LUGHA YA MAMA KISWAHILI INA UWEZO WA KULETA MAENDELEO MAKUBWA KIUCHUMI TANZANIA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

LUGHA YA MAMA KISWAHILI INA UWEZO WA KULETA MAENDELEO MAKUBWA KIUCHUMI TANZANIA

Ikiwa leo ni siku ya lugha ya mama duniani, hapa kwetu nchini Tanzania tunajivunia sana kuwa na lugha yetu ya Kiswahili ambayo imekuwa lugha ya Taifa na chombo cha mawasiliano baina ya jamii nyingi Afrika ya Mashariki na hata nje ya Afrika Mashariki, Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla, ingawa pia zipo lugha nyinginezo za makabila mbalimbali zipatazo 127

Maendeleo ya jamii yeyote ile duniani yanategemea sana lugha ya jamii husika, kwa hiyo jamii kuwa na lugha yake na ambayo wanajamii hiyo huanza kuitumia tangu wanapozaliwa na mama zao ni jambo muhimu na la kujivunia sana. Ukiacha lugha nyingine za mama kutoka makabila mbalimbali, kiswahili ndicho kinachochukua nafasi kubwa Tanzania kiasi kinachosababisha hata baadhi ya lugha hizo nyingine kuwa katika hatari ya kutoweka kutokana na sababu kwamba watoto hasa wale wanaozaliwa mijini siku hizi lugha yao ya kwanza badala ya kuwa ni ile ya makabila ya wazazi wao huwa ni kiswahili. Hapo utaona kuwa baada ya miaka kadhaa lugha ya mama kwa watu wengi itakuja kuwa ni Kiswahili.

SOMA: Ni kitabu gani hautakisahau kamwe maishani?

Nchi tajiri nyingi duniani ukichunguza karibia zote wananchi wake hutumia lugha ya mama kwenye nyanja zote muhimu za kiuchumi na maendeleo. Shughuli mbalimbali kuanzia, elimu mashuleni, vyuo na hata vyuo vikuu, kupashana habari kupitia vyombo vyote vikubwa vya habari, habari za kitaifa na kimataifa(hawajali kama kuna wageni au watu wa nje watakaohitaji kusikiliza), shughuli zote za kisiasa na kidiplomasia-wako tayari hata kutumia wakalimani kuliko kutumia lugha isiyokuwa ya mama. 

Kupanga mipango ya maendeleo yao, hutumika katika fasihi na tunaweza kushuhudia umuhimu wa fasihi katika jamii ya watu wa china, ujerumani na hata Korea ulivyokuwa mkubwa katika sinema na video zao tunazoziangalia kila siku hapa kwetu. Kwa ujumla nchi kubwa duniani lugha ya mama imechangia kwa kiasi kikubwa sana kuzifikisha pale zilipokuwa leo hii. Baadhi ya mifano ya nchi hizo tajiri ni kama vile, Marekani, China, Ujerumani, Japan, Korea ya Kusini, Uingereza na Ufaransa.

Wanawake nao wana dhima kubwa sana katika kuhakikisha lugha ya mama inadumishwa kwani ndiye mtu wa kwanza kabisa anayemfundisha mtoto lugha pindi baada ya kuzaliwa na miaka yake ya awali ya utoto, hivyo maendeleo ya wanawake nayo yana athari kubwa katika kudumisha lugha ya mama na ndiyo maana hata kukawa na hilo jina “lugha ya mama au mother tongue” kumaanisha ile lugha ya kwanza kabisa binadamu anayoanza kujifunza akiwa mtoto mchanga.

Hapa mwanamke anastahili kupewa uzito wa juu na hasa kuhakikisha katika nchi zetu hizi zinazoendelea mwanamke anathaminiwa na kupewa haki zote za kibinadamu kinyume na kama huko tulikotoka ambapo mwanamke wa Kiafrika alikuwa anachukuliwa kama daraja la pili la mwanadamu  baada ya mwanaume.

