Kuanzisha biashara mpya ni jambo linalohitaji
maandalizi, hata hivyo kiwango cha
maandalizi kitatofautiana kulingana na mambo mbalimbali yakiwemo ukubwa
wa biashara yenyewe, kiasi cha mtaji, aina ya biashara, mazingira ya biashara
nk. Katika makala hii tutaegemea zaidi upande wa zile biashara ndogondogo
ambazo wengi wa watu hapa kwetu ndio huzifanya.
Kama tulivyotangulia kusema, mambo ya msingi
au kwa maana nyingine hatua zinazopaswa kufuata wakati wa kuanzisha biashara
ndogo hayatofautiani sana na yale mtu anapotaka kuanzisha biashara kubwa;
UTAFITI
Baada ya kufanya maamuzi ni biashara gani
unayotaka kuanzisha , kama ni bidhaa au huduma, sasa chunguza maswala
mbalimbali kama vile, eneo biashara itakapokuwa, wateja, soko, mfumo wa
biashara kisheria ikiwa ni mtu binafsi, ubia au kampuni, nk. Katika utafiti
unaweza ukapata majibu mengi kwa swali moja lakini unachotafuta hapa ni jibu
moja tu au mawili katika kuandaa mpango wa biashara hatua inayofuata.
MPANGO.
Hatua nyingine na iliyokuwa muhimu sana ni
mpango wa biashara yako. Mpango wa biashara ni majumuisho ya utafiti uliofanya
, hapa sasa ndio unapoamua ni njia zipi au mikakati ipi uitumie baada ya
kufanya utafiti. Madhalani uligundua aina mbili za bidhaa unazoweza kuuza,
chagua moja inayofaa zaidi na upange kuwa ndiyo utakayoiuza. Mpango/mchanganuo
wa biashara unaweza ukauweka kichwani tu, lakini unakuwa na maana na manufaa
zaidi unapoandikwa kwenye karatasi.
SUALA
LA FEDHA.
Kutafuta fedha kwa ajili ya kuanzia pia ni
hatua muhimu kabla haujaanza kufanya biashara. Kuna njia kadhaa na moja,
unaweza kupata mtaji kutokana na akiba yako mwenyewe uliyodunduliza kutokana na
vyanzo mbalimbali kama vile, mshahara, urithi, zawadi, faida ya biashara
nyingine nk. Njia ya pili, ni mkopo kutoka kwa aidha ndugu jamaa na marafiki au
taasisi mbalimbali za fedha zikiwemo benki na saccos.
MAANDALIZI
YA SEHEMU YA BIASHARA.
Eneo biashara itakapokuwa panaweza pakawa ni
duka, ofisi ama eneo lolote lile biiashara itakapofanyika. Utahitaji leseni na
vibali mbalimbali kulingana na aina na ukubwa wa biashara yenyewe. Biashara nyingine ndogo sana
hazihitaji vibali vingi na wakati
mwingine hauhitaji kuwa na leseni wala kibali chochote kile. Utahitaji pia kuwa
na bidhaa au huduma unazotarajia kuuza, vifaa mbalimbali kama vile, ofisi,simu,
kompyuta, fax na vitabu vya kumbukumbu na hesabu za biashara yako.
UENDESHAJI.
Uendeshaji wa biashara yako utategemea sana
Mpango wako wa biashara ulivyouandaa, iwe umeuhifadhi kichwani au hata
umeuandika kwenye karatasi. Katika hatua hii utatakiwa upange bei ya
bidhaa/huduma zako, kuweka mfumo wa kumbukumbu na hesabu wa biashara, kupanga
masaa ya kazi, kutafuta masoko, kampeni za matangazo nk. Yoote hayo itakubidi
ufuate mpangilio wako wa biashara huku ukifanya marekebisho pale hali halisi
inapokuwa tofauti na ulivyopanga kwani Mpango ni Dira, hauwezi ukalingana mia
kwa mia na hali halisi.
KUAJIRI.
Inawezekana wewe mwenyewe ndiyo kila kitu,
Mkurugenzi, Meneja, Sekretari na hata Mesenja ni wewe mwenyewe, lakini kumbuka
ni lazima tu utafika wakati biashara ikipanuka utahitaji kuajiri wasaidizi.
Kabla haujamuajiri mtu kwanza pima ikiwa hatua hiyo itakuwa na manufaa kwako au
la. Mchunguze unayetaka kumuajiri, fanya naye mahojiano kufahamu historia yake
vizuri ikiwa ni pamoja na wewe mwenyewe kuzingatia sheria na taratibu za nchi kama vile kutokuajiri watoto wadogo nk.
0 Response to "KUANZISHA BIASHARA YAKO, MAMBO YA MSINGI."
Post a Comment