SIRI NAMBA 3 YA MATAJIR NA WATU WALIOFANIKIWA KIMAISHA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIRI NAMBA 3 YA MATAJIR NA WATU WALIOFANIKIWA KIMAISHA


Katika kampeni yetu ya "TOKOMEZA UMASIKINI" tuliahidi  kwamba katika kila ‘media’ nikiwa na maana kitabu, mtandao wa kijamii, jarida, CD, Makala au katika chombo kingine chochote kile cha habari, tutakuwa ‘tukianika’ (tukitoa) siri moja moja au mbili za matajiri na watu waliofanikiwa kimaisha.

Naomba tueleweke , tunaposema Matajiri na watu waliofanikiwa hatuna nia mbaya ya kutaka ‘kuwachora picha ya utuhumiwa’ kundi hilo la watu katika jamii, wala siyo kwamba labda tunawaonea kijicho kwa maendeleo waliyoyafikia.

Dhana hii ya  Matajiri na watu waliofanikiwa kimaisha katika kampeni hii, iliyoanzishwa na kampuni yenu ya SELF HELP BOOKS PUBLISHERS inawakilisha mtu, kikundi au hata asasi yeyote ile, wachoyo wa mawazo, wasiopenda kuwashirikisha japo kimawazo na ushauri, jirani, ndugu, marafiki au hata binadamu wenzao wasiobahatika ili hatimaye na wao waweze kuwa na maisha bora kiuchumi na kijamii kama wao au tu hata kuwatakia  heri. Kinyume chake watu wengi siku hizi, siyo matajiri tu bali hata na watu wa kawaida imekuwa ni jambo la kawaida kuoneana vijicho, wivu, kutakiana majanga na hata vifo.

Kuna matajiri na watu waliofanikiwa kimaisha  wengi tu hapa Tanzania ambao wamekuwa kioo, wanawatia watu moyo na hata kudiriki kutoboa siri zao nyingi mbalimbali kwa watanzania wenzao kusudi na wao waweze kufanikiwa. Orodha ni ndefu lakini kwa harakaharaka tu ipo mifano mizuri kama akina Mzee wetu Said Salim Bakhresa, Dr. Reginald Mengi, Mheshimiwa Mohamed Dewji (MO), Eric James Shigongo na wengineo wengi. Michango na juhudi zao katika kuwafanya watu wengine waweze kuondokana na umasikini haihitaji mtu uvae miwani ili uweze kuiona.

Dira yetu ni kuona Dunia na hasahasa Tanzania inageuka mahali bora zaidi pa kuishi kwa wanawake na wanaume.Waswahili husema, “usiombe samaki, omba utaalamu wa kuvua samaki”. Tufike mahali Watanzania tuanze kushirikishana namna ya kuweza kujikwamua kama wenzetu Wazungu na Waasia, na siyo kila mtu ajione yeye  kabarikiwa zaidi na Mwenyezi mungu kuliko mwenzake.

Nisiendelee sana kuelezea mambo mengi nikasahau na lile la msingi nililotaka kuliweka hapa, hebu tuje moja kwa moja kwenye siri yenyewe ndani ya blogu hii:
SIRI YA KUTANGAZA BIASHARA ZAO
Matangazo ni siri kubwa ya mafanikio! Hebu fanya utafiti mwepesi kwa mtu, watu, kikundi, kampuni, au taasisi yeyote ile yenye mafanikio, utabaini pamoja na mambo mengine lakini kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya upashanaji habari iwe ni kwa kupitia mdomo kwa mdomo, vipeperushi au hata TV ndiko kulikochangia zaidi mafanikio hayo.

Nguvu ya kujitangaza ni kubwa! Hata Dini mbalimbali na madhehebu pamoja na kwamba wanafanya kazi ya Mungu lakini pasipokuwa na promosheni ya aina fulani, hakuna mfuasi atakayejisumbua kujiunga humo. Vyama vya kisiasa, Waganga wa kienyeji pamoja na wengine kuwa na “uwezo wa kubadilisha elfu kumi kuwa million mia mbili” lakini  utawakuta katika magazeti wakijitangaza.

Ikiwa Tanzania kama nchi ilipeleka matangazo yake ya utalii CNN na kwingineko katika vyombo mbalimbali vya kimagharibi, sembuse mimi na wewe na biashara zetu ndogo ndogo? Unasubiri nini……..tengeneza hata vipeperushi viwili vitatu uwagawie watu stendi wajue unafanya kitu gani na upo wapi. Unaweza pia ukajifunza zaidi mbinu za kutangaza biashara yako kupitia masomo, semina na vitabu mbalimbali popote pale nchini kwa wataalamu wa biashara na ujasiriamali.

Mfululizo wa Siri nyinginezo katika kampeni hii ni ile ya kwanza inayopatikana ndani ya kitabu chenye kurasa 410, 'JIFUNZEU MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI' (Njia sahihi ya kuondokana na umasikini). Siri ya pili ipo ndani ya kitabu cha MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA. Siri ya nne ipo ndani ya Mtandao, (website) dada na blogu hii, (jifunzeujasiriamali.com). Siri ya tatu ndiyo hiyo tuliyoiona hapo juu ndani ya blogu hii. Na orodha bado itaendelea ndani ya ‘project’ nyinginezo zilizoko jikoni hivyo tafadhali usikose kuendelea kuwa na sisi, Asanteni kwa kusoma.

2 Responses to "SIRI NAMBA 3 YA MATAJIR NA WATU WALIOFANIKIWA KIMAISHA"