SOMA: Kina mama hubeba watoto wao miezi 9 lakini mioyoni mwao huwabeba milele.

Soko la ajira kwa mfano hapa kwetu Afrika Mashariki linaonekana kuwapendelea zaidi Wakenya na watu wa mataifa yale yanayozungumza kiingereza kwa sababu tu ya lugha ya Kiingereza inayotukuzwa na kuonekana kana kwamba ndiyo lugha iliyokuwa na uwezo wa kubeba maarifa yote makubwa Duniani. Lakini ushahidi mbalimbali zikiwemo hizo nchi tajiri nilizozitaja unaonyesha kwamba lugha na maarifa ni vitu viwili tofauti kabisa. Kinachotufanya Watanzania tusijiamini ni kutokuifahamu sawasawa lugha ya kiingereza na wala siyo eti tunakosa maarifa. Kama udahili utafanywa kwa kiswahili maeneo mengi tutakuwa vinara.

Mchina au Mjapani ataunda gari au ndege hata ikiwa hajui kiingereza cha kuombea maji na hivyo ndivyo walivyofanya, wamepata mafanikio makubwa sana kiuchumi wakitumia lugha zao zilezile za mama hata kama wengine walijifunza lugha za pili lakini siyo kwa lengo la kupata maarifa au ufundi wa aina fulani bali labda kwa ajili tu ya kuwa wakalimani nk. Mfano mwingine ni Vitabu mbalimbali vitakatifu kama vile Biblia Takatifu, Quran Tukufu na Misahafu ya dini nyingine mbalimbali kubwa Duniani. Utaona kwa mfano miaka hata kabla ya Uhuru mara tu baada ya wakoloni kuingia Barani Afrika, Wamisionari na waeneza dini mbalimbali walitafsiri misahafu hiyo katika lugha za mama za wazawa wa Afika kwa mafanikio makubwa kiasi cha kushangaza.

SOMA: Vitabu chanzo cha mafanikio makubwa Ulimwenguni.

Kuna wakati fulani nikiwa na Mzee mmoja kutoka Uru Moshi alinisimulia pamoja na kunionyesha biblia Takatifu iliyokuwa imeandikwa katika lugha ya Kichagga cha Uru, kweli nilishangazwa sana. Akanieleza kwamba miaka ya njuma Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestant kama Walutheri yaliyoenea zaidi maeneo ya Moshi vijijini, wao tofauti na wenzao Wakatoliki walioenea zaidi maeneo ya Rombo na Machame walikuwa na mtindo wa kutafsiri vitabu vyao ikiwemo biblia na vitabu vya nyimbo za Injili kwa lugha za mama za mahali husika. Vivyo hivyo na kwa Wamasai nako nimewahi kusikia kwamba na wao dini zilipofika huko ilibidi vitabu vitafsiriwe kwa lugha yao.

Kwa mantiki hiyo unaweza ukaona ya kwamba kila lugha iliyopo hapa duniani hata iwe ni ya kabila dogo kiasi gani inao uwezo kamili wa kujitegemea na kufanya kazi zote zinazoweza kufanywa na lugha zingine zikiwemo zile kubwa kubwa kama kiingereza na Kijerumani. Hata ikiwa kunakuwa na baadhi ya maneno itakayokopa hakuna shida kwani hata hizo lugha kongwe nazo kuna baadhi ya maneno zinayokopa kutoka lugha nyingine.

Tukirudi hapa kwetu Tanzania, Kiswahili kimefanya mambo mengi mno, hebu tuchukulie kitu kama muziki wa Bongo fleva na nyimbo nyingine kama vile taarabu na kwaya mbalimbali, bongo movie na sanaa nyinginezo mbalimbali ni vitu vilivyojipatia umaarufu mkubwa nje na ndani ya nchi kutokana na kuimbwa au kuigizwa katika lugha ya kiswahili ambacho kinaeleweka na idadi kubwa ya wakaazi wa eneo la Afrika ya Mashariki na ya Kati. 

