Amina Mohamed,waziri wa mambo ya nje wa Kenya |
Kenya imekuwa nchi ya
kwanza kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania kwa hatua yake ya
kutangaza bayana kwamba haiko tayari kutoka katika jumuiya hiyo kama
ilivyodhaniwa.
Wasiwasi kuwa Tanzania
ingejitoa kutoka jumuia ya Afrika Mashariki ulitokana na hali iliyojitokeza kwa
baadhi ya nchi za jumuia hiyo kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha
Tanzania na Burundi.
Baadhi ya wanasiasa na
wananchi nchini Tanzania walitaka nchi yao iachane na jumuia hiyo wakizishutumu
Kenya, Rwanda na Uganda kuitenga Tanzania hata katika mikutano ya masuala
yaliyohitaji maamuzi ya jumuia.
Kufuatia mfarakano
huo, ulionekana kutishia uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya
Kikwete wa Tanzania, wiki hii alilihutubia bunge la Muungano wa Tanzania mjini
Dodoma, katikati ya nchi na kutangaza bayana kuwa Tanzania haitatoka katika
jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani imefanya kazi kubwa kuifufua na kuiunda upya
baada ya kusambaratika mwaka 1977.
Kwa upande wake, Kenya
moja ya nchi waanzilishi wa Jumuia ya Afrika Mashariki na ambayo ilishutumiwa
kushiriki kuibagua Tanzania, imemtuma waziri wake wa mambo ya nje, Amina
Mohammed kwenda Tanzania na kuwa na mazungumzo na waziri mwenzie wa mambo ya
nje Bernard Membe kuhusu mfarakano huo na nia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa
nchi mbili hizo.
Katika mkutano na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumapili, waziri Amina Mohammed,
amesema Kenya inaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, kuhusu uamuzi wake
wa kutojitoa katika Jumuia ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza kuwa bila
Tanzania hakuna Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.
"Kama unavyojua
Kenya na Tanzania tumekuwa tukiijenga jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda
mrefu sana, tuko na mafanikio mengi sana, kuna mambo mengi tumeyafanya, kuna
njia ndefu imebakia kuna mambo mengi yasiyoweza kupimwa kati ya nchi hizi. Na
tuna tumaini kwamba tutaendelea kuijenga Afrika Mashriki kwa nguvu zote na
tutawasiliana na watu wetu kwa sababu tunataka watu wetu waishi vema na wawe
majirani wazuri na waendelee . Kwa Tunataka uchumi wetu uende vizuri. Kwa hiyo
tutaendelea kushirikiana, sisi ni wale wa kwanza tuliokuwa pale kwa hiyo
tunataka tufanye kile tunachoweza kuendeleza Afrika Mashariki..... Lakini
tumefurahia sana sana hotuba ya Rais aliyotoa pale bungeni na tunawashukuru pia
Watanzania kumuunga mkono."
Uhusiano wa Kenya na Tanzania ni wa Kindugu
Pia waziri Amina
amesisitiza kuwa hakuna namna ambavyo Tanzania na Kenya zitatenganishwa, kwa
namna ambavyo zimejenga maingiliano makubwa ya kijamii na kiuchumi, huku
akiomba Tanzania kusaidia kusukuma ombi la Kenya la kutaka kesi ianyomkabili
Rais wake, Uhuru Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi ili kumpa fursa ya
kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Benard Membe,waziri wa mambo ya nje wa Tanzania |
Kwa
upande wake waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Benard Membe amesema serikali
yake imefurahi kuona Kenya imekuwa nchi ya kwanza kuipongeza Tanzania kwa
kuinusuru jumuia ya Afrika Mashariki kama ilivyokuwa mwanzoni na kujenga
jumuiya ya watu na si ya viongozi, na kuahidi kushirikiana na Kenya katika
masuala mbalimbali likiwemo la kutaka kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta
katika mahakama ya ICC iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi.
Waziri
Membe amesema waziri mwenzake Amina kutoka Kenya amesema hotuba ya Rais Kikwete
imewazindua kwani hawakujua kuwa baadhi ya yale waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa
ni kukiuka taratibu za Jumuia ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa Kenya
itashirikiana kikamilifu na nchi waanzilishi halisi wa Jumuia ya Afrika
Mashariki.
Katika
kuonyesha nia thabiti ya kutotoka katika Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais
Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa bungeni, alisema "Tanzania ni
mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu na tunatimiza wajibu wetu kwa jumuia
na kuhusika kikamilifu katika ujenzi wake."alisema.
Rais
Kikwete alitumia muda mrefu katika hotuba hiyo kuchambua masuala mbalimbali ya
msingi ya uhai wa jumuia hiyo huku akisema ameshangazwa na nchi za Kenya,
Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania na Burundi.
0 Response to "Kenya yaiunga mkono Tz A.Mashariki"
Post a Comment