BILL GATE AMPA MKAPA ULAJI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BILL GATE AMPA MKAPA ULAJI

Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa
Tajiri maarufu Duniani Bill Gates anayemiliki Kampuni ya Microsoft amempa kazi Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa kwa kumteua kuongoza chombo cha kampuni hiyo katika uwekezaji wa kimkakati barani Afrika.


Taarifa iliyotolewa jana na kampuni hiyo ya Microsoft ambayo inamilikiwa na Gates, ilisema chombo hicho kinafahamika kama Baraza la ushauri la 4Afrika (4Africa Advisory Council) na kazi yake kubwa itakuwa ni kuishauri, kampuni hiyo katika miradi yake ya kulifanya bara hili liwe na ushindani katika sekta ya teknolojia ya mawasiliano.

Akizungumzia uteuzi wake huo Mkapa alisema amefurahishwa na uteuzi wake huo na kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha mpango wa 4Afrika unafanikiwa kwa faida ya bara hilo. “Ninaamini sana katika mpango wa 4Afrika. Ni matumaini yangu kwamba heshima hii niliyopewa ya kuwaongoza wajumbe wenzangu mashuhuri katika mpango huu itasaidia  kuwakuza viongozi wetu, kusidia na kuchochea biashara na pia kuonyesha ubunifu unaofanyika barani Afrika” Alisema Mkapa.

Mradi wa 4Afrika ulianzishwa rasmi February mwaka huu na Microsoft na kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, kikao cha kwanza cha baraza hilo la ushauri kilifanyika jijiniDar es salaam, Oktoba mwaka huu.

Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho cha kwanza cha baraza hilo yalikuwa ni kujaza nafasi nyingine za wajumbe kwa kutumia vijana wenye akili na wanaochipukia  katika maeneo mbalimbali ya kiuongozi na teknolojia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Microsoft, Makamu rais wa Baraza atakuwa ni raia wa Afrika kusini, Mteto Nyati, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Microsoft nchini Afrika Kusini.

Taarifa hiyo ya Microsoft iliwataja wajumbe wengine wa baraza hilo kuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayofahamika kwa jina la ushahidi, Juliana Rotich, Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni za Orascom, Hanan Abdelmeguid, mjasiriamali anayefanya shughuli zake nchini Ghana Bright Simons na mwanzilishi wa mtandao wa Live Wello nchini Nigeria Frorence Iwegbue.


Wengine ni Marieme Jamme, Luis Lelis, Phuti Mahanyele, Richard Attias, Benjamin Mophatlane, Monica Musonda, na taarifa hiyo ikamtaja Louis Otieno kuwa ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya kisheria wa Microsoft Barani Afrika kuwa Katibu wa Baraza hilo.

Chanzo: Gazeti la kila siku la Raia Tanzania dec. 13. 2013

0 Response to "BILL GATE AMPA MKAPA ULAJI"

Post a Comment