Katika HALI ya kustaajabisha abiria mmoja aliyekuwa
akielekea Muhimbili akitokea stendi ya Bugurunu, almanusura asababishe dereva
wa daladala kupeleka gari katika kituo cha polisi Msimbazi baada ya kumg’ang’ania
dereva wa basi hilo aliyezima ghafla wimbo huo wa bahati bukuku unaoitwa Dunia
haina huruma.
Kituko hiki kilianzia maeneo ya kona ya mtaa wa
Muheza mkabala na duka la kanda za muziki wa injili la Mbogo shop maeneo ya
Shule ya sekondari ya benjamini Mkapa. Dereva alipoanza tu kuchepuka akiingia
mtaa wa muheza ili kukwepa foleni ya pale ‘round about’ alizima redio iliyokuwa ikipiga
wimbo huo wa Bahati Bukuku, Dunia haina huruma ndipo abiria huyo mwanamke wa
makamo akaanza kulalamika ni kwa nini dereva amezima redio. Abiria tulidhani
labda atanyamaza lakini muda ulivyozidi kwenda naye alizidi kupiga kelele huku
akidai wimbo huo unamkumbusha mambo mengi sana likiwemo suala la kufiwa na mume
wake.
Mama huyu alitishia kwenda alipo dereva akafungue
redio mwenyewe ndipo kondakta alipoamua kumzuia. Mpaka tunafika maeneo ya kituo
cha Msimbazi Polisi ,mama huyo alikuwa bado akilalamika, huku watu wakishangaa
na kusema labda alikuwa na matatizo ya akili na alikuwa akipelekwa muhimbili
kwa matibabu. Wengine walidiriki hata kusema huyo aliyekuwa na huyu mama
ajitokeze kumtuliza lakini ilionekana alikuwa peke yake.
Mwishowe dereva
aliamua kufungulia tena redio yake akipiga wimbo ule ule wa Bahati Bukuku, Dunia
haina Huruma. Nilishuka kituo cha Msimbazi na sijui ni kitu gani kilichoenda
kujiri huko mbele ya safari,ikiwa yule mama aliendelea kupiga kelele au
aliridhika na kunyamaza baada ya kuwekewa ule wimbo.
0 Response to "WIMBO WA BAHATI BUKUKU DUNIA HAINA HURUMA NUSURA UPELEKE DALADALA KITUO CHA POLISI MSIMBAZI"
Post a Comment