WE WILL MISS YOU MANDELA: KAMA ALIVYOIMBA CHICCO 1987 WE MISS YOU MANELO” KWELI TUTAMKOSA MANDELA. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WE WILL MISS YOU MANDELA: KAMA ALIVYOIMBA CHICCO 1987 WE MISS YOU MANELO” KWELI TUTAMKOSA MANDELA.


















Kumbukumbu zangu za utotoni miaka ya 80, hasa mwaka 1987 na kuendelea mpaka Nelson Mandela alipoachiwa kutoka gerezani mwaka 1990, wimbo wa mwanamuziki maarufu nchini Afrika ya kusini Chicco “WE MISS YOU MANELO” au We miss you Mandela kama watu walivyoutafsiri ulitikisa sana mitaani na hata katika madicso ya kienyeji. Umaarufu wa wimbo huu ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na umaarufu aliokuwa nao Shujaa wa kupigana na ubaguzi wa rangi Nelson Madiba Mandela.

Sikiliza audio ya wimbo huo "we miss you manelo" hapa


“Selo Twala” kwa jina la utani ‘Chicco’ wakati akitunga wimbo huu inasemekana alikuwa anamlenga Mandela moja kwa moja wakati huo akiwa amefungwa katika gereza la “Robben Island” lakini kutokana na hali ya kisiasa wakati huo ya Makaburu kutokupenda kusikia harakati za watu weusi kudai Mandela aachiwe huru, kwa kufanya hivyo wazi wazi mtu ungeweza hata kuuwawa au kufungwa jela ndiyo maana Chicco akaamua kutumia jina la Manelo badala ya Mandela. Hata hivyo ujumbe ulifika barabara  kwa hadhira aliyokusudia.

Video ya wimbo 'we miss you mandela' hii hapa ukipenda itazame




Tukiwa leo hii tunaomboleza kifo cha Shujaa huyu wa Afrika aliyefariki jana usiku akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuugua na kulazwa hospitalini Medclinic kwa muda mrefu, siyo vibaya tukajikumbusha kidogo historia yake na ya mapambano dhidi ya Ubaguzi wa rangi pamoja na Uhuru wa Binadamu kwa ujumla. Mandela alizaliwa hapo mwaka  1918 na kupewa jina  la kienyeji Rolihlahla  lenye maana ya “Trouble maker” au mtu wa matata, baba yake alikuwa ni chifu wa kabila. Mwaka 1952, alifungua kampuni yake ya Sheria, ya kwanza kufunguliwa na mtu mweusi nchini A.Kusini.

Mwanasheria Nelson Mandela akiwa ofisini na mafaili yake mkononi.

Aliyekuwa sekretari wake katika kampuni hiyo Ruth Mopati akiandika kumhusu Mandela alivyokuwa alisema hivi; “Alikuwa na uwezo wa kuhusiana na watu kwa heshima, na kwa hiyo watu nao walimheshimu vilevile”

Baada ya Mandela kuingia chama cha ANC mwaka 1952  alianzisha maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi kote nchini A.Kusini jambo lililoifanya serikali ya Makaburu mwaka 1960 kukipiga chama cha ANC marufuku kwa lengo la kuzuia maandamano na migomo zaidi. Lakini kitendo kile ni kama vile walimwagia petrol kwenye moto uliokuwa unaanza kuwaka. Chama cha ANC kikaanzisha tawi la kijeshi mwaka 1961 chini ya kamanda wake wa kwanza Bwana Nelson Mandela.

Kijana Nelson Mandela miaka hiyo ya 60

Mwaka 1962 Mandela alifungwa gerezani kwa kosa la kuchochea migomo, na miaka miwili baadaye akahukumiwa kwenda jela maisha kwa makosa ya uhaini kutaka kupindua serikali. Katika miaka yote 27 aliyokaa gerezani, muda mrefu aliupotezea katika gereza la Robben Island ambako alifanya kazi ngumu katika machimbo ya chokaa.

Kwa kipindi chote hicho akiwa nyuma ya Nondo Serikali ilijitahidi sana kuhakikisha kwamba kizazi kijacho hakipati kabisha nafasi ya kufahamu ukweli kuhusu Shujaa huyu mfungwa maarufu zaidi duniani wa kisiasa. Ilipiga marufuku, picha zote, maneno,  miziki, na kitu cha aina yeyote kilichoashiriakumuenzi Mandela.

