MADEREVA WA BODABODA, TAX NA DALADALA ZA USIKU SASA NI HATARI KULIKO ABIRIA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MADEREVA WA BODABODA, TAX NA DALADALA ZA USIKU SASA NI HATARI KULIKO ABIRIA

Mfano wa bodaboda
Madereva wa bodaboda na taxi siku za nyuma  na hata mpaka sasa hivi wanaogopa sana kuwabeba abiria nyakati za usiku, hasa wale abiria wanaowatilia mashaka, mathalani, wanaotaka kupelekwa safari za mbali,  nje ya jiji, kwenye njia za vichochoroni, ikiwa abiria wamekuja wawili au watatu, na ikiwa abiria amekuja akiwa na vitu visivyoeleweka kama silaha nk.

Mimi binafsi, kuna siku moja  majira ya saa tano za usiku nilichukua bodaboda maeneo ya stendi ya Buguruni Sheli inipeleke nyumbani. Karibu na maeneo nilipokuwa nikiishi, njia yake ilikuwa ni uchochoro wenye giza. Ghafla nilishangaa kumuona yule dereva wa bodaboda akisita na kusimamisha pikipiki baada ya kumuelekeza tuingie mle njia ya uchochoro. “ Kaka na nauli yenyewe nakusamehe shuka niondoke mimi huko sitaweza kwenda” Aliniambia yule dereva wa bodaboda. Jitihada zangu kumshawishi tuendelee na safari ziligonga mwamba, na mimi nikakasirika nikamjibu “Basi ondoka na nauli sikupi” Lakini kesho yake  baada ya kutafakari na kuona alikwisha nifikisha zaidi ya robotatu ya safari nilikwenda pale stendi nikamtafuta na kumlipa.

Kisa nilichotaka kukieleza hapa ni hiki cha abiria sasa kuwaogopa zaidi madereva wa bodaboda, tax na hata wakati mwingine wale wa daladala hasa zile za usiku zisizokuwa na TBL Sababu kubwa ya madereva hao kuogopwa ni visa vya uporaji, unyanganyi, utesaji na hata mauaji ambayo baadhi ya  abiria wamewahi kukumbwa nayo kutoka kwa hao madereva wenyewe na makondakta wao.

Kilichonisukuma kuandika kisa hiki ni kijana mmoja kwa jina Juma Muya anayesoma katika chuo kimoja huko Mbezi kwa Msuguri. Kijana huyo alinisimulia mkasa uliompata hivi majuzi na nilimuonea huruma sana. Akiwa anatokea maeneo ya chuoni kwao, yaliyo ndani kidogo kutoka barabara kuu  ‘Morogoro road’ Ili kufika stendi ya basi Mbezi kwa Msuguri ilimbidi apande bajaji au bodaboda. Ilikuwa majira ya saa 2 hivi usiku akaingia kwenye bajaji moja lakini dereva wa bajaji ile alimueleza  kwamba angechelewa kwani bajaji  ni lazima isubiri mpaka abiria wafike angalao wanne. Juma aliamua kuchukua bodaboda na aliyemuitia dereva wa hiyo bodaboda ni huyu dereva wa bajaji aliyempatia ushauri.
 
Bajaji ya miguu mitatu
Bodaboda walikuwa watu wawili , juma akadhani labda ni abiria ambaye naye alitaka kuwahi. Walipanda ‘mishikaki’ yaani watu watatu wakaondoka kuelekea stendi mbezi kwa Msuguri. Njiani juma alianza kuingiwa na wasiwasi  baada ya kuona bodaboda ikielekezwa kwenye mteremko, njia tofauti na ile waliyokuwa wakielekea. Aliruka kwa madhumuni ya kukimbia lakini bahati mbaya alitua chini na kuanguka kitendo kilichomfanya achelewe kukimbia. Alifanikiwa kuamka na kuanza kukimbia lakini tena wale jamaa walimzuia na pikipiki kwa mbele huku yule dereva akimhimiza mwenzake, kwa kumtaja jina, “‘Fulani’ fanya fasta, maliza kazi tusepe zetu”

Juma alihakikisha lile jina analishika vizuri akilini na baada ya kumpa kipigo, huku wakimchukulia kila kitu ikiwemo simu ya mkononi, pesa na hata viatu. Alirudi pale stendi walipoanzia safari na mtu wa kwanza kuonana naye ni yule dereva wa bajaji aliyemuitia bodaboda. Baada ya kumsimulia kisa kizima pamoja na kumtajia lile jina la kibaka mmoja, dereva wa bajaji aliwapa wenzake taarifa na wote walitoa ushirikiano wa kutosha huku wakiwalaani mno wahuni wale, “Hawa wanataka kutuharibia kijiwe chetu” walisema. Walikwenda polisi usiku ule ule na kesho yake ikabainika kumbe yule dereva kibaka wa bodaboda alikuwa ameachiwa pikipiki kama deiwaka, hakuwa dereva wa kudumu pale.

Alitiwa mbaroni na kupelekwa mahabusu, alipohojiwa alikiri kuhusika na tukio hilo la unyang’anyi na kumtaja mwenzake lakini walipomfuata kumkamata walikuta amekwisha kimbilia mafichoni kusikojulikana. Upelelezi wa kesi hiyo ungali bado unaendelea na mtuhumiwa namba mbili anaendelea kusakwa.
 
Daladala

Vitendo kama hivyo  wamewahi kufanyiwa abiria wengi pia katika daladala hasa zile za usiku ambazo unakuta hazina ruti maalumu. Licha ya kutokuwa na TBL, utakuta pia hazina vibali vingine muhimu kama bima na hata madereva wenyewe utakuta hawana leseni na wengi ni madeiwaka. Mkiwa abiria wachache na wakihisi mnaweza mkawa na fedha au vitu vya thamani kama simu za mkononi, huendesha gari kuelekea uchochoroni au njia tofauti ambapo huenda kuwadhuru na kuwapora kila kitu. Huna pa kwenda , na hata ukienda polisi huna ushahidi wowote wala vielelezo kama risiti nk. 

*Picha zilizotumika siyo za matukio yaliyosimuliwa, ni mifano na ni kwa hisani ya blogu za Burudani na kagera.org

0 Response to "MADEREVA WA BODABODA, TAX NA DALADALA ZA USIKU SASA NI HATARI KULIKO ABIRIA"

Post a Comment