Anayedaiwa
kuwa mchawi aliyedondoka na ungo akisulubiwa kabla ya kuuwawa.
|
Matukio
ya watu kudondoka na ungo siyo mageni hata kidogo miongoni mwa jamii za Kitanzania
na hata za Kiafrika kwa ujumla. Ni mara nyingi tu hasa kwenye vyombo vya habari
utasikia mtu/watu katika eneo fulani wamedondoka kwa ungo na katika kila tukio
hadithi ya mchawi/wachawi hao kuwa walikuwa wengi, lakini wenzake wakakimbia na
kumuacha huwa haikosekani, hamna hata siku moja imewahi kusikika kwamba watu
wawili ama wote waliokuwa katika safari moja wameanguka.
Matukio
haya hugubikwa na imani potofu za kishirikina huku wananchi wanaowakamata
wachawi hao wakidai kuwa wamechoshwa na vitendo vya kishirikina na hujidai kuwa
na hasira kali, huongozwa na “Mob Psychology”, kitendo
kinachosababisha mtuhumiwa kuuwawa pasipo hata kuchunguza ushahidi ikiwa ni
kweli alidondoka kwa ungo ama la. Matukio hayo yapo mengi sana na kila mwaka
utasikia jijini Dar na hata huko mikoani watu wakiwa wamenaswa baada ya
kudondoka na ungo, lakini tukio lililonifanya niandike makala hii ni hili
lililotokea hivi karibuni huko mbezi, “Picha za namna mchawi alivyoanguka jijini Dsm na kuuwawa na Wananchi”, unaweza kulitazamahapa kabla hujaendelea na makala hii zaidi.
Ukweli
kwamba watu hao hudondoka kwa ungo hakuna mtu anayeweza kuthibitisha pasipokuwa
na shaka yeyote, hata kama ikiwa mtuhumiwa mwenyewe anakiri hadharani kwamba
alidondoka kweli. Inawezekana kabisa mtuhumiwa akakiri hivyo kutokana na sababu
mbalimbali zikiwemo kuogopa hasira na kipigo kutoka kwa wananchi hao, kutokana
na sababu zake binafsi kwa mfano ni kutokana na lengo la yeye kujifanya
amedondoka kwa ungo sababu ambazo mara nyingi huwa ni za kujinufaisha kibiashara aidha kwake binafsi
au kwa mtu mwingine na mara nyingi huwa ni waganga wa kienyeji ambao humtumia mhusika na kisha kujifanya yeye
ndiye aliyemdondosha halafu baadaye wananchi walioshuhudia hujenga imani kwake
na kuwa wateja wazuri.
Sababu
nyingine hutokana na baadhi ya madhehebu ya dini ambayo hutengeneza tukio la
kuigiza kwa mtu kuambiwa ajifanye kadondoka kwa ungo na kisha huandaliwa mazingira
ambayo wahusika wa lile dhehebu huhusishwa kwa namna moja au nyingine. Wakati
mwingine hata mtuhumiwa huelekezwa kupanda juu ya paa la nyumba ya ibada na
kisha kujidondosha katikati ya waumini wakiomba, waumini hao utakuta hawana
taarifa yeyote juu ya ‘mchongo’ huo isipokuwa wale viongozi wanaohusika tu.
Waumini kwa kuwa hawakuwa na habari basi hueneza taarifa hizo haraka na mara moja
dhehebu hupata waumini wengi baada ya kuambiwa kuwa ni nguvu za Mungu ziliweza
kumdondosha mchawi na isingewezekana kabisha akatize katika anga lile kirahisi.
Sabau
nyinginezo hutokana na Magonjwa ya akili, matukio mengi yanayosemekana ni watu
kuanguka kwa ungo, ukiyachunguza kwa makini utabaini ya kwamba watuhumiwa ni
wagonjwa wa akili, na wengi ni vikongwe ambao magonjwa ya namna hiyo hasa ugojwa
wa kusahau ni kitu cha kawaida. Anapoulizwa katoka wapi hushindwa kujibu
kutokana na ugojwa wa kusahau, na hata anakokwenda pia huwa masikini haelewi,
kwa hiyo wananchi kitendo hiki hukitafsiri kama kwamba mtuhumiwa ni mchawi na
kuzidi kumuadhibu pasipo kujua kwamba hata na wao ipo siku watazeeka na pengine
kukutwa na hali kama hiyo. Wenzetu nchi kama Uingereza hili wanalitambua na
wazee waliokuwa na matatizo kama hayo huwekwa sehemu moja na kutunzwa vizuri.
Cha
kushangaza sana ni kwamba katika matukio yote hayo, stori huwa ni ile ile
haibadiliki sana, utaambiwa kwamba wananchi kabla hata ya kumuua mtuhumiwa
kwanza zana zake zote za kichawi ikiwa ni pamoja na ungo wenyewe walivitia moto.
Pia utaambiwa kuwa mchawi huyo alikuwa akienda kwenye mkutano na wachawi
wenzake na kama siyo visiwa vya shelisheli, Comoro sumbawanga, au Brazili basi
watakuambia ni msumbiji. Hapa inatia shaka sana, ni kwa nini vifaa hivyo
visitunzwe vikaja kuonyeshwa kwa waandishi wa habari na picha zikapigwa?
Umati
wa raia ukiwa umemzingira aliyedaiwa kudondoka na ungo
|
Ukikuta
matukio ya kutengenezwa mfano na waganga wa kienyeji kwa lengo la kujipatia
wateja mara nyingi mhusika humuwekea na vifaa zikiwemo tunguri za vibuyu na
ungo wa ukweli lakini shaka huja pale ambapo haijawahi hata siku moja ‘mchawi’
akanaswa akiwa angani na mtu angalao akafanikiwa kupiga picha ikaonekana.
Na
waandishi wa habari nao kwa kutaka kuuza huweka chumvi yingi katika habari hizo
na kuandika kwa mtindo ambao huwafanya watu kuamini kuwa ni kweli watu hao
walidondoka kwa ungo, hebu tazama habari hii hapa iliyoandikwa na uwazi mwaka
2010 ya mtu mwingine tena aliyedaiwa kudondoka na ungo na kuuwawa, “Aliyedondokana ungo na kuuwawa: kumbe siyo mchawi” utafahamu ukweli juu ya matukio
haya na jinsi ambavyo watu huyachukulia ndivyo sivyo. Habari iliyotanguliwa na
hiyo ambayo ndiyo iliyoanza kutolewa ni hii hapa iliyosema “Aliyedondoka na Ungo Dar”
Shukurani kwa mitandao ya Global publishers na Sangafesto blog.
0 Response to "NI MAAJABU:MCHAWI ALIYEUWAWA BAADA YA KUDONDOKA NA UNGO HUKO MBEZI"
Post a Comment