TEKNOLOJIA DUNI SIYO SABABU YA TATIZO LA UVUSHAJI MIHADARATI KIHOLELA UWANJA WA J.K NYERERE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

TEKNOLOJIA DUNI SIYO SABABU YA TATIZO LA UVUSHAJI MIHADARATI KIHOLELA UWANJA WA J.K NYERERE


Habari na IPP MEDIA gazeti la The Guardian.
Uwanja wa J.K Nyerere, picha kutoka maktaba
Juzi, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa tatizo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kufanywa uchochoro wa kupitishia dawa za kulevya hautokani na kukosekana kwa vifaa vya kisasa, bali ni wafanyakazi wenyewe waliopewa dhamana ya kuusimamia.

Dk. Mwakyembe aliyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini kuwa katika uwanja huo kuna mitambo ya kisasa iliyofungwa kufuatilia shughuli zote zinazofanyika ikiwa ni pamoja na ukaguzi wa mizigo.

Kwa msingi huo, alisema siyo rahisi kwa mtu kupitisha dawa za kulevya bila kubainika.
Alisema taarifa kwamba yupo ofisa mmoja aliyechukuliwa hatua kutokana na sakata la dawa za kulevya, ni sawa na utani kwa sababu kwa mujibu wa picha zilizorekodiwa katika mitambo (CCTV) iliyopo uwanjani hapo siku ambayo dawa hizo kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8 zilipopitishwa Julai 5, mwaka huu kwenda Afrika Kusini ni wengi wanaostahili kuchukuliwa hatua.

“Tatizo hapa siyo mfumo wa mitambo, ni uswahili tu ndiyo unaofanyika hapa” alibainisha Dk. Mwakyembe.

Aidha, Dk. Mwakyembe aliahidi kuwa atavisafisha viwanja vya ndege ili dawa za kulevya zisipite tena hapo.

Alisema hatua atakazochukua itakuwa ni historia na kama wapo watu waliozoea kupitisha dawa za kulevya katika viwanja hivyo labda watafute njia nyingine ya kusafirisha kama ya punda.

Alisema haiwezekani dawa za kulevya kupitishwa kirahisi katika uwanja huo wakati kuna vyombo mbalimbali vya serikali kama Usalama wa Taifa, Polisi, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji na nyingine na wanalipwa mshahara na serikali.

Dk. Mwakyembe alisema alikaa kimya ili kuvipa muda vyombo vya usalama vijiridhishe na kumpa taarifa kutokana na sakata hilo kwani ni aibu kwa uwanja wa ndege wenye jina la Mwalimu Nyerere na nchi kwa ujumla, kuchafuka kimataifa kutokana na watu wachache wazembe.

Kwa hakika sisi tunaungana na Waziri Dk. Mwakyembe kuwa tatizo lililopo JNIA si vifaa vya kisasa vya kubaini dawa hizo, bali ni watumishi waliopo uwanjani hapo.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba yapo matukio kadhaa ambayo watu waliobeba dawa za kulevya, hunaswa katika uwanja huo huo na kwa kutumia vifaa hivyo hivyo vilivyopo.

Mfano rahisi ni muda mfupi baada ya Waziri Dk. Mwakyembe kufanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo juzi, mtu mmoja alinaswa akiwa na dawa za kulevya kwa kutumia vifaa hivyo hivyo ambavyo tunaelezwa kwamba si vya kisasa.

Mtuhumiwa huyo Mtanzania mwenye uraia wa Italia, anadaiwa kukamatwa akiwa na pipi 86 za dawa za kulevya na misokoto 34 ya bangi.

Tunataka tuamini kwamba kumbe kinachofanyika JNIA ni uzembe na tamaa ya watumishi wachache kutaka kupata utajiri wa haraka haraka.

Kama baadhi ya watuhumiwa wanakamatwa kwa kutumia mitambo hiyo hiyo, inakuwaje wengine mashine hizo hizo zishindwe kutambua dawa za kulevya?

Hili ni swali gumu kwetu kulijibu lakini watumishi wa JNIA wanaweza kulijibu kwa ufasaha kwa kuwa wanafahamu kila kinachoendelea kuhusiana na biashara hiyo haramu.

Tunawashauri na kuwasisitiza watumishi wa JNIA wawe waadilifu na kuacha kulichafua jina la Tanzania katika sura za kimataifa kutokana na tamaa zao zisizo na tija.

Ni dhahiri kwamba Tanzania inaheshimika sana kimataifa kutokana na mambo mengi mazuri.

Sisi tunazidi kusisitiza kuwa Waziri Dk. Mwakyembe asilegeze kamba aendelee hivyo hivyo kuwabana watumishi wachache wa JNIA wenye dhamira mbaya ya kuichafua Tanzania.

Imefika wakati sasa tuseme tumechoka na kwa kweli tumechoka na hatutaki tena Uwanja wetu wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uwe uchochoro wa kupitishia dawa za unga.

Na tunatoa rai kwa Waziri Dk. Mwakyembe asiwaonee huruma hata chembe wote watakaobainika kuwa walihusika kwa namna moja ama nyingine kupitisha dawa za kulevya zilizokamatwa nchini Afrika Kusini mapema mwezi uliopita.


0 Response to "TEKNOLOJIA DUNI SIYO SABABU YA TATIZO LA UVUSHAJI MIHADARATI KIHOLELA UWANJA WA J.K NYERERE"

Post a Comment