Moja kati ya madhumuni mawili makubwa ya tamasha hilo ni kukumbushana umuhimu wa uzalendo wa dhati wa kudumisha amani, kurejesha matumaini kwa Watanzania waliopoteza matumaini, kuipenda na kujivunia Tanzania. Tunaamini kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kuhutubia Watanzania, ameweza kutimiza malengo hayo kwa kiasi kikubwa.
Tunapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mhe. Rais kwa kukubali kuacha shughuli zingine na kujumuika nasi katika tamasha hilo na pia kukubali kuzungumza na wananchi na hatimaye kuandika historia mpya ya kuwa rais wa kwanza kuingia uwanjani kuanzisha mechi ya mpira wa miguu, kati ya Yanga na Simba za wabunge kwa kupuliza filimbi!
Tamasha la Matumaini limethibitisha kuwa pamoja na tofauti tulizonazo za kidini na kiitikadi, lakini sisi bado ni Watanzania ambao tunaweza kuishi pamoja na kushirikiana katika shughuli zetu za kijamii kwa amani na upendo kama ilivyojionesha katika timu za waheshimiwa wabunge, ambapo waliunda timu bila kujali tofauti zao za kisiasa.
Watanzania tunaamini tulikotoka ni mbali na tunakokwenda ni karibu, ile nchi ya matumaini, ile nchi ya neema tunayoiota kila siku imekaribia. Tunaamini baada ya miaka michache ijayo, kwa utajiri tulionao wa mafuta na gesi, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye mafanikio makubwa kiuchumi barani Afrika. Hivyo hatuna budi kuendelea kuilinda amani tuliyonayo na kudumisha mshikamano wetu.
Madhumuni ya pili ya tamasha hilo ni kutoa sehemu ya mapato yake na kuchangia Mfuko wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), ambao tangu mwaka jana, wamekuwa kwenye kampeni ya kuchangisha shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kujenga mabweni 30 katika shule za sekondari nchini Tanzania. Hivyo Watanzania siyo tu wanapata matumaini mapya kwa kushiriki katika tamasha, bali pia wanachangia maendeleo ya elimu nchini.
Aidha, tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Watanzania wote waliobahatika kuhudhuria tamasha la mwaka huu pamoja na wale ambao hawakubahatika kufika uwanjani lakini walifuatilia kupitia runinga zao.
Katika hili tunapenda pia kuchukua nafasi hii kuishukuru TBC1 kwa kuonesha ‘live’ tamasha hilo kwani kitendo hicho kimewezesha Watanzania wengi zaidi kusikia hotuba zote mbili, ya Mhe. Rais pamoja na ile ya waandaaji halikadhalika kujionea wenyewe mechi ya wabunge wa Simba na Yanga.
Mbali ya TBC1, tunapenda pia kuvishukuru vituo vingine vya televisheni vya Channel Ten, Clouds TV, Star TV, EATV, DTV na ITV kwa kuwahabarisha Watanzania maendeleo ya tamasha, kabla na baada ya kufanyika kwake. Hakika mmefanya kazi kubwa na mmeonesha mshikamano mkubwa.
Halikadhalika shukrani za kipekee ziviendee vituo vya redio vyote hususan Times FM, Clouds FM, Radio One, Praise Power, Wapo Radio na Radio Free Africa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuwahabarisha Watanzania ujio wa Tamasha la Matumaini.
Katika orodha hiyo ya shukurani kwa vyombo vya habari, hatuna budi kuwashukuru pia wadau wenzetu kwa upande wa magazeti; Jambo Leo, Tanzania Daima, Mwananchi, Habari Leo, Nipashe, Majira, Mtanzania, Bingwa, Dimba, Spoti Leo, The Citizen na mengine yote yaliyoripoti tamasha hilo.
Tutakuwa wachoyo wa shukurani kama tutaacha kuishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na uongozi mzima wa Uwanja wa Taifa kwa kutupa ushirikiano wa kutosha na kutuamini kufanya tamasha hilo katika uwanja wao.
Pia hatuna budi kulishukuru Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Kipolisi Temeke kwa kuimarisha ulinzi na ushirikiano mkubwa walioutoa wakati wa tamasha hilo.
Mwisho kabisa lakini ni wa muhimu sana, tunawashukuru wadhamini wetu TIGO kwa kutuunga mkono na kufanikisha tamasha kwa kiasi kikubwa. Watengenezaji wa vinywaji baridi nchini PEPSI kwa kuliunga mkono na kufanikisha tamasha hilo. Wasafirishaji wa vifurushi nchini, CDS kwa kutuunga mkono. TSN ambao ni wasambazaji wa kinywaji cha Willy Chilly na Shirika la PSI linalojishughulisha na vita dhidi ya HIV/AIDS, Malaria na magonjwa mengine nchini Tanzania.
MUNGU IBARIKI AFRIKA, MUNGU IBARIKI TANAZANIA
MUNGU LIBARIKI TAMASHA LA MATUMAINI
Asanteni kwa kusoma shukurani zetu za dhati kwenu.
Eric Shigongo
Mwenyekiti wa Tamasha
Na
Abdallah Mrisho
Mratibu Mkuu wa Tamasha
Chanzo Globalpublishers
0 Response to "TAMASHA LA MATUMAINI 2013: TUNAWASHUKURU WATANZANIA."
Post a Comment