Biashara ya duka la rejareja inalipa tofauti na tetesi na
imani potofu zilizoenea mitaani kwamba biashara hii hailipi, ni ngumu,
inachosha na wala haiwezi kumtoa mtu katika umasikini na kumfanya aishi maisha
bora yenye mafanikio.
Ukimsikia mtu akikupa sababu hizo zisizokuwa na mashiko,
mwambie hebu akachunguze vizuri mtu kama Mohammed Dewji CEO wa METL Group na
tajiri kijana zaidi Afrika alianza na biashara gani au baba yake Mzee Gulam Dewji
kabla mwanaye hajafanya mapinduzi makubwa katika kampuni yake alikuwa akifanya
biashara gani?
Baada ya utangulizi huo kidogo naomba sasa nikakupe
dondoo muhimu za leo ambazo siyo nyingi ni 2 tu lakini naamini kabisa kuwa ni
moja kati ya mbinu ambazo ukizitumia vyema kamwe hautakaa useme eti biashara ya
maduka ya vyakula mitaani maarufu kama maduka ya rejareja, hayawezi kumpa mtu
mafanikio na utajiri katika maisha yake.
1. MTU SAHIHI WA KUKUUZIA DUKA LAKO(Shopkeeper)
Kama unapanga kufungua duka la rejareja, hakikisha kwanza
una uhakika ni nani atakayeuza kwenye duka hilo. Kama ni wewe mwenyewe basi
hamna shida kwani tayari kwa kuwa unao uchungu na mtaji uliowekeza pale
utahakikisha mambo hayaendi mrama, hata hivyo kuwa ni wewe utakayeuza dukani
mwenyewe isijekuwa ndiyo tikiti ya kutapanya mtaji, inakupasa uwe na nidhamu ya
pesa ya hali ya juu kabisa kwani wengine huwa wabaya hata kushinda hata vile wangeweka
mfanyakazi.
Kama utamuweka msaidizi, ambaye anaweza akawa ni
mfanyakazi uliyemwajiri, ndugu wa karibu, mke au mme nk. basi hakikisha
kunakuwa na vipimo au tuseme mnahesabiana mali kabisa na kuhakikisha kunakuwa
na mfumo thabiti wa uwekaji na ukokotoaji kumbukumbu za mahesabu ambao utatumika
kumwajibisha huyo msaidizi endapo mambo yataharibika pasipokuwa na sababu ya
msingi. Hapa hasa ndipo penye kizungumkuti katika biashara nyingi za rejareja,
ndipo mahali chuma ulete anapoibuka, ndipo unaposikia watu wakilalamika
biashara ya duka ni kichaa nk.
Kwa bahati nzuri kwenye kitabu cha “SIRI YA MAFANIKIO:
BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA” nimeelezea kwa kina sana mifumo yote mikubwa mtu
unayoweza kuitumia kwa ufanisi katika kuhakikisha kizungumkuti hiki hakikukuti
wakati ukiendesha biashara yako ya duka hata ikiwa unaendesha maduka zaidi ya 6
kwa wkati mmoja.
2. MUDA MUAFAKA WA KUFUNGUA NA KUFUNGA DUKA LAKO.
Katika listi ya vitu vinavyochangia sana kufanikiwa au
kufeli katika biashara ya duka la rejareja au dula la vyakula mtaani hii
inashika namba mbili 2 baada ya mtu wa kukuuzia. Muda ni kigezo muhimu sana
kwenye biashara ya duka. Hakikisha unafungua mapema na kufunga angalao baada ya masaa 12 kulingana na vigezo vingine kama
umbali kutoka unapoishi, usalama wa eneo nk.
Kwanini nakuambia hivyo? Biashara ya duka la rejareja
faida ya bidhaa zake ni ndogondogo, na hivyo ili kuona faida kubwa inakupasa
uuze vitu vidogovidogo vingi ambavyo faida nayo itajikusanya na kuwa kubwa.
Sasa ili kuuza vitu vingi inabidi pia duka liwe wazi muda mwingi wa kutosha.
Kwa mfano kuna watu maduka yao hufunguliwa saa 12 asubuhi na kufungwa saa 5
usiku. Mtu kama huyo huwezi kumlinganisha na yule anayefungua saa 3 asubuhi na
kufunga saa 12 jioni, huyo wa kwanza atapata mafanikio makubwa zaidi na kwa
muda mfupi.
Nakumbuka wakati fulani enzi za akina Makamba na Kandoro,
nikiwa na kioski pale Msimbazi, kioski hakikuwa na mlango na nilikiendesha
hivyohivyo bila mlango kwa takribani zaidi ya mwaka mmoja. Tulikuwa tukiita ‘kukomaa’
maana yake ni kwamba mtu unaanza asubuhi mpaka kesho yake tena asubuhi, lakini
ilikuwa huwezi kufanya vile peke yako kwa muda mrefu ni lazima uwe na msaidizi
ambaye mnapokezana. Nakumbuka nilikuja kuona umuhimu wa kuweka mlango kwenye
kile kioski kipindi cha maandamano ya kesi ya Hamisi Rajab Dibagula iliyohusu
mivutano ya kidini baada ya askari waliokuwa wakivurumisha mabomu ya machozi
kunilazimisha nifunge kioski na mimi nikawa nababaika nifunge kwa kutumia nini.
Ukweli ni kwamba faida niliyokuwa nikiipata pale sidhani kama
hata baadhi ya wenye maduka makubwa waliokuwa wakifunga saa 12 kama walikuwa
wanaipata. Sishauri watu ‘kukomaa’ dizaini niliyokuwa nikifanya mimi kipindi
hicho cha Yusuph Makamba hapana, kwanza ni kinyume cha sheria siku hizi
ukikutwa unaweza ukafungiwa leseni yako au ukatupwa mahakama ya city, ila
nataka tu kusisitiza umuhimu wa kufungua maduka muda wa kutosha.
…………………………………………………………………..
Usikose kuwa na mimi kila wakati hapa, nitaendelea
kukuletea dondoo mbalimbali kwa kadri muda unavyokwenda kuhusiana na vile
unavyoweza kutoka kupitia biashara ya duka. Lakini pia ikiwa utapenda kufahamu
kwa kina ni kwa namna gani unavyoweza kuifanya biashara yako ya duka kwa
mafanikio makubwa zaidi, basi jipatie kitabu nilichokuandalia cha SIRI YAMAFANIKIO: BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA kwa bei ya shilingi elfu 10 tu.
Ukiwa
Dar es salaam utaletewa mpaka pale ulipo na Ukiwa Mkoani tunakutumia kwa basi au mwagize mtu
anayekuja Dar akuchukulie. Pia unaweza ukakinunua kama softcopy PDF kupitia
email yako kwa bei ya shilingi 5,000/= namba za simu ni 0712 202244 au 0765 553030 Jina ni Peter Augustino. Tarimo
Kuna semina pia inayohusu uandaaji wa mpango wa biashara
yako na inafanyika kwa njia ya email sambamba na kwenye blogu maalumu ya
uanachama, kwa maelezo zaidi ya semina hiyo fungua, SEMINA YA MICHANGANUO YABIASHARA NDANI YA TANZANIA ONLINE SCHOOL OF BUSINESS PLANNING.
Deo
ReplyDelete