MAKAMPUNI 100 VINARA, NDIYO HAYA HAPA. YAKIONGOZWA NA KIPIPA MILLERS LTD | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAKAMPUNI 100 VINARA, NDIYO HAYA HAPA. YAKIONGOZWA NA KIPIPA MILLERS LTD


Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, akimkabidhi tuzo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Seedco Tanzania Limited, Dk Joel Kabisa (kulia) na mkewe Agnes Kabisa baada kampuni hiyo kushika nafasi ya tatu katika kinyang’anyiro cha tuzo za kampuni za kati zinazofanya vizuri (Top 100). Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Zuhura Muro. PICHA | EMMANUEL HERMAN

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema kuwa, Serikali itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili wawekezaji wa nje na ndani waweze kutekeleza majukumu yao bila kikwazo.


Dk Kigoda aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa kwenye hafla ya kuzitambua Kampuni 100 Bora zinazokua kwa kasi nchini (Top 100 Mid–Sized Companies), ambapo Kampuni ya Kipipa Millers Limited ya jijini Mwanza ilishika nafasi ya kwanza.
Kampuni hizo zilitambuliwa na kupewa tuzo kutokana na shindano linaloendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) na KPMG Tanzania na kudhaminiwa na Benki ya NBC pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Dk Kigoda alisema shindano hilo linaimarika kila mwaka na lina nafasi kubwa ya kuimarisha uchumi kwa Kampuni za Afrika Mashariki.
Alisema ili kampuni hizo ziweze kufikia mafanikio, Serikali itajitahidi kuweka mazingira yatakayoziwezesha kufanya shughuli zake vizuri na kufanya uzalishaji kwa gharama nafuu.
Alizitaka kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye kundi la kampuni 100 bora, kujitambua kuwa sasa wao ni washindi na hivyo wajitahidi kufanya shughuli zao kitaalamu zaidi.
“Kwa kiwango hiki mlichofikia sasa ni washindi, mfanye kazi zenu kitaalamu zaidi,”  alisema Dk Kigoda.
Alisema kwa sasa Tanzania imeshuka kwenye nchi zenye viwango vizuri vya kufanya biashara duniani, hali inayofanya baadhi ya wawekezaji kukimbia.
Alieleza suala hilo linaipa Serikali changamoto ya kutengeneza mazingira bora na rafiki ili kuvutia wawekezaji kufanya shughuli zao kwa faida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Zuhura Muro alisema kwa kushirikiana na KPMG, wanaendesha shindano hilo kwa sababu wanaelewa kuwa hiyo ni njia muhimu ya kuhamasisha kampuni kufanya vizuri.
Alisema kuwa, kampuni hizo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na ustawi wake kwani kodi wanazolipa ndizo zinazotumika kwa maendeleo ya nchi.
“Sasa ni wakati wetu wa kuinuka, lakini hatuwezi kuinuka bila kuwa na watu muhimu kama ninyi (kampuni 100 bora) kwani ndiyo mnaotengeneza ajira, nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii,” alisema Muro.
SOURCE: MWANANCHI

0 Response to "MAKAMPUNI 100 VINARA, NDIYO HAYA HAPA. YAKIONGOZWA NA KIPIPA MILLERS LTD"

Post a Comment