MWENYEKITI Mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi,
amesema kuwa biashara inayofanikiwa ni ile inayoanza na wazo kubwa na bora na
inaweza kuanza na mtaji mdogo.
Dk. Mengi alitoa mbinu hiyo ya biashara jana wakati wa hafla ya
kukabidhi zawadi kwa washindi watatu wa shindano la ‘Twitti’ na Reginald Mengi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Makao Makuu ya IPP, jijini
Dar es Salaam, Dk. Mengi alisema bila wazo bora la biashara, hata kama ukipata
sh milioni 100, huwezi kufanikiwa kibiashara.
Dk. Mengi ambaye alikuwa akichambua Tweet ya wazo bora la
mshindi wa kwanza, Lilian Wilson, alisema tatizo la wengi wanajiingiza kwenye
biashara na kukopa fedha nyingi kwa ajili ya mtaji, hawana mawazo bora la
biashara na ndiyo maana wanashindwa.
“Wengi wanaingia kwenye biashara bila mawazo bora na hata wale
wenye mawazo bora wakati mwingine hawajiamini kama wazo hilo ni bora na hawana
ujasiri wa kuyasimamia mawazo yao, hapo lazima utashindwa tu. Jambo jingine si
lazima uanze na fedha nyingi,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Uwekezaji
nchini, alisema vijana wakitumia vizuri fursa za biashara zilizopo, Tanzania
ina uwezo wa kuzalisha mabilioni 100 kila mwaka.
Washindi wa mwezi huu na kiasi cha fedha walizozawadiwa kwenye
mabano ni pamoja na Lilian Wilson (sh 1,000,000), Suzana Senga (sh 500,000) na
Ombeeni Kaaya (sh 300,000).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, kila mshindi alisema anatumia
zawadi walizopata kwa ajili ya kuanzisha biashara kwa kuzingatia mawazo
waliyoyatoa na kushinda.
Mratibu wa shindano hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Uongozi na Ujasiriamali (IMED), Dk. Donath Olomi, alisema jumla ya Tweets 979
zilishindanishwa na tatu kuibuka na ushindi.
Kwa mujibu wa shindano hilo la kila mwezi, washiriki wanatakiwa
Kutweet na Dk. Mengi kuibua mawazo mapya ya jinsi ya kuondokana na umaskini.
Katika swali la mwezi huu, washiriki wanatakiwa kuibua mawazo
mapya; ‘Jinsi gani rasilimali za nchi hii zinaweza kutumika kuongeza ajira kwa
vijana.
Chanzo:Gazeti, Tanzania daima.
0 Response to "DR.MENGI ATOA SIRI ZA BIASHARA"
Post a Comment