Jumuiya ya
Ushirikiano wa Kiislamu OIC imelaani na kukosoa vikali uamuzi wa serikali ya
Angola wa kuipiga marufuku dini ya Kiislamu nchini humo. OIC imetoa taarifa na
kusema imesikitishwa na kushangazwa na uamuzi wa serikali ya Angola wa kuipiga
marufuku dini ya Kiislamu na kuzitaka jumuiya na taasisi zote duniani kulaani
vikali hatua hiyo.
Taarifa ya OIC pia
imeutaka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, nchi zinazozungumza lugha ya Kireno
na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kuchukua msimamo madhubuti
wa kukabiliana na uamuzi huo wa serikali ya Angola. Jumuiya ya Ushirikiano wa
Kiislamu imesema uamuzi wa Angola wa kuipiga marufuku dini ya Kiislamu unakiuka
sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kuabudu. Wizara ya
Utamaduni ya Angola imetangaza kuwa dini ya Kiislamu ni marufuku nchini humo na
kwamba sasa serikali hiyo imeamua kuibomoa misikiti yote nchini humo.
Serikali ya Angola
imedai kuwa Uislamu si dini bali ni tapo tu la imani.
Wakati huohuo
mtandao wa habari wa Al Misril Yaum umemnukuu Mkuu wa masuala ya habari wa
chama tawala nchini Angola MPLA akisema kuwa hakuna msikiti wowote utakaofungwa
nchini humo. Ramadhan Shiblolo amesema Uislamu ni moja ya dini muhimu zaidi
duniani na kwamba habari za kufungwa misikiti nchini Angola hazina ukweli. Huku
akiashiria kuwepo misikiti mia moja nchini humo amesema Angola katu haitoupiga
marufuku Uislamu.
Katika upande
mwengine Sheikh Othman bin Zaid, Imamu wa msikiti wa Nurul Islam ulioko katika
mji mkuu wa Angola Luanda amesema serikali haijachukua uamuzi wa kufunga
misikiti na kwamba mkuu wa masuala ya kiutamaduni na kidini wa serikali
amekanusha habari za kuchukuliwa uamuzi kama huo. Sheikh Zaid amesema kuna
misikiti miwili iliyobomolewa kutokana na kujengwa katika eneo ambalo halikuwa
limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa misikiti.
SOURCE: IRB WORL SERVICE
0 Response to "OIC YALAANI KUPIGWA MARUFUKU UISLAMU ANGOLA"
Post a Comment