na Asha Bani
VYAMA vya CHADEMA na CUF
vimezidi kumwandama Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa hatua yake ya
kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi mkuu wa
kambi hiyo, Freeman Mbowe.
Wakati Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim
Lipumba, akilaani kitendo hicho cha Ndugai kumzima Mbowe na kuamuru askari
wamtoe nje kwa nguvu, alikiita ni cha udhalilishaji na kisichokubalika;
sekretarieti ya CHADEMA imeitisha kikao cha dharura kwa ajili ya kupokea
taarifa ya masuala mbalimbali yaliyojitokeza bungeni na kisha kutoa uamuzi wa
nini kifanyike.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari,
Prof. Lipumba alisema kuwa kitendo hicho ni cha aibu hakikupaswa kufanywa na
Naibu Spika wa Bunge kwani angesimama Waziri Mkuu Mizengo Pinda asingeweza
kumnyima nafasi ya kuzungumza.
“Sisi CUF tunajiuliza, angesimama Pinda
kuongea Naibu Spika angemnyima nafasi? Angethubutu kuamrisha askari wamtoe nje?
“Kwa nini haya yanatendwa kwa mpinzani na
hayawezi kutokea kwa kiongozi wa serikali?” alihoji.
Lipumba pia alihoji kama serikali ina
mamlaka makubwa katika Bunge kuliko Bunge lenyewe hadi kiti cha Spika kiendeshe
masuala kwa taratibu za kupendelea serikali.
Alisema kwa kuwanyima haki wabunge wa
upinzani hasa kiongozi wao wa pande zote mbili ni njama za wazi za serikali na
kiti cha Spika kutelekeza maoni ya wananchi na kuyapatia kipaumbele yale ya CCM
kwa maslahi yao.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa kufanya
hivyo kunaondoa uhalali wa Bunge na kiti cha Spika katika kusimamia mchakato
huo huku akitaja moja ya njama za wazi kuwa ni pamoja na ile ya wabunge 166 wa
Bunge la Katiba wanaopaswa kupendekezwa na taasisi mbalimbali na kuteuliwa na
rais.
“CUF tumesikitishwa na mabadiliko
yaliyofanywa na lengo la CCM la kupitisha muswada unaompa mamlaka ya uteuzi
rais kwani hivi sasa kila taasisi bila kujali uzito wake husika itapaswa kuteua
majina tisa na kumpa rais na kisha atateua jina moja au asiteue kabisa jina
lolote,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria hiyo inampa rais
mamlaka kuteua watu anaowataka kuwa wajumbe wa Bunge la Kutunga Katiba.
Prof. Lipumba alisema CCM na serikali yake
inajua kuwa hujuma wanazozifanya katika mchakato wa Katiba ndizo zitawapa
Katiba wanayoitaka wao kama chama na haitakuwa na uhalali wa wananchi.
Alisema kuwa ombi la wabunge wa upinzani
kuwa muswada huu urudishwe kwa wananchi na kwa kamati kujadiliwa upya lilikuwa
na mantiki kubwa, kwamba msimamo wao kupinga muswada huu unapaswa kuungwa mkono
na kila Mtanzania.
Lipumba pia alizungumzia kitendo cha
kudhalilishwa kwa wabunge akiwemo mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa
kupigwa waziwazi na askari ndani ya Bunge na kisha kutupwa kama mzigo nje ya
lango.
Alisema pia mbunge wa viti Maalum CUF,
Mozza Abeid, kuvuliwa vazi lake la hijabu ni udhalilishaji mkubwa kwa wanawake
na usiokubalika.
Alisema CUF inaendelea na juhudi ya
kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa
kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata Katiba mpya.
CHADEMA wakutana
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam jana, mkurugenzi wa habari na uenezi wa CHADEMA, John Mnyika,
alisema kikao chao cha sekretarieti kitakuwa chini ya Katibu Mkuu, Dk.
Willibrod Slaa.
Alisema kiongozi wa wabunge wa chama hicho
atatoa taarifa ya yaliyojiri wakati wa kujadili muswada wa sheria ya
marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 ambayo itajadiliwa
na wajumbe wa kikao hicho.
Mnyika alisema jambo kubwa
watakaloliangalia katika kikao hicho ni tafsiri ya mambo yote yaliyotokea kabla
muswada huo haujafikishwa bungeni ikiwamo uamuzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM)
kuingilia kati mchakato huo kwa manufaa yake.
“Yaliyotokea Septemba 4 hadi 6 bungeni
yalipangwa kwa sababu maalum na hii ni baada ya CCM kuona kila mwanya waliotaka
kuutumia kukwamisha rasimu ya katiba umeshindikana sasa wakaamua walitumie
Bunge,” alisema.
Mnyika alisema katiba ni ya wananchi na
kwamba kitendo chochote cha kuihujumu ni mbinu ya kuwanyima kupata haki ya
msingi ya kusikilizwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa mwelekeo wa kuwa na
katiba mpya itakayotumika mwaka 2015 haupo na kwamba hicho ndicho CCM
inakitafuta kwa nguvu zote baada ya kuona wananchi kutaka muundo wa serikali
tatu.
Alisema CHADEMA haiamini katika katiba
isiyojali maslahi ya wananchi na kwamba uharaka wa kukimbilia suala hilo hauna
maana kwa kuwa suala la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 linaweza kutungiwa kanuni
zake huku mchakato wa kupata katiba bora ukiendelea.
“Madai ya katiba ni zaidi ya vyama vya
upinzani, tutafanya taratibu ya kukutana na wadau mbali mbali nchini kwa ajili
ya kutoa uamuzi wa pamoja,” alisema.
Mnyika alisema njama za kuhakikisha wabunge
wa upinzani hawapati nafasi ya kujadili rasimu ya sheria ya mabadiliko ya
katiba zilianza mara baada ya rasimu kutolewa hali aliyoeleza kuzua hofu kwa
CCM.
Alisema hata maazimio ya Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria iliyokutana na wadau mbalimbali yaliathiriwa na kikao cha CCM
kilichokutana mjini Dodoma ambapo jukumu hili lilirudishwa kwa wabunge wao kwa
ajili ya kuhakikisha katiba ya Watanzania haifanikiwi.
“Kamati ya wabunge wa CCM ilipewa jukumu
hilo na mtekelezaji mkuu akiwa ni yule atakayekaa katika kiti cha spika
kuhakikisha wabunge wa upinzani hawatoi hoja zao,
CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA.
0 Response to "LIPUMBA, MNYIKA WAMKABA NGUGAI SAKATA LA KINA SUGU NA MBOWE "
Post a Comment