Duka moja wapo la Home Shopping Centre lililopo jijini Dar es Salaam |
Dar es Salaam. Mtu asiyejulikana juzi usiku alimvamia mmiliki wa
maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad (pichani) na kumwagia maji
usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.
Tukio hilo lililotokea juzi saa 1 usiku karibu na kituo cha
Polisi cha Oysterbay, lilithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Ally Mlege kwa kusema kuwa bado polisi wanaendelea na
uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika.
“Ni kweli tukio hili limetokea ila polisi wanaendelea na
uchunguzi. Tukikamilisha uchunguzi tunatarajia kutoa taarifa kamili za tukio
zima,” alisema na kuongeza;
“Hatuna haja ya kuficha ukweli wa tukio hili, uchunguzi wetu
ukikamilika na watuhumiwa wakikamatwa kila mtu atajua.”
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilizolifikia
gazeti hili zilieleza kuwa mtu huyo, alimkuta Saad akiwa anazungumza na mmoja
wa wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo karibu na Kituo cha Polisi
cha Oysterbay.
“Wakati akizungumza na mfanyakazi wake, huyo mtu alikuwa kama
anapita na alichomoa kitu fulani na kummwagia Saad usoni na kisha kukimbia,”
zilieleza taarifa hizo na kuongeza;
“Baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya AMI, sasa
hatujui kama bado yupo hapo au ameondoka, ila sisi tulizungumza naye na
alitueleza mwonekano wa mtu aliyemwagia tindikali.”
Taarifa hizo zilifafanua kwamba polisi wanazitumia taarifa hizo
walizopewa na Saad, ili kuweza kumkamata mhusika.
Taarifa hizo zilifafanua kuwa polisi wanapanga tena siku ya
kumhoji kwa mara ya pili Saad, kwamba watataka kufahamu kama mfanyabiashara
huyo alikuwa akipewa vitisho au ujumbe wowote, kabla ya kukutwa na tukio hilo.
Hata hivyo, habari nyingine zilizolifikia Mwananchi Jumapili
zilieleza kuwa mtu huyo baada ya kummwagia Saad tindikali, alipanda pikipiki na
kutokomea eneo hilo.
“Walikuwa wawili, mmoja alikwenda kufanya unyama na mwingine
alibakia katika pikipiki, baada tu ya kumwagia tindikali mtu yule alikimbia
mpaka pale alipokuwa imesimama pikipiki, alipanda na kuondoka kwa kasi,”
zilieleza habari hizo.
Taarifa zilizopatikana jana asubuhi zilieleza kuwa ndugu na
marafiki wa mfanyabiashara huyo, walikuwa katika mipango ya kumpeleka nje ya
nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
Chanzo: MWANACHI
0 Response to "MMILIKI HOME SHOPPING CENTRE AMWAGIWA TINDIKALI"
Post a Comment