Tazama hapa historia yake kwa ufupi katika video hii


Baada ya miaka 27, hapo mwaka 1990, aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini wakati huo  F.W. de Klerk alitangaza rasmi kwamba Bwana Mandela ataachiwa huru kutoka gereza la ‘Victor Vestor’  na ilipofika Mwezi Februari 11 mwaka 1990 Nelson Mandela kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takriban miongo mitatu akaliona tena jua.

Miji inayokaliwa na watu weusi ililipuka kwa vifijo na kila aina ya nderemo, huku kiongozi wao mpendwa Nelson Mandela akiwahutubia kwa kusema “Leo hii wananchi wote wa Afrika ya Kusini, Weusi kwa Weupe-fahamuni kwamba Ubaguzi wa rangi umemalizika”

Ijapokuwa kulitokea machafuko ya hapa na pale kipindi kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwaka 1994, na baadhi ya watu wakafariki, hata hivyo ilipofika tarehe 27, April 1994 katika hali ya kutokuamini kile kilichokuwa kikitendeka mamilioni ya waafrika weusi walikuwa wakimiminika kwenye vituo vya kupiga kura yao yao kwanza. Katika uchaguzi ule chama cha ANC kiliibuka mshindi na  Nelson Mandela akawa Rais wa kwanza mweusi wa Taifa la Afrika kusini. Alibakia madarakani kwa miaka mitano mpaka mwaka 1999, alipokabidhi madaraka kwa njia ya amani kwa mrithi wake Thabo Mbeki.

Tazama hapa chini hotuma ya Rais Nelson Mandela wakati akistaafu hapo mwaka 1999

Maisha yake na Winnie Mandela baada ya Kutoka gerezani hayakuwa mazuri sana kutokana na mke wake huyo wa zamani kukabiliwa na ‘skendo’ za aina mbalimbali ikiwemo ya kuwateka vijana wa kiume wanne ambao mmoja wao alikuja kukutwa ameuwawa, kesi iliendelea akafungwa miaka 6, lakini hatimaye Winnie alikuja kupunguziwa kifungo na  kutiwa hatiani kwa kosa la wizi  akatozwa faini. Skendo hizo pamoja na madai ya Mandela mwenyewe kuwa Mkewe huyo hakuwa mwaminifu vilimfanya mwaka 1995 aende mahakamani kudai watengane akionyesha ushahidi wa mkewe kutokuwa mwaminifu jambo lililomfanya aishi mpweke.

Mke wa zamani wa Mandela Bi Winnie Mandela.

Hata hivyo Mandela baada ya kuachana na Winnie penzi jipya lilimea kati yake na Graca Machel, aliyekuwa mjane wa Rais wa Msumbiuji, Samora Machel. Mwana mama huyu ni mpiganiaji maarufu wa haki za watoto. Wawili hawa walifunga pingu za maisha rasmi hapo mwaka 1998 Mandela alipokuwa akitimiza umri wa miaka 80 wakati Graca yeye akiwa na umri wa miaka 52.
Hayati Mzee Nelson Mandela akiwa na mkewe mpya Bi Graca Machel

Mwaka 2001 Mandela aligundulika kuwa na kansa ya kibofu cha mkojo, lakini madaktari walisema ni ya kawaida hasa kwa mtu aliyekuwa na umri kama wa kwake, walimtibu kwa mionzi akapona. Baada ya kuondoka ofisini kama Rais Mandela aliendelea na kazi za usuluhishi wa migogoro maeneo mbalimbali duniani.

Mwishowe Shujaa Nelson Mandela Dunia nzima itamkumbuka kama alama ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na haki za binadamu kwa ujumla na kama kiongozi aliyeweza  kuliunganisha tena Taifa lililokuwa limegawanyika vibaya kwa siasa za kibaguzi.


Mtoto wa kiume aliyepewa jina la Mleta matata “Troublemaker “  anageuka na kuwa Mleta amani na matumaini “Peace maker” wa karne nzima ya 20.

0 Response to "WE WILL MISS YOU MANDELA: KAMA ALIVYOIMBA CHICCO 1987 WE MISS YOU MANELO” KWELI TUTAMKOSA MANDELA."

Post a Comment