Johannesburg: “Happy birthday
Mzee Madiba.” Rais wa kwanza na mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo
anatimiza umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika
Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.
Maadhimisho ya miaka 95 tangu
kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine
yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika
wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika
hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake
imeelezwa kuwa ni mbaya.
Leo, Rais Jacob Zuma
atawaongoza mamilioni ya wananchi wa Afrika Kusini katika maadhimisho ya nne ya
kimataifa ya ‘Siku ya Mandela’ ambayo yanakwenda sambamba na siku yake hiyo ya
kuzaliwa.
Tangu kulazwa kwa Mandela huko
Pretoria, Rais Zuma amekuwa akiwahimiza wananchi wake wajiandae kusherehekea
miaka 95 ya Mandela akiwatia moyo wale waliokuwa na wasiwasi kwamba Madiba
asingeweza kuifikia leo kutokana na matatizo ya kiafya.
Siku ya Mandela huadhimishwa
kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa
wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye
kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.
Pia ‘Mandela Day’ hutumika
kukumbuka kampeni yake dhidi ya ubaguzi wa rangi na utetezi wa haki za binadamu
maarufu kwa jina la “46664”, ambayo ni namba ya utambulisho aliyoitumia
alipokuwa mfungwa katika Gereza la Visiwa vya Robben.
Dakika 67 za Mandela
Kwa maana ya Siku ya Mandela
ambayo pia imeidhinishwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, wananchi wa Afrika
Kusini wanatumia dakika 67 kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni
hatua ya kuenzi kile wanachokiita ‘kazi za mtu aliyejitoa maisha yake kwa ajili
ya kupigania haki na utu’.
Dakika hizo 67 zinawakilisha
idadi kama hiyo ya miaka ambayo Mandela alitumika, hivyo Waafrika Kusini
watakuwa wakitoa msaada na huduma kwa jamii iwe ni kwa watoto yatima au watu
wengine ambao ni wahitaji katika jamii.
Kituo cha Kumbukumbu ya Mandela
kimewataka wananchi kuungana na kuonyesha ushirikiano wao kwa Mandela kwa
kutumia dakika 67 za muda wao kuzisaidia jamii zao ili kumuenzi kiongozi huyo
ambaye ni alama ya dunia.
0 Response to "Sherehe ya Mandela hospitalini Medclinic."
Post a Comment