Mwenyekti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi (kulia), akizindua kitabu cha mashairi kwa lugha ya Kiingereza chenye kichwa cha habari `Ndege anayeimba jina langu`.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amewataka wananchi kuwa
wavumilivu katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kushuka kwa kiwango cha elimu
nchini, kutokana na kazi hiyo kuwa ngumu.
Dk. Mengi, alisema hayo jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, wakati
akizindua kitabu cha mashairi kiitwacho 'Ndege anayeimba jina langu, Shairi la
Moyo wangu' kilichotungwa na Mtanzania Edna Hogan.
Katika uzinduzi huo, Dk. Mengi, amenunua vitabu vyenye thamani ya Sh.
Milioni 51 kwa ajili ya shule 30 katika mikoa mbalimbali nchini.
Alisema kazi ya kufanya marekebisho msingi wa elimu wa nchi, unahitaji muda kwa
ajili ya uboreshaji wa miundombinu na maslahi ya walimu kuanzia shule za awali,
msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Dk. Mengi alisema kwamba matokeo ya kazi hiyo yanaweza kuonekana kati miaka 21
hadi 25 kulingana na kasi ya utekelezaji wake.
"Kitu muhimu lazima tukubali kuchukua muda katika kuboresha elimu
yetu ambayo imepoteza muelekeo, huwezi kukurupuka tu kuanza kuboresha shule za
sekondari wakati shule za msingi zipo taabani, kwani wakifanya hivyo
watazalisha wanafunzi wachovu watakaokwenda kwenye shule na vyuo," alisema
Dk. Mengi.
Aliitaka serikali kuacha kuwapa ajira walimu wasio na sifa na walio kwenye
ajira wafanye utambuzi maalum ili kutambua uwezo wao wa ufundishaji.
\"Nchi ya Finland imefanikiwa kwa kuijenga sekta ya elimu, kiasi
ambacho kwa sasa walimu ndiyo kada pekee inayolipwa mshahara mkubwa,"
aliongeza.
Alimpongeza mtunzi wa kitabu hicho pamoja na Taasisi ya Camara kwa kuchukua
hatua ya kuzindua kitabu hicho na kuendesha uchangiaji wa upatikanaji wa
kompyuta mpakato kwa baadhi ya shule nchini.
Awali, Hogan alisema kitabu hicho cha mashairi kimelenga kutoa ufahamu na
kufundisha watu mbalimbali, hasa wanafunzi katika kukabiliana na masuala
mbalimbali ya maisha.
Alisema kitabu hicho chenye kurasa 130 kilichoandikwa kwa lugha ya Kiingereza
kimehakikiwa na kupitiwa na wasomi na wanataaluma maarufu nchini na kizuri
kutumika katika shule za sekondari.
|
0 Response to "Dk. Mengi ataka muda kuboresha elimu"
Post a Comment