Urafiki wa mashaka wamaliza tembo | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Urafiki wa mashaka wamaliza tembo

Betty Kangonga wa Tanzania Daima 
WIKI iliyopita vyombo vya habari nchini viliripoti kukamatwa kwa pembe za ndovu 706 katika nyumba moja ya Mikocheni, Dar es Salaam wanakoishi wafanyabiashara watatu wa Kichina.
Operesheni ya kuwakamata Wachina hao na pembe hizo iliongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Pembe  za ndovu 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika nchi ya Tanzania ambayo idadi ya tembo katika mbuga zake inapungua kwa kasi.
Hii ni ishara kuwa hatua ya kuwakaribisha Wachina kuna haja ya kuwa waangalifu kutokana na taifa hilo kuaminika kuwa ni lenye watu wenye vipaji vya hali ya juu, hivyo kuna uwezekano wa kupukutika kwa wanyama hao kama tutaendelea kuwachekea Wachina.

Mfunyuku analijadili hili kwa kuwa taifa hili linaonyesha wazi ndilo lenye idadi kubwa ya wageni nchini kuliko taifa jingine lililowekeza.
Tunaambiwa kuwa Wachina hao walijifinya kuwa wanafanya biashara ya unga wa ndimu na vitunguu swaumu.
Watanzania tumejaliwa kuwa wakarimu na kushindwa kuhoji jambo, hasa tunapoona ngozi nyeupe, na hii ni kasumba inayoweza kuchangia rasilimali tulizobarikiwa kuendelea kutokomea.


Ninaamini kuwa hii si mara ya kwanza kwa Wachina kukamatwa na nyara hizo, wamekuwa wakijihusisha katika biashara mbalimbali kama magogo na hata madini.
Mara ngapi tumeshuhudia Wachina wakiingia katika maeneo ya vijiji na kuendesha shughuli mbalimbali zikiwamo za uchimbaji wa madini na kuharibu vyanzo vya maji, tena bila kuwa na vibali maalumu?

Pamoja na kushiriki katika matukio ya aina hiyo, jaribu kuuliza hadi sasa kuna Wachina wangapi waliohukumiwa kwa hujuma hizo?
Unaweza kukuta labda wapo wawili au hakuna hata mmoja. Ni kwanini? Labda unaweza kupata jibu rahisi kuwa kuna fedha inayotembea au kuna rushwa iliyoshamiri katika kila idara.

Ndiyo, unashangaa, si tumeambiwa kuwa Wachina hao walikutwa na kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya sh milioni 30 ndani? Unafikiri fedha hiyo ni kwa ajili ya matumizi yao tu au kuna ajenda nyuma yake?

Wachina wameshajua kinachotusumbua, hasa ukosefu wa fedha, hivyo wameamua kutumia fedha waliyonayo kuhakikisha wanaondoka na rasilimali zetu, tena wanajua kuwa hawawezi kuwekwa ndani kwa muda mrefu hata kama wanakamatwa na nyara.

Tunaambiwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipotembelea nchini China alipewa takwimu za Watanzania 120 kufungwa kutokana na kukamatwa na dawa za kulevya, tukanyamaza na kuona kuwa Watanzania hao wanastahili kukaa katika vifungo hivyo kutokana na dawa hizo kuwa na athari kwa jamii na wana haki ya kusubiri adhabu ya kunyongwa kwa kuwa sheria ya nchi hiyo ni kali kwa watu wanaokamatwa na ‘sembe.’
Pamoja na taifa hili kuwa nchi rafiki na Tanzania lakini urafiki wake una dosari. Nasema una shaka kwa kuwa vitendo vya Wachina kujifanya wawekezaji katika biashara ndogo ndogo zinazoweza kufanywa na Watanzania wa kawaida, kunatoa picha kuwa kuna biashara nyingine iliyojificha nyuma yao.

Hili linafanikiwa kwa kuwa wanatumia umaskini tulio nao na kuwatumia baadhi ya Watanzania wasio wazalendo na taifa hili, ndio wanaoweza kuwasaidia Wachina hao kuweza kufika katika hifadhi zetu na kuendesha vitendo vya ujangili.

Uzalendo uliopotea kuanzia kwa viongozi umesababisha hata baadhi ya Watanzania kuamua kushiriki katika vitendo hivyo vya kuihujumu nchi. Si tunaambiwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wamehongwa kuhakikisha wanapigania kusimama kwa Operesheni Tokomeza Ujangili? Je, hawa wana uzalendo na taifa hili? La hasha!

kufukua hata kama wapo wanaochukizwa na kalamu hii. Hili ni taifa langu, hatakuwapo Mchina wa kutetea rasilimali zetu.

