Kiongozi wa Timu, Dk Ellen Otaru Okoedion
akiongea wakati wa uzinduzi wa tovuti hiyo
|
Wajasiriamali wazawa sasa wanaweza kurasimisha biashara zao kwa urahisi, ziwe ndogo au kubwa, baada ya kuanzishwa kwa tovuti iliyosheheni taratibu za kufuata pamoja na hati muhimu za kisheria zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ambazo ujazwa kabla ya kurasimisha biashara.
Tovuti hiyo - www.fanyabiasharatanzania.com – ni zao la Timu ya
Tanzania ya mwaka 2013 katika Programu ya Maendeleo ya Sekta Binafsi iliyopewa
mafunzo na Serikali ya Sweden kupitia shirika lake la Sida, ikishirikiana na
SIPU International na Jarskog Konsult kwenye masuala ya Mkakati wa Usimamizi wa
Biashara na ukuaji wa sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa mahafali na uzinduzi wa tovuti hiyo,
Kiongozi wa Timu, Dk Ellen Otaru Okoedion alisema tovuti hiyo imetengenezwa na
timu ya wajasiriamali wa Kitanzania na wawakilishi kutoka sekta ya umma chini
ya mpango wa PSD, unaolenga kuwasaidia wajasiriamali wazawa na watu wengine
wanaojihusisha na biashara kupata taarifa mbali mbali muhimu zakuendeleza
biashara zao.
“Hii tovuti itawaokolea muda wao, fedha na nguvu zao katika
kutafuta taarifa ambazo mara nyingi utawanyika, na kutopatikana kwa urahisi na
mara nyingi mjasiriamali ulazimika kutumia gharama kubwa kukusanya taarifa
hizi,” alisema.
Uanzishwaji wa tovuti hiyo ni hatua ya kuhamasisha ukuaji wa
biashara ndogo, wakati huohuo kuunga mkono jitihada za Serikali katika
kurasimisha biashara hizo, ambazo uhamasisha si tu biashara kuwa na ushindani
ndani ya nchi, kanda na kimataifa, lakini pia kuongeza mapato ya serikali
kupitia kodi.
Tovuti hiyo ina taarifa zote muhimu zinazohitajika kuanza,
kusajili na kupanua biashara nchini Tanzania. Pia imeunganishwa moja kwa moja
na mfumo wa wizara zote muhimu, mashirika na sekta binafsi. Pia imetoa
maelekezo ya jinsi ya kujaza fomu za usajili wa biashara zinatolewa na Wakala
wa Usajili wa Biashara na Utoaji Leseni (BRELA).
Chanzo Mwananchi.
0 Response to "HAYA WAJASIRIAMALI CHANGAMKIENI FURSA TOVUTI YENU HII HAPA"
Post a Comment