SHINDANO HATARI LA KUFUNGA MWAKA 2013 NA KUUPOKEA MWAKA MPYA 2014 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SHINDANO HATARI LA KUFUNGA MWAKA 2013 NA KUUPOKEA MWAKA MPYA 2014

“Ama kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni” na Dunia haiishi vituko kwani kila kukicha iwe ni hapa Tanzania au Ughaibuni mambo ya kustaajabisha hutokea. Siyo Ulaya, Asia wala Amerika, ni hapa hapa Bongo kweli yametokea. 


Jamaa mmoja kwa jina Saidi Shija maarufu kwa jina la utani ‘PENGO’ huko mkoani Pwani katika kitongoji cha Picha ya Ndege, amefunga mwaka kwa kituko cha aina yake baada ya kuitisha shindano la Hatari la kifo, kuufunga mwaka 2013 na kuukaribisha ule wa 2014.

Ni hivi; yeye Shija ameweka dau la  shilingi  laki tano, na kisha mtu mwingine yeyote atakayependa kushiriki naye atatakiwa kuweka dau kama hilo au kiwanja nusu hekari. Kinachoshindaniwa hapa ni bahati ya kuuvuka salama mwaka 2013 na kuingia mwaka 2014 pasipo kuiaga Dunia. Hii  ina maana kwamba ikiwa mshiriki atakufa kabla ya kuuona mwaka 2014 basi atakuwa ameshindwa shindano na dau lake aliloweka litagawanywa kwa washiriki watakaokuwa wamevuka salama bila ya kupoteza maisha.

Hii siyo mara yake ya kwanza Saidi Shija kufanya shindano kama hilo, alilifanya tena mwaka jana kwa kuweka dau la sh.laki moja, lakini kutokana na hofu watu hawakujitokeza kushiriki na hivyo yeye mwenyewe akaibuka mshindi bila kupingwa. 

Watu wengi walisikika wakisema hawawezi kushindana na Mungu, kutokana na kitendo hicho kuonekana kama ni cha kumkufuru Mwenyezi Mungu,ni kama kujichuria kifo vile. Bado haijajulikana mara moja ikiwa mwaka huu watajitokeza washiriki zaidi kwani ni mapema mno, mpaka pale mwaka utakapomalizika.

Tayari taarifa za kuwepo kwa shindano hilo zimekwishafikishwa katika ofisi za serikali ya Mtaa ya eneo la Picha ya Ndege na Mtayarishaji wake ambaye ni Bwana  Pengo mwenyewe ikiwa ni hatua za kuzidi kuliweka bayana na kulitangaza kwa washiriki wengi zaidi.

Chanzo cha Habari: WAPO radio fm na kuandikwa upya na SHPL



0 Response to "SHINDANO HATARI LA KUFUNGA MWAKA 2013 NA KUUPOKEA MWAKA MPYA 2014"

Post a Comment