Kama Watanzania wanawekwa gerezani huko kwao kwanini tuhofu wao kukaa ndani na hata kupewa adhabu kali ili kukomesha vitendo hivyo? Huu ni urafiki wa mashaka usio na tija.
Ndiyo maana wakati fulani baadhi ya Watanzania walitaka kuandamana kwenda kwa Waziri wa Viwanda na Biashara kulalamikia Wachina kuzagaa katika Soko la Kariakoo huku wakiuza bidhaa kwa bei ya chini, jambo linalowapa hasara wao, hatua ambayo ilizimwa na waziri wa kipindi hicho.

Wachina wanaamini kuwa jeuri yao ni fedha ndiyo maana wanaweza kufanya vitendo vya ovyo lakini huwakuti wakikaa ndani, hata si ajabu kuona kesi inayowakabili Wachina wa meno ya tembo 706 ikipigwa danadana na kushindwa kufahamu hatima yake.

Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete kuwa kama Operesheni Tokomeza Ujangili itaachwa, tukubali kuingia katika historia ya kuwa tuliwahi kuwa na tembo lakini sasa wamekwisha. Hii itakuwa aibu kwa taifa na Wachina hao tuliokuwa tukijifanya kuwa ni marafiki wakibaki kutucheka.

Mfukunyuku anachoona ni kuwa hakuna urafiki baina ya Wachina na Watanzania, bali viongozi wetu wamekubali kulaghaiwa juu ya uhusiano huo kwani vitendo vya Wachina kukutwa na wingi wa meno hayo ni ishara ya wazi kuwa urafiki wao si wa dhati.

Wachina na wanaojiita wawekezaji wameamua kutulaghai na kujifanya wema kwetu huku wakijua wanachovuna. Kukubali kuwa karibu na mataifa mbalimbali ni lazima tujue kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa changamoto mbalimbali hasa katika hili la ujangili. Inafahamika kuwa soko la biashara ya meno ya ndovu lipo nje ya nchi, hivyo vitendo hivyo vitafanywa na kuendeshwa na mataifa yanayohitaji bidhaa hizo.

Rais Kikwete alisema katika hotuba yake kuwa Tanzania ilikuwa na tembo 350,000 wakati inapata uhuru mwaka 1961 kabla ya ujangili kuibuka kati ya miaka ya 1970 na 1980.
Alisema sensa iliyofanyika mwaka 1989 ilibaini kubaki kwa tembo 55,000 tu nchini wakati Tanzania ilikuwa ikiongoza kwa idadi kubwa ya wanyamapori hao.

“Baada ya hapo serikali ilianzisha Operesheni Uhai iliyoongozwa na Kamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali John Walden, ambaye ametangulia mbele ya haki dhidi ya majangili. Tulifanikiwa, kwani mwaka 2009 ilipofanyika sensa ya wanyama, ilibainika tembo walikuwa 110,000,” alisema.

Alisema baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya la ujangili wa meno ya tembo. “Kati ya mwaka 2010 hadi Septemba 2013, meno ya tembo yaliyokamatwa ni 3,899, yenye uzito wa kilo 11,212. Pia vilikamatwa vipande 22 vya meno vilivyochakatwa kuwa fimbo na urembo ambavyo vilikuwa na uzito wa kilo 3,978,’’ alisema Rais Kikwete.

Alisema pia vilikamatwa vipande 4,692 vya meno ya tembo vikiwa vimetoroshwa nje ya nchi vikiwa na uzito wa kilo 17,797. “Hapo unazungumzia zaidi ya kilo 36,000, sawa na zaidi ya tembo 15,000.

“Operesheni Tokomeza Ujangili ni sahihi kabisa kulingana na manufaa yaliyopatikana katika operesheni zilizopita. Tusipochukua hatua ni sawa na kuwapa kibali majangili kuua tembo. Wanyama watakwisha na historia itatuhukumu vibaya,” alisema.

Kutokana na takwimu hizo ni muhimu kuangalia mahusiano yetu na mataifa yanayopatikana na nyara hizo, la sivyo tukubali kuendeleza urafiki wa mashaka huku tukiendelea kuumizwa.

HABARI NA MTANDAO WA FREE MEDIA


0 Response to "Urafiki wa mashaka wamaliza tembo"

Post a Comment