Elimu ya Pesa na Mafanikio, wahi sasa kukipata bure kwa kubonyeza maandishi yafuatayo; JIUNGE NA BLOGU YAJIFUNZEUJASIRIAMALI KUPATA VITABU VIZURI BILA MALIPO. hii ni ofa ya muda mfupi tu, baada ya muda tutaanza kukiuza.

Mkazi yeyote wa Dar es salaam anayehitaji vitabu kutoka kwetu kwa sasa tunamletea mpaka pale alipo bila malipo ya ziada isipokuwa tu kitabu cha “MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA”, ambacho kutokana na gharama za usafiri kuwa juu, tunakuomba wewe mteja unayehitaji kitabu hicho peke yake basi utuchangie nauli ya shilingi 1,000/=. Inamaana badala ya shilingi elfu 4 kitagharimu Sh. elfu 5 kukuletea mpaka  ulipo.  Ukiagiza na moja ya vitabu vikubwa gharama hiyo huwa haipo au unaponunua kwa mawakala wetu utalipa hiyohiyo elfu 4.

ASANTE,
Mwandishi na mhamasishaji wako,

Peter Augustino.

0 Response to "BIASHARA YA MITINDO YA NGUO ZA KIUME NA VIATU INAVYOWEZA KUKUTAJIRISHA"

Post a Comment