Kiswahili kama lugha ya mama kingefaa kutiliwa mkazo zaidi hasa kwenye elimu na ndiyo tungeliweza kuona maendeleo ya haraka ya nchi kwani kila mwanafunzi kuanzia chekechea hadi chuo kikuu angeelewa kwa urahisi zaidi maarifa yeyote yale ambayo angejifunza.

SOMA: Kuandika mchanganuo wa biashara yako kwa kiswahili kuna faida kubwa.

Wapinzani wengi wa kiswahili hudai eti kiswahili msamiati wake ni duni hivyo haiwezekani kutafsiri maarifa mengi hasa yale ya sayansi lakini dai hilo halina mashiko yeyote unapoyatazama mataifa kama Korea ya kusini, China na Ujerumani. Si hivyo tu kuna ushahidi mwingi kwa mfano kuna hata watu wengi waliokwisha wahi kutafsiri vitabu mbali mbali vikubwa duniani kama vile, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyewahi kutafsiri katika kiswahili kitabu cha mwandishi mashuhuri zaidi Duniani, Shake Spear cha Matajiri wa Venisi(The Merchant of Venace) Mfano mwingine tunao hapa hapa kwenye blogu hii wa tafsiri ya kitabu maarufu zaidi duniani cha elimu ya Pesa na Mafanikio kilichoandikwa na Napoleo Hill, Think & Grow Rich (Fikiri Utajirike) au “Msahafu wa mafanikio”

Kwa maoni yangu binafsi kutokana na mifano yote hiyo, sioni mahali popote pale kiswahii kinapoweza kushindwa zaidi ya ‘fitina’ tu za watu wachache wanaopenda kuutukuza ukoloni kwa kuona kiingereza ndiyo kila kitu linapokuja suala la ustaarabu. “Lugha ya mama ni tamu, unaongea kwa uhuru ukijiamini, huogopi utakosea mahali na wala hutumii nguvu nyingi kujifunza kama lugha nyingine za kuazima.”-Peter A.  

Katika maadhimisho ya siku ya lugha ya mama Duniani leo tarehe 21 feb., Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO umetoa taarifa inayosema kwamba duniani kote kuna lugha za mama kiasi cha lugha elfu sita(6,000) ambazo miongoni mwa hizo karibu nusu yake yaani asilimia 50 zinakabiliwa na hatari kubwa ya kutoweka kabisa. Kauli mbiu ya siku hiyo mwaka huu ni, elimu jumuishi kupitia lugha; Lugha ina umuhimu!”

Kwa mujibu wa mtandao wa Language of the World, Tanzania inazo lugha za mama zipatazo 127, ambazo 125 zipo hai huku 2 zikiwa zimesha kufa na katika hizo nane 8 zipo kwenye hatari ya kufa. Kiswahili na Kiingereza ni miongoni wa lugha hizo 127. Lugha moja iliyotoweka ilijulikana kama lugha ya Waware na waliishi maeneo ya Mashariki mwa ziwa Victoria, haijulikani kama kabila hilo siku hizi wanaongea lugha ipi lakini inasadikiwa wanazungumza lugha za Kibantu za makabila mengine ya jirani.

………………………………………………………………………

Ndugu msomaji wangu endelea kufurahia punguzo la bei ya vitabu hasa softcopy na semina kutoka Self  Help Books. Unaweza ukajipatia vitabu vyote toka kwetu pamoja na semina kwa gharama ya shilingi elfu 15 pekee, kwa maelezo zaidi ya ofa hiI bonyeza maneno yafuatayo na usome, FURAHIA OFA YA SHILINGI 90,000/= KWA VITABU VYAKO VYA PESA & MAFANIKIO NASEMINA YA MICHANGANUO.


0 Response to "LUGHA YA MAMA KISWAHILI INA UWEZO WA KULETA MAENDELEO MAKUBWA KIUCHUMI TANZANIA"

Post a Comment