MWANAFUNZI ASIYEJUA KUSOMA WALA KUANDIKA AFAULU MTIHANI DARASA LA SABA MWAKA HUU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MWANAFUNZI ASIYEJUA KUSOMA WALA KUANDIKA AFAULU MTIHANI DARASA LA SABA MWAKA HUU

Katika hali ya kushangaza, Mkazi wa Kibaha Pwani bwana John Swai ambaye ni baba wa mwanafunzi aliyemaliza darasa la saba mwaka huu amelalamika akiilaumu Wizara ya Elimu na mafunzo ya  Ufundi baada ya mwanaye Immanuel Swai  aliyekuwa akisoma katika shule ya msingiRuhuwiko, Manispaa ya Songea mjini, Mkoani Ruvuma kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu  ili-hali mtoto huyo hajui kabisa kusoma wala  kuandika herufi za jina lake.


Akihojiwa na Radio WAPO FM leo hii asubuhi Swai alisema kuwa yeye na mkewe walitengana na watoto wakaenda kuishi na mama yao mkoani Ruvuma ambapo Immanuel baada ya kumaliza mtihani wake wa darasa la vii alikuja Kibaha Pwani ili aje amsaidie baba yake huyo shughuli za kuuza Duka. Anasema lakini baada ya kumchunguza mwanaye alibaini licha ya kumaliza elimu hiyo ya msingi  alikuwa hajui kitu, hata dukani kwenyewe alikuwa akimwacha na mfanyakazi ambaye humfundisha kwa kumuonyesha kitu fulani bei yake ni kiasi hiki nk.lakini siyo kwa kumuandikia au kusoma katika karatasi. Anasema aliwahi kumpima kwa kumpa gazeti la Mwananchi asome angalao kichwa cha habari lakini tena alichemsha hata kutamka herufi ya kwamna.

Baba huyo alisema yeye alikuwa na mpango wa kumrudisha mwanaye darasa la nne au la tano ili akajifunze upya kusoma na kuandika ndipo aliposhangazwa na taarifa kutoka kwa mzazi mwenzake kutoka Songea kwamba Immanuel ameshinda darasa la saba na alitakiwa kurudi Songea akaendelee na taratibu za kuanza form one.

Wapo fm iliongea na Afisa wa Elimu wa Manispaa ya Songea Edita Kagomba na kumuuliza kuhusiana na sakata hilo, yeye akajibu kwamba kwa wakati huo alikuwa nyumbani hivyo ni mpaka pale atakaporudi ndipo atakapolifuatilia suala hilo kujua kulikoni. Alisema yeye hawezi akakisia makosa yalikuwa ni ya nani, Shule, baraza la mtihani au mwanafunzi mwenyewe kwani wakati mwingine wanafunzi ni wajanja sana, anaweza akatumia mbinu zake kiujanja na akaweza kufaulu bila hata ya kusaidiwa na mwalimu.


Juhudi za Wapo kumtafuta Mkuu wa shule aliyokuwa akisoma mwanafunzi huyo hazikufanikiwa. Wakati wasikilizaji wakitoa maoni yao wengine walidai kwamba inawezekana hizo ni hila za baba mzazi wa Immanuel John kutaka mwanaye huyo asiende sekondari kwa lengo la kumtumikisha kazi za kuuza duka ukizingatia kwanza uhusiano wake na mzazi mwenzake sio mzuri, asingependa tena mwanaye arudi Songea kwa mama yake.

Picha kwa hisani ya  WWW.moe.go.tz

0 Response to "MWANAFUNZI ASIYEJUA KUSOMA WALA KUANDIKA AFAULU MTIHANI DARASA LA SABA MWAKA HUU"

Post a Comment