Huu ni uamuzi muhimu sana na pengine mgumu zaidi
unaopaswa kuchukua mwaka huu mpya wa 2017 ili uweze kuendelea kuona mafanikio
makubwa yakitokea katika biashara yako. Iwe ndiyo unaanzisha biashara au tayari
unamiliki biashara yeyote ile unatakiwa uwe na vipaumbele vyako ambavyo piga
ua, ni lazima uhakikishe unavifanyia kazi kikamilifu na kuvikamilisha katika
muda muafaka uliojiwekea.
Biashara au kampuni yako haiwezi kufanya kila kitu kwa
kila mtu, vivyo hivyo na hata kwako wewe mwenyewe, haiwezekani kumridhisha kila
mtu hapa duniani. Kujaribu kufanya kila kitu kwa kila mtu, iwe ni mtu au
biashara, hiyo ni tikiti ya kuanguka vibaya kibiashara. Badala yake unatakiwa
kufanya au kushughulika na baadhi tu ya vitu, wateja kwa mfano kwa ajili ya
ufanisi bora kabisa.
Kuna vitu vingi ambavyo unaweza ukachagua na kuacha
vingine. Kwa mfano katika muktadha wa biashara, vitu kama, aina ya biashara, wateja(soko),
aina ya bidhaa, vyombo vya habari unavyotumia kutangaza biashara yako, bei, eneo
la kuuzia bidhaa/huduma zako nk.
Hauwezi mathalani kuanza kufanya aina mbili au tatu za
biashara ghafla kwa wakati mmoja na ukategemea kuona mafanikio mazuri. Kama labda unauza
matunda aina ya ndizi na mananasi, komaa kwanza na ndizi na mananasi kwa muda
mrefu wa kutosha uone matokeo yake kwanza kabla ya kuhamia kwenye biashara tuseme, ya
mahindi au viazi, basi tu kwa vile umeona wenzako wanaofanya biashara kama hizo
wanapata faida kubwa.
Ndivyo hivyo hivyo ilivyo kwa wateja au soko la biashara
yako, kama umeshaamua kuwa wateja wa nguo zako au bidhaa yeyote unayouza ni
kundi fulani la wateja kwa mfano umechagua ‘kudili’ na watoto peke yao, basi ni
jambo lenye tija zaidi endapo utaamua kufanya jitihada zote kuhakikisha wewe
mteja yeyote mwenye shida na nguo ya mtoto anapata suluhisho kutoka kwako.
Siyo vibaya kufanya vitu tofauti tofauti, nikimaanisha “kutokuweka
mayai yako yote kwenye kapu moja” kama kwenye Kitabu cha MIFEREJI 7 YAPESA” kinavyohimiza, lakini dhana hiyo ifanyie kazi kwa tahadhari. Hamia kwenye
kitu tofauti au ongeza kipaumbele cha pili baada ya kuhakikisha kwamba kile cha
kwanza umeshakifikisha mahali pazuri na mafanikio angalau umeyaona ndipo
utakuwa na nguvu na ari ya kufanya kitu/jambo jingine bila ya kukata tamaa
upesi.
Aina ya bidhaa/huduma unazouza kwa wateja, katika
biashara moja tuchukulie mfano wewe unatengeneza juisi asili ya matunda na
kuwauzia wateja kwenye kioski chako kilichopo stendi, Juisi za matunda kwa kuwa
zipo za aina nyingi kama juisi ya passion, juisi ya embe, juisi ya ukwaju,
juisi ya nanasi, juisi ya ubuyo na nyinginezo nyingi, wakati unaanza kabla
hujalifahamu vizuri soko lako ni vizuri kwanza ukaanza na aina ya juisi unayoona
inapendwa zaidi na wateja na pia ni rahisi zaidi wewe kuitengeneza kisha
ukaanza nayo na aina hizo nyingine utakuja kuziweka taratibu kadiri uzoefu
unavyozidi kuongezekana soko lako kukua.
Hali ni hiyo hiyo kwa vitu vingine kama njia za kutangaza
biashara yako, eneo nk. Angalia ni njia ipi ukitumia kutangaza biashara yako
itakuwa muafaka zaidi ya zingine, tazama unafuu wa gharama, kufikiwa wateja kwa
urahisi zaidi, idadi ya wateja watakaofikiwa nk. Itumie njia hiyo ama chombo
hicho cha matangazo hadi pale utakapoona mafanikio kabla ya kuamua kuongeza
njia ya pili. Hii itakusaidia kwanza kupima matokeo ya kampeni yako ya
matangazo na pia kutokuingia gharama kubwa sana mwanzoni kabla ya kuona
mafanikio.
Pia kwenye eneo la biashara, huwezi mara leo umeweka
biashara yako kariakoo, kesho kimara na keshokutwa Mbagala labda iwe ni
biashara ya kutembeza bidhaa. Biashara kama za utoaji wa huduma unashauriwa
kuwa na sehemu maalumu wateja watakayojua unapatikana bila wasiwasi wowote,
vinginevyo basi iwe unafungua matawi katika maeneo mengine.
Ndugu msomaji wa blogu hii, mambo haya yanaweza kuonekana
ni madogomadogo lakini yana athari kubwa sana katika maisha yetu ya biashara na
ujasiriamali. Mafanikio katika biashara hayahitaji mpaka ufanye vitu vikubwa
sana, unaanza na mambo madogomadogo kwanza kama haya kwa ukamilifu na makubwa yatakuja
yenyewe.
Ili kuhakikisha malengo yako unayojiwekea mwaka huu unayatimiza kweli na huishii tu kutamani kuyatimiza, hakikisha unayaandika mahali, kuna malengo ya muda mfupi na yale ya muda mrefu, yale ya muda mrefu ndiyo yanayopaswa kuandikwa zaidi kwa sababu ndiyo mepesi zaidi kusahau njiani. Jitoe kikwelikweli na siyo lelemama, weka katika vitendo yale uliyoazimia vinginevyo matazamio yako yataishia kuwa ndoto na wewe kuishia kulalamika mwishoni mwa mwaka kwa kusema, "oo, kuweka malengo hakusaidii chochote, ni bora kuishi bila kuweka malengo".
Sasa utaishi vipi bila malengo?, haiwezekani kabisa, labda unaweza kuniambia utaishi kwa mtindo wa kuweka malengo ya muda mfupi mfupi, mtindo ambao watu badala ya kujiwekea malengo na mipango ya muda mrefu, wao huweka malengo na mipango ya muda mfupi mfupi na hujitahidi kuyatimiza kwa wakati, lakini siyo kuishi bila ya malengo kabisa.
Nichukue nafasi hii rasmi kukutakia wewe jamaa na marafiki
zako wote, HERI NA FANAKA KATIKA MWAKA WOTE HUU WA 2017, mwaka ambao ninaamini
tutakuwa wote pamoja na kila kitu kitakwenda kubadilika tofauti na miaka
mingine yote iliyopita.
Kama ndiyo upo katika kilele cha ukuu wako, basi ni
wakati wa kuhakikisha huupotezi, endelea kuushikilia hivyo hivyo na ikiwa basi
kwa bahati mbaya uliupoteza ukuu wako miaka iliyopita, mwaka huu ndio mwaka wa
kwenda kuurudisha tena ukuu wako huo uliokuponyoka,
#MAKEYOURSELFGREATAGAIN
#Jirudishietenaukuuwako
0 Response to "UAMUZI MGUMU NA MUHIMU KUCHUKUA ILI BIASHARA YAKO IZIDI KUKUPA FAIDA MWAKA 2017"
Post a Comment