Na Suleiman Abeid, Shinyanga (BLOGU YA MAJIRA)
Wanachama wa vikundi vya wajasiriamali wadogo
katika kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuepuka kuingiza
siasa katika vikundi vinginevyo vitasambaratika
Tahadhari
hiyo ilitolewa juzi na diwani wa viti maalumu (CCM) manispaa ya Shinyanga,
Mariamu Nyangaka, alipokuwa akizungumza na viongozi wa vikund imbalimbali vya
wajasiriamali waliokutana kwa ajili ya kuanzisha Chama cha Ushirika wa Akiba na
Mikopo (SACCOS ).
Nyangaka
alisema viongozi wa vikundi vya wajasiriamali pamoja na wanachama wao kwa
ujumla wanatakiwa kuhakikisha wanaendesha shughuli zao bila kuingiza au
kutanguliza itikadi ya vyama vya siasa katika vikundi vyao kitu ambacho
kinaweza kusababisha mgawanyiko miongoni mwao.
Alisema
wapo baadhi ya wanasiasa wanaotumia wajasiriamali wadogo kufikia malengo yao
waliyojipangia huku wengine wakidiriki hata kuwazuia wafuasi wa vyama vyao
wasishirikiane na watu ambao si wafuasi wa vyama vyao vya siasa hata kama
shughuli zao zinapaswa kuendeshwa kwa ushirikiano wa pamoja.
"Ndugu
zangu mkakati ambao mnataka kuuanzisha ni mkakati mzuri utawasaidia kuendesha
shughuli zenu kwa ufanisi mkubwa, mtakapokuwa na SACCOS yenu itawasaidia kuweza
kupata mitaji ya kuendesha biashara zenu kupitia mikopo mtakayokopa yenye
masharti nafuu tofauti na inayotolewa na benki zetu nyingi
nchini,"alisema.
"Lakini
naomba mjihadhari na siasa katika vikundi vyenu, mkimruhusu mdudu huyu kuwa
miongoni mwenu eleweni wazi hamtadumu kwa kipindi kirefu, hakikisheni
mnaendesha shughuli zenu bila kuchanganya na itikadi za kisiasa na wakemeeni
wale wote watakaoonesha dalili za kuingiza siasa ndani ya vikundi,"
alisema Nyangaka.
Kwa upande wake ofisa
ushirika kutoka manispaa ya Shinyanga, Athumani, alisema serikali kwa kipindi
kirefu imekuwa ikihimiza umuhimu wa wananchi kujiundia vyama vyao vya ushirika
wa akiba na mikopo (SACCOS) kwa vile ni rahisi zaidi kusaidiwa na asasi
mbalimbali za kifedha. Alisema kupitia SACCOS watu wengi wamefanikiwa katika
biashara zao na baadhi wameweza kujenga nyumba za makazi huku wengine
wakisomesha watoto wao bila matatizo.
Alisema jambo la msingi ni uaminifu wa
viongozi wa SACCOS zinazoanzishwa kwa kuhakikisha zinakuwa na wanachama
waadilifu na wenye kuzingatia sheria za uendeshaji wa ushirika huo.
Katika hatua nyingine, viongozi
hao wa vikundi vya wajasiriamali wadogo wameunda uongozi wa muda utakaosimamia
taratibu za uanzishwaji wa ushirika wa akiba na mikopo.
Alisema utaundwa na
vikundi vyote vilivyopo katika kata ya Kitangili na kuhakikisha SACCOS hiyo
inasajiliwa kisheria ili iweze kuanza kazi mara moja.
Viongozi wa muda waliochaguliwa Elias Joseph (Mwenyekiti), Richard
Maige (mwenyekiti msaidizi), Patrick Kileo (katibu), Masunga Elias (katibu
msaidizi) ambapo Timothy Kakiri, alichaguliwa kuwa mweka hazina.
0 Response to "WAJASIRIAMALI WAONYWA KUHUSU SIASA"
Post a Comment