Wafungwa Guantanamo wagoma kula Ramadhani | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Wafungwa Guantanamo wagoma kula Ramadhani

Wafungwa wa jela ya Marekani ya Guantanamo waliokuwa wanafanya mgomo wa kula wanaendelea na mgomo wao hata ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Zaidi ya wafungwa 130 walioko kwenye jela hiyo ya kutisha ya Marekani, kwa miezi mitano na nusu sasa wanagoma kula kama njia ya kulalamikia kushikiliwa kwa muda usiojulikana na kuteswa na maafisa wa jela hiyo ya Marekani.
Wafungwa hao wanaendelea na mgomo wao katika mwezi huu wa Ramadhani katika hali ambayo, maafisa wa jela hiyo wanawalazimisha kula wafungwa hao na wanatumia mirija ya plastiki kuwatilia chakula tumboni kupitia puani.
Makundi ya haki za binaadamu yamelaani kitendo hicho na kusema kuwa kuwatilia chakula tumboni wafungwa hao kwa kuwalazimisha na kwa kupitia mirija hiyo ya plastiki ni aina nyingine ya mateso kwa wafungwa hao.

Katika kampeni zake za uchaguzi mwaka 2008, Rais Barack Obama wa Marekani aliahidi kuifunga jela hiyo, na alikiri wakati huo wa kampeni kuwa jela ya Guantanamo ni nembo ya uvunjaji wa haki za binaadamu kwa serikali ya Marekani, hata hivyo miaka mitano imepita, na bado Obama hajatekeleza ahadi zake na hadi hivi sasa wafungwa 166 wanashikiliwa kwenye jela hiyo bila ya kuelezwa makosa yao.

0 Response to "Wafungwa Guantanamo wagoma kula Ramadhani "

Post a Comment