WANASAYANSI WA TIBA WATUZWA TUZO YA NOBEL KWA UGUNDUZI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WANASAYANSI WA TIBA WATUZWA TUZO YA NOBEL KWA UGUNDUZI

Msimu wa kutoa tuzo za Nobel umeanza kwa kutunzwa wanasayansi watatu na tuzo ya Fiziolojia au Utabibu, ambayo mwaka huu imewaendea Mjerumani Thomas Südhof na Wamarekani wawili, James E. Rothman na Randy W. Schekman.


Mmoja wa washindi wa tuzo ya utabibu ya Nobel, Thomas Südhof
Watafiti hao wametunzwa jana na kamati ya Nobel mjini Stockholm nchini Sweden kwa kugundua jinsi homoni na viini vingine vinavyotembea kati ya seli katika mwili wa binaadamu. Katika taarifa yake kamati ya Nobel katika taasisi ya Karolinska mjini Stockholm imesema kupitia uvumbuzi wao wanasayansi hao wamefichua mfumo wa udhibiti wa usafirishaji na upakuaji wa 'mizigo' ya seli.
Kamati hiyo imesema kwa mfano utafiti wao unaonyesha jinsi insulini inavyotengenezwa na kutolewa katika damu kwa wakati unaofaa na mahala panapostahiki. Kamati pia imesema washindi hao wametanua uelewa kuhusu jinsi matatizo na kuvuruga usafirishaji wa seli kunavyochangia kusababisha magonjwa ya neva, kisukari na matatizo ya maradhi

Profesa James E. Rothman, Randy W. Schekman na Mjerumani
 Thomas C. Sudhof (kutoka kushoto)
Mchakato wa 'usafirishaji na upakuaji' mwilini
Dereva wa basi la shule kimsingi ana shida kama ile ya seli mwilini. Analazimika kuusafirisha mzigo wake, yaani wanafunzi, kutoka sehemu moja hadi nyingine - kutoka nyumbani hadi shuleni na kisha kuwarudisha. Lakini ni kitu gani kinachoweza kutokea milango inapokwama na kukataa kufunguka anapofika kituo cha mwisho? Ama dereva anapowapoteza wanafunzi njiani? Bila shaka kutakuwa na ghadhabu kubwa!
Hivyo ndivyo mambo yalivyo pia kwa seli mwilini: husafirisha viini kama vile homoni kutoka sehemu moja hadi nyingine na hufanya hivi kwa kuvikusanya vitu hivi mfano wa kiputo. Kunapotokea matatizo wakati wa usafirishaji na vitu hivi visifike mahala vinapotakiwa, matokeo yake huwa mabaya: binaadamu huwa mgonjwa.
"Mchakato huu wa usafirishaji ni muhimu kwa maisha ya binaadamu," amesema Ann Wehman, mtafiti katika taasisi ya Rudolf-Virchow mjini Würzburg nchini Ujerumani. "Unajumuisha seli zote katika mwili wa kila kiumbe. Kama mchakato huu ungezuiliwa kabisa, sote tungekufa," akaongeza kusema mtafiti huyo.

Mjerumani na Wamarekani wawili
Utafiti wa mfumo huu muhimu wa maisha ya binaadamu umetunukiwa tuzo ya mwaka huu ya Fiziolojia au utabibu ya Nobel na kamati ya Nobel. Watafiti watatu waliotunukiwa tuzo hiyo ni Mjerumani Thomas Südhof, mwenye umri wa miaka 57, anayefanya kazi katika chuo kikuu cha Stanford katika jimbo la California nchini Marekani. Wengine ni James Rothman, mwenye umri wa miaka 62, wa chuo kikuu cha Yale mjini New Haven katika jimbo la Connecticut na Randy Schekman mwenye umri wa miaka 64, anayefanya kazi katika chuo kikuu cha Carlifonia huko Berkeley.
"Walistahiki. Wanasayansi hao watatu ndio mabingwa wakubwa katika eneo hili la utafiti," anasema Ann Wehman. Thomas Südhof anatokea Göttingen, ambako alisomea utabibu katika chuo kikuu cha mjini humo na kisha baadaye kuendelea na masomo yake ya shahada ya udaktati katika sayansi ya biokemia katika taasisi ya Max-Planck. Alipokuwa na umri wa miaka 27 Südhof alikuwa tayari na shahada ya uzamifu ya udaktari. Hatimaye akaelekea Marekani ambako anafanya utafiti katika chuo kikuu cha Stanford.
"Ni mwanasayansi anayefanya utafiti wa kina kwa umakini mkubwa. Ana kumbukumbu nzuri na kila mara hutoa mawazo mapya ili kuendeleza fani yake ya utafiti. Na hufanya hivyo kwa bidii kabisa," amesema Susanne Schorch McGovern wa hospitalini ya chuo kikuu cha Bonn. Susanne, ambaye alifanya kazi na Südhof kwa miaka mitano nchini Marekani, anasema alikuwa akitarajia bosi wake wa zamani angekuja kupata tuzo hiyo ya Nobel.
Kinyume lakini Südhof mwenyewe hakuwa na matarajio makubwa kwani hata alipopigiwa simu na kamati ya Nobel kujulishwa kuhusu ushindi wake aliuliza: "Unamaanisha kweli?" Südhof alijihusisha na suala la vipi seli za neva katika ubongo zinavyowasiliana.
Mwandishi: Osterath, Brigitte/Josephat Charo
Mhariri: Daniel Gakuba

0 Response to "WANASAYANSI WA TIBA WATUZWA TUZO YA NOBEL KWA UGUNDUZI"

Post a Comment