MABILIONEA wanne waliotajwa na Jarida la Forbes la nchini
Marekani wiki hii, wamemuumbua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, ambaye amekuwa akiwabeza kwamba hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta
ya gesi. (Gazeti la Tanzania Daima linalotoka kila siku Linaripoti)
Kwa mujibu wa jarida hilo, Rostam Aziz, ametajwa kuwa kinara kwa kumiliki utajiri wa dola za Marekani bilioni moja (sh trilioni 1.6), hivyo kuwa na uwezo wa kumiliki vitalu zaidi ya vitano vya gesi.
Mwenyekiti
Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, ametajwa kushika nafasi ya pili
katika orodha ya mabilionea hao kwani ana uwezo wa kumiliki pia visima zaidi ya
vinne kutokana na utajiri wake wa dola milioni 550 (sh bilioni 861).
Mo na Bakhressa
nao wametajwa kuwa na uwezo wa kumiliki vitalu vya gesi zaidi ya vitatu.
Wataalamu wa
mambo ya uchumi, waliliambia gazeti hili jana kuwa kwa viwango hivyo vya
utajiri, mabilionea hao si tu kwamba wana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya
gesi, bali pia wana sifa ya kuwekeza kwa pamoja na wawekezaji wa nje.
Taarifa ya
jarida hilo na kauli ya wachumi ni dhahiri kwamba imemvua nguo Waziri Muhongo
ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akibeza uwezo wa wafanyabiashara hao
kwamba wanaweza kuwekeza kwenye juisi na soda, akimlenga Mengi anayemiliki
viwanda vya soda na Bakhressa viwanda vya juisi.
Kauli hiyo
ilimfanya waziri huyo kuingia katika mzozo na Dk. Mengi, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Uwekezaji nchini (TPSF).
Dk. Mengi
amekuwa akisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania katika uchumi wa gesi
na kuishauri serikali kusitisha ugawaji wa vitalu hadi sera ya gesi itakapokuwa
tayari.
Rais Jakaya
Kikwete naye aliwahi kusema uchimbaji wa kisima kimoja cha gesi, unagharimu
dola milioni 100, sawa na sh bilioni 150, hivyo hakuna mzawa anayeweza kumudu
gharama hiyo na kuwataka kujiunga katika vikundi ili kuweza kumiliki ugawaji wa
vitalu hivyo uliozinduliwa mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa
utafiti wa jarida hilo, ni wazi kuwa iwapo Rostam Aziz ana nia ya kuwekeza
katika sekta hiyo, anaweza kumiliki vitalu zaidi ya vinne kutokana na kutajwa
kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Utajiri wa
Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi
na uchimbaji wa madini.
Anamiliki
asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom. Ni kampuni
inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini Tanzania, ikiwa na wateja
zaidi ya milioni 9.5.
Pia anamiliki
Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini katika migodi
inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Vilevile ana
hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa, inayofanya kazi za kupakua mizigo
bandarini na anamiliki majumba nchini na katika nchi za Mashariki ya Kati.
Mwingine mwenye
uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya gesi ni Dk. Mengi ambaye anaelezwa kuwa na
uwezo wa kumiliki visima zaidi ya vinne kutokana na utajiri wa dola 550 milioni
(sh bilioni 861).
Utajiri wake
unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki
magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni na takriban vituo 10 vya
redio. Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya soda aina ya
Coca-Cola.
Bakhressa kwa
upande wake, pia ana uwezo wa kumiliki rasilimali hiyo. Ana kampuni kubwa
inayoajiri zaidi ya watu 2,000 ikijishughulisha zaidi katika kusaga nafaka,
kusindika matunda, usafiri wa meli na biashara ya mafuta. Pia hutengeneza
pipi na ice cream.
Mo, ambaye
anafungana na Bakhressa kwa utajiri wa dola milioni 500 (sh bilioni 783),
mafanikio yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya wazazi wake.
Anafanya
biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta. Alinufaika baada ya
kununua viwanda vilivyobinafsishwa na serikali.
Alivifanya
viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya Mohamed Enterprises
(MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa Tanzania.
CREDIT: TANZANIA DAIMA
0 Response to "MUHONGO AVULIWA' NGUO"
Post a Comment