Dar es Salaam.Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa jana
aliadhimisha miaka 75 ya kuzaliwa kwake kwa kufanya Ibada ya Misa iliyoongozwa
na Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Katika ibada hiyo ya shukrani iliyofanyika Kanisa Katoliki la Maria Imakulata, Upanga jijini Dar es Salaam, Mkapa aliwataka Watanzania kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Tunamshukuru Mungu kwa majaliwa aliyoipatia nchi yetu ya
Tanzania na tunamwomba azidi kuijalia umoja katika yote tunayofanya na
tunayokusudia kuyafanya,” alisema Mkapa.
Mkapa pia aliwashukuru waumini wenzake katika kanisa hilo, huku
akifichua siri kwamba, Kadinali Pengo alimtaka ahamie Kanisa la Mtakatifu
Joseph wakati alipokuwa rais, lakini hakukubali.
Kwa upande wake, Kardinali Pengo aliwataka Watanzania kuwa na
tabia ya kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
“Alichofanya Rais Mstaafu Mkapa ni cha kuigwa. Tunatakiwa
kutambua kuwa hatuishi kwa nguvu zetu bali kwa uwezo wa Mungu hivyo ni lazima
tumshukuru kama alivyofanya mwenzetu,” alisema Kardinali Pengo.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na
Mawaziri Wakuu Wastaafu, Edward Lowassa na Cleopa Msuya, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi na Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Wengine ni waziri wa zamani, Profesa Philemon Sarungi, Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa
pamoja wakuu wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Majenerali,
Robert Mboma na George Waitara.
CHANZO: MWANANCHI
0 Response to "Mkapa atimiza miaka 75 ya kuzaliwa wake"
Post a Comment