Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam
Aziz (49), ametajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa sasa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la Marekani la Forbes
na kutoa taarifa yake juzi, Rostam amekamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika
akiwa na utajiri wa Dola za Marekani bilioni moja (Sh1.6 trilioni).
Mbunge huyo wa zamani wa Igunga, ameingia kwa mara ya kwanza katika orodha ya matajiri 50 wa Afrika ya jarida hilo, pamoja na wafanyabiashara wengine wa Tanzania, Reginald Mengi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji ‘Mo’. Katika orodha hiyo pia yumo Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma.
Rostam, ambaye aliachana na siasa mwaka 2011, amempiku Bakhresa,
ambaye mwaka jana Jarida la Ventures Africa la Nigeria lilimtaja kuwa ndiye
aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho
alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni).
Katika orodha hiyo ya Ventures Africa, Bakhresa alifuatiwa na
Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi anashika nafasi ya pili kwa Tanzania na ya 34 Afrika akiwa
na utajiri wa Dola 550 milioni (Sh861 bilioni).
Forbes linaonyesha kuwa Bakhresa amefungana na Mo katika nafasi
ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika, wote wakiwa na
utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni).
Rostam, Mengi na Bakhresa hawakupatikana jana kuzungumzia suala
hilo huku Mo akisema kwamba asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa kuwa jana
alikuwa katika mapumziko ya Sikukuu ya Ashura.
Tajiri wa Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anajenga Kiwanda cha
Saruji huko Mtwara ndiye anayeshika nafasi ya kwanza katika orodha ya Afrika,
akiwa na utajiri wa Dola20 bilioni (Sh31.7 trilioni), akifuatiwa na familia ya
Johanny Rupert ya Afrika Kusini yenye utajiri wa Dola7 bilioni (Sh10.7
trilioni) na Nick Oppenheimer, pia wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa Dola 6.6
bilioni (Sh10.3 trilioni).
1)Rostam Aziz
Jarida la Forbes limeripoti kuwa utajiri wa Rostam unachangiwa
zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa
madini.
Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za mkononi
ya Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini
Tanzania ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.
Pia anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za
kuchimba madini katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na
Barrick Gold.
Pia ana hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi
za kupakua mizigo bandarini na anamiliki majumba nchini na katika nchi za
Mashariki ya Kati.
2) Mengi
Ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP.
Utajiri wake unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda
cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya
televisheni na takriban vituo 10 vya redio.
Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na viwanda vya CocaCola.
Alijiunga na Chama cha Wahasibu cha Uingereza kabla ya kurejea
Tanzania mwaka 1971 na kuajiriwa na Kampuni ya Ukaguzi ya Coopers & Lybrand
Tanzania (sasa Price Water House Coopers) hadi mwaka 1989, alipoacha kazi na
kujikita zaidi katika biashara.
3) Bakhresa
Said Salim Bakhresa ni mwasisi na Mwenyekiti wa Kampuni ya
Bakhresa Group na ana utajiri wa Dola500 milioni (Sh783 bilioni).
Ni kampuni kubwa inayoajiri zaidi ya watu 2,000 ikijishughulisha
zaidi katika kusaga nafaka, kusindika matunda, usafiri wa meli na biashara ya
mafuta. Pia kwa kutengeneza pipi na ice cream.
Bakhresa aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuanza
biashara ya kuuza viazi mbatata. Baada ya hapo alifungua mgahawa na baadaye
kuingia katika biashara ya kusaga nafaka.
4) Mo
Mafanikio yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza mali ya
wazazi wake. Anafanya biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Mo alirejea Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo
Kikuu cha Georgetown, Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo
yalianzishwa na baba yake.
Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na
Serikali.
Alivifanya viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni
ya Mohamed Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa
Tanzania.
Mo pia anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda
vya nguo na kilimo.
Jarida hilo lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao
kwa kuangalia thamani ya bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na hasa
wale walio kwenye sekta ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.
CHANZO NI MWANANCHI
0 Response to "ROSTAM AZIZ BILIONEA NAMBA MOJA MPYA TANZANIA AMPITA BAKHRESA"
Post a Comment